{"id":640083,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/640083/?format=json","text_counter":224,"type":"speech","speaker_name":"Hon. (Ms.) Wanyama","speaker_title":"","speaker":{"id":1076,"legal_name":"Janet Nangabo Wanyama","slug":"janet-nangabo-wanyama"},"content":"Mwenzangu ambaye aliwania kiti katika eneo la Endebes, Jenipher Masis, pia ameathirika na ugonjwa huo wa saratani. Tunapojadiliana katika Bunge hili, lazima tuhakikishe kwamba Serikali imetekeleza kulingana na vile sisi viongozi tunataka katika Bunge hili. Tunaweza kuongea hapa na baada ya kuongea, hakuna kitu chochote kinachotendeka. Najua kwamba Serikali imesikia na itahakikisha kwamba imetilia maanani maoni yetu na inatekeleza maneno haya ya saratani katika nchi yetu ya Kenya. Namshukuru dadangu, Mhe. Wanga, kwa sababu watu wanalia katika nchi yetu ya Kenya, hasa akina mama ambao wanakatwa matiti yao wakiwa bado wangali wachanga. Hawawezi kuwanyonyesha watoto wao kwa ajili ya ugonjwa wa saratani ya matiti. Wenzangu wengi wameongea kuhusu ugonjwa wa saratani. Watu ambao wanakufa ni karibu 18,000 na wale wameathirika kwa sasa ni 82,000. Hii ni idadi kubwa sana. Tunaomba Serikali ihakikishe kwamba inawahamasisha watu kuhusu ugonjwa wa saratani katika nchi yetu ya Kenya. Namuunga mkono Mhe. Wanga aliposema kwamba tunatakikana tuwe na afisa mmoja katika kaunti. Afisa mmoja hatatosha. Tunapaswa tuwe na afisa katika kila wodi katika nchi yetu ya Kenya, ili wahamasishe watu kuhusu ugonjwa wa saratani. Sio hayo tu, kuna magonjwa mengi ambayo Wabunge wenzangu wameyasema hapa. Kuna ugonjwa wa Ukimwi. Siku hizi, wengi wakiambukizwa ugonjwa wa Ukimwi au saratani, wanafikiria wamerogwa. Nataka kuwaambia wale walioathirika na hata wale ambao bado hawajaathirika wahakikishe kwamba wametafuta matibabu kwa wakati unaotakikana. Kuna wagonjwa tuliowachangia, lakini kuna wengi ambao hatujawachangia kwa sababu hawajatufikia sisi kama viongozi. Tunawachangia wale ambao wameangaziwa. Asilimia kubwa sana hawatufikii sisi viongozi au hata hospitali kuhakikisha kwamba wamepata nafasi ya kupata matibabu. Pesa ambazo zimeenda katika kaunti zetu, na haswa zile ambazo zimeenda upande wa afya, hazijwasaidia watu mashinani. Ndiposa viongozi wa kutoka eneo langu tulikuwa tunawaza kwamba sekta ya afya inapaswa kurudishwa katika Serikali kuu ili kuhakikisha kwamba watu wanapata nafasi ya kufikia matibabu kwa wakati unaotakikana. Heko dadangu, Mhe. Wanga, kwa kuleta Hoja hii katika Bunge hili. Nawaomba Wabunge wenzangu tuipitishe."}