{"id":806087,"url":"http://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/806087/?format=json","text_counter":150,"type":"speech","speaker_name":"Sen. Faki","speaker_title":"","speaker":{"id":13211,"legal_name":"Mohamed Faki Mwinyihaji","slug":"mohamed-faki-mwinyihaji-2"},"content":"Asante Bw. Naibu Spika kwa kunipa fursa hii kuomboleza na familia, ndugu, marafiki, wakaazi na wapiga kura wa Migori, Spika wa Seneti pamoja na Maseneta wote wa Jamhuri ya Kenya kutokana n akifo cha mwenzetu, Mheshimiwa, Sen. Ben Oluoch Okello. Sen. Ben Oluoch alikuwa ni Seneta wa mara ya kwanza kama mimi na wengine ambao tuko hapa na kwa hivyo, kifo chake ni pigo kwetu pamoja na Seneti nzima ya Jamhuri ya Kenya. Bw. Naibu Spika, nilimjua Sen. Ben Okello wakati tulipoingia mara ya kwanza katika Bunge la Seneti mnamo mwezi wa sita, mwaka wa elfu mbili na kumi na saba. Kwa kauli, alikuwa ni mtu mkimya lakini mwenye tajiriba kubwa kama mwanahabari na msimamizi wa show ya Ramogi Radio ambayo iko katika kundi la redio za kienyeji katika nchi yetu ya Kenya. kifo chake kinatukumbusha kwamba ugonjwa wa saratani umekuwa ni adui mkubwa katika Jamhuri yetu ya Kenya. Mawazo yangu yako na wanaougua ugonjwa huu na hawana huwezo wa kupata matibabu kama aliyoyapata mwendazake, Sen. Ben Okello Oluoch. Mawazo yangu pia yako katika familia ambazo zinauguza wagonjwa wa saratani katika hali tofauti tofauti, iwapo ni saratani ya koo, ya titi, ya tumbo na mengineo ambayo yanaathiri Wakenya kwa jumla. Hivyo basi, iko haja ya Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba tunakinga magonjwa ya saratani kuliko kutibu kwa sababu tumeona kwamba kuyatibu ni ghali na Wakenya wengi hawapati fursa ya kupata matibabu ya kisasa ambayo yata hakikisha kwamba ugonjwa huu unaangamizwa. Inabidi Serikali itoe mikakati ya kuhakikisha kwamba tunalindwa na kujikinga na saratani kuliko ilivyo sasa. Kwa mfano, moja ya kinga ya saratani ni kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kuhakikisha mwili unapata mazoezi. Hili ni jambo moja ambalo Serikali inaweza kufanya ili kuhakikisha kwamba watu wanahimizwa kufanya mazoezi ya mwili ili kujikinga na saratani. Habari zilikoko katika vyombo vya habari ni kwamba ile sukari ambayo iliingizwa katika nchi ya Kenya imepatikana na viini vya saratani. Ni lazima Kenya Plant Health Inspectorate Services (KEPHIS) ambayo inachunguza bidhaa zote zinazoingia katika nchi ya Kenya iwe macho kuhakikisha kwamba hatuingizi vyakula ambavyo vitakuja dhuru afya za Wakenya. Hii ni kama kujipa sumu, iwapo shirika kama hili halitafanya kazi yake kuhakikisha kwamba chakula kinachoingia katika nchi ya Kenya ni salama kwa matumizi ya binadamu na hata mifugo watakaokila. Bw. Spika, mpira uko katika mikono ya Serikali kuhakikisha kwamba ina linda maisha ya Wakenya na kwamba, chakula kinacholiwa ni safi kwa mwanadamu na Wanyama. Vilevile, ihakikishe kwamba Wakenya tunapata huduma sawa sawa za afya ili magonjwa kama haya yasiwe donda ndugu katika nchi yetu. Tunapo omboleza na ndugu zetu wa Kaunti ya Migori na wengineo ambao wameathirika na maradhi ya saratani, ni jukumu letu kama Wabunge kusaidia Serikali kuweka mikakati ya kutosha ili kuhakikisha kwamba Wakenya wako salama kutokana na magonjwa kama hayo. The electronic version of the Senate Hansard Report is for information purposes only. A certified version of this Report can be obtained from the Hansard Editor, Senate"}