GET /api/v0.1/hansard/entries/1186470/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 1186470,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1186470/?format=api",
"text_counter": 276,
"type": "speech",
"speaker_name": "Kuria East, UDA",
"speaker_title": "Hon. Maisori Kemero",
"speaker": null,
"content": " Mhe. Spika wa Muda, ningependa kuchukua nafasi hii kukushukuru na vilevile kukupongeza kwa sababu tangu uwe kwenye kiti sijazungumza mbele yako. Hoja hii ni muhimu sana. Imefika bungeni wakati mwafaka. Hivi majuzi Mheshimiwa Rais alisema kuwa, ili kuongeza upanzi wa miti, atapeana stakabadhi kwa wale watakaofanya kazi hiyo kwa njia itakayoridhisha. Hivyo ni nzuri sana. Nataka kukushukuru Mhe. KJ kwa kuleta Hoja hii, kwa sababu hela zinazopeanwa katika idara hiyo ya kujenga barabara, kutengeneza au kuiboresha kwa namna yeyote ile, ni nyingi sana. Ninajua kwamba kwenye kandarasi huwa kuna kiwango cha fedha ambazo zinatengewa shughuli za kuhifadhi mazingira. Mara nyingi watu wengi wanapuuzilia mbali mambo haya kwa sababu hakuna anayejali. Tukiweka katika sheria iwe inazingatiwa kwamba mkandarasi akipewa kazi ni lazima, kuanzia siku ya kwanza, apande miti, litakuwa jambo la busara. Mipaka ya barabara inajulikana. Ikiwa barabara hiyo itachukua mwaka mmoja au miaka miwili kujengwa, kufikia wakati huo, miti hiyo itakuwa mikubwa. Masharti mengi yamewekwa hapo awali, kama vile sharti ya kupanda miti kutumia NG-CDF. Hata hivyo, watu huenda siku moja, wanapanda miti alafu wanaondoka na kuwaachia wanyama miti hiyo waiharibu. Kwa hivyo Mhe. KJ ameileta Hoja hii wakati mzuri sana. Kiangazi ambacho sasa hivi kinaikumba nchi hii kinatuonyesha umuhimu wa kulivalia njuga swala hili na kuangalia tutakachofanya ili jambo hili liweze kuwafaidi watu wote. Mhe. Spika Wa Muda, niruhusu nitumie dakika moja kuzungumzia swala la NG-CDF. Mimi sina vita vyovyote na wale ambao wanapata pato lao kwa kwenda kortini. Kuna watu wengi sana wamepata elimu yao kupitia fedha za NG-CDF. Wamekuwa mawakili na wengi wana nyadhifa za juu katika nchi hii. Inasikitisha sana kuwa baadhi yao walifaidika kutokana na ufadhili wa NG-CDF na baadaye wakajiona kuwa wametosheka na kuaanza kutafuta utajiri kwa kwenda kortini kusimamisha kila sehemu ambayo ingemfaidi mtoto maskini aweze kufikia kiwango chao. Ningependa kuhitimisha kwa kusema kuwa suala la NG-CDF haliondoki. Ingependeza kama tungetafuta njia mbadala ya kuweka fedha hizi katika sehemu ambayo haitaingiliwa tena na watu ambao wanaiona kama ni ya kuwatajirisha wabunge ilhali wabunge hao ndio wanaofanya walale usingizi mzuri. Sisi tusipopata pesa za kuwasaidia maskini, nao pia hawatalala katika nyumba zao kwa sababu watoto hawa wasipoenda shuleni watageuka kuwa majambazi na hali hiyo italeta shida katika nchi hii. Hivi sasa kuna janga kubwa la ukosefu wa usalama humu nchini. Ikiwa sasa hivi tunalia kuna ukosefu wa usalama, Nairobi haikaliki; tunataka tuongezee kwa kuwatoa watoto wetu shuleni kwa sababu hawawezi kulipa karo na kuwaweka kwenye mitaa? Tupande miti na tulipie watoto wetu karo. Hazina ya NG-CDF iendelee na tufanye hayo maendeleo mengine yote ili nchi hii iweze kuwa bora. Ahsante Mhe. Spika wa Mda."
}