GET /api/v0.1/hansard/entries/101440/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 101440,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/101440/?format=api",
    "text_counter": 256,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Muthama",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 96,
        "legal_name": "Johnson Nduya Muthama",
        "slug": "johnson-muthama"
    },
    "content": "Asante sana, Bwana Naibu Spika wa Muda. Nami nasimama kuchangia Mswada huu ambao ni wa maana sana na unahusu watu na watoto wetu. Huu ni Mswada ulioletwa na Mheshimiwa Ms. Odhiambo kuhusu ulanguzi wa binadamu. Ni dhahiri kwamba jambo hili limekuwa jambo la kuudhi sana, la kusikitisha na la kuumiza sana, hasa katika Bara letu la Afrika. Jambo la kuhuzunisha mno ni kwamba ulanguzi unapotokea, hautokei kwa njia ya utumwa peke yake. Hautokei kwa njia ya kulazimishwa. Ni madhara makubwa sana ambayo yanawahusu watu ambao waliumbwa na Mungu na wanastahili kuishi katika sheria zao. Mambo yaliyotajwa hapa ni mazito sana. Tumeona katika vyombo vya habari mambo ambayo yanaendelea. Yanahusu watu wetu ambao wameenda nje kufanya kazi. Watu hao huenda huko na kufanywa watumwa. Taifa hili lilipigania Uhuru ili liweze kujitawala. Kujitawala ni kuangalia na kuona kwamba maadili ya maisha ya mtu yanaendelea kulingana na sheria zilizowekwa na Mwenyezi Mungu. Hapo zamani, Waafrika walitezeka. Waliuzwa na kufungwa na minyororo kama ng’ombe na kutumika. Hadi leo, baada ya kupigania Uhuru, Taifa hili linashuhudia mambo haya. Haiwezekani kutokuwa na sheria ya kulinda haki za kibinadamu. Tulikuwa tunadhani mambo haya yanatendeka katika nchi za nje. Lakini katika nchi yetu, mambo haya yanaendelea kutendeka. Tumeshuhudia visa vya watoto wa miaka kati ya minane na kumi. Ulanguzi sio lazima upitie katika mipaka. Hata ule wa ndani ni ulanguzi. Tumeona na tumeshuhudia watoto wa kike wakiozwa kwa lazima. Wanachukuliwa kwa lazima, wanatekwa nyara, wanafungiwa kwa nyumba na kutendewa madhambi ambayo hayafai kuonekana. Mambo haya yanafanyika katika nchi huru ambayo ina sheria. Bwana Naibu Spika wa Muda, hakuna kitu kibaya kama kuona mtoto wa miaka nane ama kumi wa kike akiwa amechukuliwa na mtu mzima na kuolewa - na hata mahari yamelipwa kwa wazazi wake - na sheria haitumiki. Sheria hii inafaa iwekwe ili iwalinde wale walio na nguvu na wanyonge ili usawa uonekana. Hatutaki kusikia kuna jamii moja inabaguliwa na nyingine inatunzwa. Serikali inafaa kuangalia na kuingilia mambo ya wale ambao wanateseka kwa sababu ya umaskini. Hivi leo, tuna wakimbiziki wa kisiasa wa ndani. Watoto wa watu hao wanalala nje na hawana mahala pa kwenda. Wengi wao hawaendi shule. Wakati umefika wa kuangalia maisha ya Wakenya ili watoto wao wasije wakawa vile vile. Hicho ni kizingizio na wanaweza kuanguka katika ule mtego wa kuenda nje kuuzwa na kutendewa matendo mabaya. Serikali inaweza kujimudu na kuwasaidia watu masikini na watoto ambao nia yao ni kusoma ili waweze kujikimu na kuwa kama Wakenya wengine. Tukiangalia mambo ya nje na pia yale ya ndani, inafaa tuhakikishe waliopo hapa wameshughulikiwa. Sisi kama wazazi tunateseka na mambo haya. Yanatuudhi! Lakini ukweli ni kwamba akina mama wanaumwa sana kwa sababu wao ndio walio na mzigo mkubwa sana. Kama Waswahili walivyosema: “Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi.” Akina mama wanateseka sana na wao ndio watu ambao wanapatikana katika mambo yanayoudhi na kutatanisha maisha ya binadamu. Naunga mkono sheria hii. Nasema kwamba ipite kwa dhati na iangalie kabisa na kuona kwamba katika makadirio ya bajeti ya Serikali, kuna kiwango kilichowekwa cha kuwasaidia watoto ambao ni masikini ili wasije wakaingia katika mtego wa kuuzwa nje, kupelekwa nje na kuolewa kwa lazima. Kwa hayo machache, naunga mkono."
}