{"id":624479,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/624479/?format=json","text_counter":166,"type":"speech","speaker_name":"Hon. Mwadeghu","speaker_title":"","speaker":{"id":98,"legal_name":"Thomas Ludindi Mwadeghu","slug":"thomas-mwadeghu"},"content":"La muhimu ni kwamba sukari inatumika kwa njia ya kawaida na takriban watu wote humu nchini. Tukiwa na upungufu wa sukari, utasikia kelele kutoka pembe zote za nchini hii. Tukiwa na mapendekezo yanayoweza kuiboresha sekta ya sukari nchini, ni bora kuyatoa. Inastaajabisha kwamba hata fedha zikitengewa shughuli ya kuboresha viwanda vya sukari, punde tu zinapowasili kwenye kampuni husika, pesa hizo hupotea. Kampuni ambayo ilikuwa maarufu wakati nilipokuwa chuoni na wakati nilipoanza kufanya kazi ni kampuni ya Sukari ya Mumias. Kampuni hiyo ilikuwa imebobea enzi hizo; kila mtu alikuwa akiisifu. Hivi leo kila mtu anastaajabu ni kitu gani kimetokea katika kampuni hiyo ndiyo ikajikuta katika hali yake ya hivi sasa. Sababu ni ufisadi na wizi ama ni utendakazi duni? Sababu ni sukari yenye bei rahisi inayoingizwa nchini? Wakati umefika wa kujiuliza ni lini tutahakikisha kwamba viwanda vya sukari ambavyo tumevianzisha humu nchini vimeimarika na kutimiza malengo na matakwa ya wananchi."}