GET /api/v0.1/hansard/entries/1119391/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 1119391,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1119391/?format=api",
"text_counter": 68,
"type": "other",
"speaker_name": "",
"speaker_title": "",
"speaker": null,
"content": "Hii inaonyesha kwamba hapa Kenya hakuna haki. Mnyonge msonge. Hakuna haki kabisa kwa sababu itakuwaje watu waliofanya kazi zao sawa sawa wakaonyesha kwamba mambo yote yako sawa kwa upande wao wanapoteza kazi zao wakati wale ambao walipokea pesa nyingi, mabilioni, wanaendelea na shughuli zao bila shida yeyote. Bi Spika wa Muda, kazi ya madawa inayofanyika na KEMSA sio kazi ambayo unaweza peleka mtu yoyote kwenda kufanya pale. Ni kazi ambayo inahitaji ujuzi fulani na hatuwezi kuchukua askari wa National Youth Service (NYS) tukawapeleka kufanya kazi hiyo. Hatuwezi kuchukua askari wa jeshi ambao kazi yao kubwa ni ulinzi tukawapeleka kwenda kufanya kazi hii. Bi Spika wa Muda mabilioni yamepotea tayari kwa zabuni gushi na vile vile pia bidhaa gushi ambazo zililetwa KEMSA. Na vile vile kuna wengine ambao mpaka sasa hawajalipwa kwa hizo bidhaa zao gushi. Hii itatumika kama njia ya kuziba haya mapengo ili wale ambao walitakikana kulipwa walipwe halafu wale ambao watapata hasara ni wafanya kazi wadogo wadogo ambao wamefanya kazi yao bila matatizo yoyote. Bi Spika wa Muda, iwapo hawa wafanyakazi watafutwa kazi, wote itabidi waende mahakamani kudai haki zao na itabidi Serikali ilipe mabilioni ya pesa ili kuhakikisha wale wamepata haki kama watakavyoamrishwa na mahakama. Kwa hivyo badala na kupambana na lile swala la ufisadi lililokuwepo katika KEMSA Serikali inatumia mbinu mbadala kuweza kuziba matatizo hayo ili kuonekana kwamba mambo yote yako sawa na kuwadanganya wafadhili kwamba kila kitu kiko sawa. Haiwezekani katika karne hii wanyonge kunyongwa katika KEMSA wakati Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa liko hapa kutetea masilahi ya wananchi wanyonge katika nchi yetu ya Kenya. Bi Spika wa Muda, ijapokuwa swala hili utalipeleka kwa kamati, mimi naomba utoe amri kwamba Waziri wa Afya, aje hapa katika Bunge la Seneti wiki ijayo ili tumuhoji atueleze sababu gani hawa watu wamepelekwa likizo ya lazima, kwa sababu gani hawa watu wameambiwa wafanye kazi nyumbani; na je, ni sawa sasa kila sekta ipewe jeshi, wakati sisi tunajua jeshi linapata shida Somalia? Tunajua katika jeshi pia kuna mambo ya zabuni na wao pia ni wafisadi zaidi kuliko sehemu yeyote ingine katika nchi yetu. Kwa hivyo, si sawa kupeleka hili jambo kwa kamati halafu ikalaliwe kwa sababu tayari kuna repoti ya KEMSA huko. Zaidi ya miezi miwili ripoti hio haijajaduliwa. Mwenye kiti haonekani bungeni kupeleka ripoti yake mbele izungumziwe. Nimefurahi kwamba Sen. Sakaja amekuwa hapa wiki nzima na ameweza kupeleka mbele ripoti yake lakini wenye viti wengine wa kamati hawana shughuli ya kuweza kusukuma ripoti zao ziweze kusikizwa na yale mapendekezo yao yaweze kukubaliwa na Bunge ili tuweze kusonga mbele. Katika kumalizia nasema kwamba Waziri aitwe hapa na bodi mpya ya KEMSA ije hapa watuambie ni kigezo gani wametumia kuwapeleka nyumbani hawa wafanya kazi 900 wakati wale wahusika na zabuni nyengine kabisa. Asante."
}