GET /api/v0.1/hansard/entries/110717/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 110717,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/110717/?format=api",
    "text_counter": 407,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Mwakulegwa",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 101,
        "legal_name": "Danson Mwazo Mwakulegwa",
        "slug": "danson-mwazo"
    },
    "content": "Asante Bw. Naibu Spika kwa kunipatia nafasi hii ili mimi pia nitoe mchango wangu kuhusu Katiba tunayoitengenezea Wananchi wa Kenya. Kwanza, tumechukua muda mrefu kutengeneza Katiba hii na wakati ni sasa na Bunge la Kumi lina nafasi ya kuweka historia kwamba tumewasaidia Wakenya kuwa na uongozi mpya na Katiba mpya. Bw. Naibu Spika, Ninapoangalia katiba, mambo ya uzito ni mawili, kwamba katiba ni kuangalia uongozi wa siasa na utawala, na ya pili, ugawaji wa rasilmali ya nchi hii. Kwa hivyo, kila wakati tumezungumza na kila wakati wa uchaguzi kumekuwa na utata kuanzia mwaka wa 1992, kwa sababu tunaamini kama Wakenya kwamba Rais akitoka kwa jamii yako, basi rasilmali zitakuja kwako. Hiyo ndiyo maana tumekuwa na utata, na hata mwaka wa 2007 kukawa na umwagikaji wa damu kwa sababu tunapiga kura kwa jamii kwa sababu rasilmali zitakuja kwa jamii yako. Tuna nafasi nzuri ya kurekebisha mambo haya. Makabila yote ya Kenya yameumbwa na Mwenyezi Mungu kuwa hapa kama Wakenya. Hata uwe Mtaita, wewe ni Mkenya na ujivunie kuwa Mkenya. Demokrasia inasema kwamba, wengi wape lakini wale wachache wapate haki yao. Mimi naangazia mambo mawili katika Katiba hii; uongozi wa siasa, wengi watachukuwa. Lakini wale wachache pia wapate rasilmali sawa na wale wengi. Tukifanya hivyo, uongozi na Serikali ile inaweza kutusaidia kutekeleza mambo hayo ni Serikali ya ngazi tatu. Serikali ya Kitaifa, Serikali ya Mikoa na Serikali ya Wilaya. Kwa nini ninasema ngazi tatu? Ni kwa sababu kwa hii miaka 47 tunaangalia serikali ya kitaifa ambayo inagawa rasilmali zote; iwe ni barabara hata mashamba, zote zinatolewa na Serikali ya Kitaifa. Ndiyo maana kumekuwa na utata nchini Kenya. Kumekuwa na wale wachache wakisema: “Keki hii yaliwa na wachache”. Wale wachache hawawezi kupata nafasi ya kuweka Rais pale. Ndiyo maana ninasema kwamba, tukienda katika Serikali ya ngazi tatu na tuwape mamlaka kila ngazi; kwamba ngazi ya katikati kama ni ya mikoa, iwe na nafasi ya kuangalia rasilmali za mikoa kama vile mashamba na rasilimali zingine zote. Basi ile wilaya pia itakuwa na nafasi ya kuchunga mali yao. Kama ni mashamba yao, au maji. Bw. Naibu Spika, tukifanya hivyo na tugawe kwa usawa, mambo ya lazima kwamba Rais atoke katika jamii yangu haitakuwa tena na nguvu maanake hata mimi ninayetoka kwa jamii ndogo ninajua haki yangu naishikilia mimi, na rasilmali zangu nazichunga mimi. Kwa hivyo, ni muhimu sana. Tunapozungumza tuwe na ngazi tatu katika mamlaka ya kujiongoza sio eti Serikali ya kitaifa inapuuzwa; hapana. Itakuwa na mamlaka yake. Serikali ya mikoa itakuwa na mamlaka yake na Serikali ya wilaya ni ya jamii ya wananchi wanaoishi katika wilaya ile pia wawe na msingi wa kujitawala. Jambo lingine ni kwamba, tusipokubali kwamba sisi ni watu tofauti na jamii mbali mbali; tukiwa hapa tunasema sisi ni Wakenya, lakini tukitoka nje, kila mtu anazungumzia kabila lake, itakuwa ni vizuri tukubali sisi ni watu mbali mbali na tugawe mali katika hali hiyo. Pia, katika Katiba Kielelezo ambayo tunaizungumzia hivi sasa, ukiangalia kipengee cha 89 kinasema kwamba, uwakilishi Bunge kwa sasa utagawanywa kulingana na idadi ya watu. Kwa mfano, kama tuko milioni 40 na maeneo Bunge mia 290 inaonekana taratibu ni kwamba kila eneo Bunge liwe na watu 138,000. Kwa hivyo, tukitumia idadi hiyo, kuna maeneo Bunge mengi sana ambayo yatapotea katika ramani ya Kenya. Kwa mfano, kule Pwani tukitumia idadi hiyo, kuna maeneo Bunge saba yatakayopotea. Kwa hivyo, tunasema kwamba, kama tutatumia idadi ya watu, tutumie idadi ya watu kulingana na misingi mitatu. Msingi wa kwanza ni maeneo katika miji mikuu, ya pili ni maeneo kwa watu wengi na ya tatu ni maeneo ambapo kuna idadi ndogo ya watu lakini yana eneo kubwa la ardhi. Tukifanya hivyo, tutakuwa na usawa. Maanake, tukitumia idadi ya watu pekee yake, baada ya miaka nane ama 12, basi tutakuta maeneo Bunge fulani yatakuwa yanaondoka katika ramani ya Kenya, na wale wengi wataendelea kujiongezea viti vya Bunge. Kwa hivyo, hapo ndipo tunasema haitakuwa ni sawa. Wachache pia ni Wakenya, wasikizwe na waishi katika nchi hii katika hali ya ustaraabu na raha wanazopata kama Mwanakenya mwingine."
}