{"id":563879,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/563879/?format=json","text_counter":144,"type":"speech","speaker_name":"Sen. Muthama","speaker_title":"","speaker":{"id":96,"legal_name":"Johnson Nduya Muthama","slug":"johnson-muthama"},"content":"Bw. Spika wa Muda, ninashukuru sana kwa nafasi hii ili nichangie Hoja hii ambayo ni ya maana sana. Matukio au vituko haviishi katika taifa letu. Kutoka mwaka wa 1963 tuliponyakua Uhuru, majukumu fulani yalipewa kipaumbele. Haya ni elimu, maji na umasikini. Jinsi tulivyo sasa ni dhahiri kwamba taifa hili linarudi nyuma. Kamwe hatuendi mbele. Ukigusia mambo ya elimu ni shida tupu. Walimu hawatoshi na wale walioko wanadai malipo zaidi. Waziri mhusika ameweka miguu katikati; hatembei wala hasimami. Zaidi ya hayo, swala la ukosefu wa usalama linajitokeza; linawavuta na kuwatoa walimu wachache kutoka sehemu ambazo wanahitajika sana. Tume ya kuwaajiri Walimu nchini ndio ya kwanza kusema, “Ondokeni!” Bw. Spika wa Muda, niliangalia juzi wakati walimu walipokuwa wakiajiriwa. Niliona Serikali ya Jubilee ikitapatapa na kujidai kwamba inaajiri walimu zaidi, ilhali tunajua kwamba nafasi za walimu ambazo tunahitaji kujaza ni 87,749. Serikali ya Jubilee imetangaza kwamba itaajiri walimu 5,000 peke yake, wala haifikirii miaka miwili, 10 au 20 ijayo. Makadirio ni kwamba ukiajiri walimu 5,000 kila mwaka, itachukua takriban miaka 16a ndipo tutimize idadi ya walimu 87,749 inayohitajika. Hiyo Serikali ambayo inaajiri walimu kiasi hicho, inatumia Kshs24 bilioni kununua vipakatalishi vya watoto wa darasa la kwanza. Sasa unashindwa kuelewa kama hii nchi ina viongozi ambao wanapanga mambo hayo. Ni nani anahitaji profesa kumwambia hizi hesabu zinaenda nyuma? Kando na hayo, kuna Kshs17 bilioni zingine ambazo zinatakiwa kutumika mwaka huu kugharamia usimamizi wa madarasa ambayo hayana watoto. Kisha tunasema tunamaliza umasikini katika taifa letu. Tumeongea nje na ndani ya Bunge na hata katika Bunge lililopita. Viongozi wa taifa hili waache ubwanyenye na kujitajirisha. Bw. Spika wa Muda, tuko katika njia panda. Serikali ya leo haiangalii uekezaji kwa niaba ya Wakenya lakini inaangalia kandarasi na biashara. Katika ujenzi wa reli ambapo kuna pesa nyingi, wana Jubilee wote wanakimbia bila viatu wakiwa na kalamu mikononi kuenda kuweka sahihi kwa kandarasi ya kutoa marupurupu. Ukijitokeza na useme tunataka shule za watoto wetu zijengwe na walimu waajiriwe, hawataki. The electronic version of the Senate Hansard Report is for information purposes only. A certified version of this Report can be obtained from the Hansard Editor, Senate."}