{"id":610533,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/610533/?format=json","text_counter":144,"type":"speech","speaker_name":"Hon. Chea","speaker_title":"","speaker":{"id":1694,"legal_name":"Mwinga Gunga Chea","slug":"mwinga-gunga-chea"},"content":"Hizi ndizo baadhi za taasisi ambazo zilikuwa zikitumiwa na watu kuangalia mambo hapa na pale ili kuhakikisha ya kwamba wamepeana habari ya jinsi mkoloni alivyokuwa anapanga kunyanyasa Wakenya. Taasisi hizi zimeachwa nyuma. Wale wazee ambao wanakaa ndani ya zile kaya wanateseka na taasisi hizi pia zimeachwa nyuma. Zingine zinachukuliwa na watu ambao wanachukua ardhi ilhali serikali tofauti tofauti hazijaingilia kati na kuchukua hatua. Ni kweli watu walienda mahakamani na kuna malipo ambayo yalitoka na kuna wale ambao walilipwa na wengine hawajalipwa. Kile ambacho ningehimiza ni kwamba mbali na mahakama, Serikali yetu ya Kenya, ambayo tuko na imani nayo, kwa hakika inaweza kufanya jambo fulani kuhakikisha kwamba familia hizi, watu hawa na taasisi ambazo zilipigania uhuru huu pia zinaangaliwa. Jambo hilo likifanyika tutakuwa tumeanza safari nzuri. Kwa kumalizia, hata tukiangalia swala la wale waliopigania uhuru ambapo sasa tumekaa hapa na tunaendelea kufaidi, kuna baadhi ya mambo ambayo pia hukera. Nakumbuka tukiingia Bunge na nimefurahi kuona Mheshimiwa Mustafa Idd, alileta Hoja ya baadhi ya watu ambao husaidia Serikali kufanya kazi yake. Huu ulikuwa ni Mswada kuhusu wazee wa vijiji. Hawa ni watu ambao wanafanya kazi ya kusaidia Serikali hasa za utawala kuhakikisha mambo yanaenda sawa."}