{"id":680613,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/680613/?format=json","text_counter":493,"type":"speech","speaker_name":"Hon. Bady","speaker_title":"","speaker":{"id":1612,"legal_name":"Bady Twalib Bady","slug":"bady-twalib-bady"},"content":"kuwa hawatafurushwa kabla ya kujua watakachofanya. Ni muhimu kuwa wanapojulishwa, Kamati izingatie uhalali wao kwa sababu kule Mombasa kuna watu wanaoishi mahali na mikataba ya kupangisha yana mtu mwingine. Ni vile tu hakuwatoa mahali pale. Kwa hivyo, ni muhimu uhalali uangaliwe ili mikataba ya kupangisha yakiisha, mashamba yarejeshewe wenyewe badala ya kuyarejesha kiholela. Ni muhimu kuzingatia mambo haya na kuhakikisa kuwa wenyeji wanapewa haki yao. Tulihakikisha kuwa dhuluma za kihistoria zimeshughulikiwa na Mwenyekiti ametaja mambo yote katika maeneo haya. Vile vile, Hoja hii imehusisha watu wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi na inafafanua jinsi ya kushughulikia dhuluma za kihistoria. Kipengele cha 97 kinazungumzia hali itakayozingatiwa kabla ya watu hao kufurushwa. Sheria inasema kuwa watu wakikaa mahali zaidi ya miaka kumi na miwili, wana haki ya kusema hapo ni kwao. Kupitishwa kwa Hoja hii kutatupa sisi afueni. Kwa mfano, pale Jomvu, kuna watu ambao wameishi pale Alidina kwa muda wa zaidi miaka 40. Ninaona Mwenyekiti anafurahia kwa sababu anaelewa hali hiyo na tutaendelea kuishughulikia. Nina hakika kuwa watu hawa watapata afueni. Ningependa kupongeza juhudi za Kamati. Hivi juzi, Kamati hii ya Ardhi ilikuwa kule Miritini. Kama nilivyosema hapo awali, kuna mradi wa Standard Gauge Railway (SGR) na ule wa barabara ya Dongo Kundu, na wananchi wangu wanafanyiwa kipimo cha nyumba, lakini si cha ardhi. Mwenyekiti alifika pale na kuwapa moyo sana kuwa mambo hayo yalifanywa kinyume na sheria. Kamati, vile vile, ilifanya tathmini ya mahali pale. Walisema kuwa si sawa watu kuondolewa kwenye ardhi bila kulipwa fidia. Kwa mfano, ikiwa mtu ameishi pale kwa miaka 20 au 25, kumfanyia fidia ya nyumba ya udongo kwa sababu yeye ni maskini si sawa, na kumlipa Ksh25,000, Ksh30,000 au Ksh50,000 haiwezi kujenga nyumba mahali pengine akaweza kuishi. Kamati ilishughulikia mambo haya kwa kidete na kusema kuwa watu wenye barua ya kumiliki shamba wanafaa kupewa hati miliki kwa sababu barua hizo zinaonyesha dhahiri kuwa wao ndio wenye ardhi. Fidia ya ardhi sharti iangaliwe mwanzo. Ningependa kumshukuru Mhe. Mwiru kwa juhudi zake. Ningependa kuondoa tetezi na ninazungumza bila kuogopa kuwa watu wa Pwani hawakupewa nafasi. Tulichangia Hoja hii na ikaungwa mkono, kupitia kwa Mwenyekiti, kuhakikisha kuwa mapendekezo yetu yaliletwa. Ikiwa kutakuwa na tetezi yoyote, tutashirikiana na Kamati hii ya Pamoja ya Uwiano kuangalia jinsi ya kuzitatua shida za watu wa Pwani. Matatizo yako zaidi kwa wale ambao wana barua ya kumiliki mashamba lakini hawajapewa hati miliki. Kama wenzangu walivyosema, mtu atapata usingizi pale atakapopewa hati miliki ya ardhi. Hati miliki itamwezesha kusema kuwa habanduki mahali pale kwa sababu ni shamba lake."}