GET /api/v0.1/hansard/entries/1194751/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 1194751,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1194751/?format=api",
    "text_counter": 66,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Ilani",
    "speaker_title": "",
    "speaker": null,
    "content": "wanaojifanya kuwa wazungu katika nchi zao. Lugha ya Kiswahili, ambayo inapaswa kuunganisha Wakenya, haiheshimiwi, haipewi hadhi yoyote, na imedharauliwa sana na watu wachache. Leo hii Kenya ina mayatima wa lugha ya Kiswahili, lugha ya uzalendo. Kuna ukabila Kenya kwa sababu tumekubali lugha zingine ziteke nyara lugha adhimu ya Kiswahili; lugha teule ya kitaifa ambayo sasa inatumiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ukabila utaisha katika nchi hii wakati ambapo sote, kwa kauli moja, tutakubali kuzungumza lugha hii adhimu ya Kiswahili, inayounganisha kila mtu. Mfano mzuri ni wanasiasa tunapoenda kufanya kampeni Mashinani tukiomba viti mbali mbali, hatutumii Kiingereza, kwa sababu tunajua hatutafua dafu. Tunajua vyema kuwa sera tunazouza hazitaeleweka zikiuzwa kwa lugha ya Kiingereza. Tunapofika mashinani, sisi hupiga siasa na kuomba kura kwa lugha ya Kiswahili. Lakini pindi tu tunapoapishwa na kuvaa masuti na kuja katika Bunge hili, tunajifanya wazungu zaidi ya wazungu wenyewe. Kiswahili kimedharauliwa hadi shule za kibinafsi ambazo hazifunzi lugha hii. Leo utakutana na vijana na wazee ambao ukiwazungumzia kwa Kiswahili, wanakwambia, e xcuseme; kwa kuwa hawaelewi lugha ya kitaifa ya Kiswahili. Leo hii, unapozungumza Kiswahili au kuomba kazi kwa lugha hii, unaonekana kuwa mjinga kwa sababu hujui lugha ya Kimombo. Huo ni ukoloni mamboleo. Tunapozidi kudharua lugha hii, ndivyo tunavyozidi kujidharau wenyewe kama Wafrika kwa kukataa lugha yetu. Lugha hii ni adhimu, na ndio lugha tamu duniani. Ukienda Ujerumani, Marekani na kote duniani, wote wanajifunza lugha ya Kiswahili. Mwaka uliopita, Afrika Kusini walijadiliana kuifanya Kiswahili lugha ya Afrika nzima. Lakini sisi wenye lugha ambayo ni kiio cha jamii ya Afrika, hatutaki kutumia lugha hii vizuri ili iweze kuunganisha Afrika yote. Lugha hii inaunganisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na ya Kati. Sasa hivi Jumuiya ya Afrika imekuwa kubwa. Kama alivyosema mwenzangu, Mhe. Owen Baya, Marais wa mataifa mengine wakizuru nchini Kenya, wanazungumza lugha ya Kiswahili kwa sababu nchi zao zimeongozwa na mabaraza ya Kiswahili, kama vile BAKITA, ambazo zinahakisha kuwa lugha hii imeheshimika na inaendesha Mataifa hayo. Kwa mfano, nchini Tanzania, watu hujadiliana kwa Kiswahili, shule wanafunza kwa lugha ya Kiswahili; na wameunganishwa na lugha moja. Hayati Julius Kambarage Nyerere aliondoka kama ameunganisha nchi ya Tanzania, ndio maana leo hakuna ukabila katika nchi hiyo. Tanzania mtu hakuulizi wewe ni wa kabila lipi. Hapa Kenya, utaulizwa unatoka katika kabila lipi; ila Tanzania unaulizwa “Kaka, unatokea sehemu ipi ya Taifa hili?” Hii ni kwa sababu hatuna lugha ya kutuunganisha. Hatuna heshima, hatuna mapenzi na hatuelewani. Lugha inayotawala ni lugha ya Kiingereza. Bi. Spika wa Muda, hapa Kenya watu wanapozungumza Kiingereza, wanaonekana wasomi. Ila mtu asiyejua lugha yake ya taifa si msomi; ni mjinga. Ni mjinga kwa sababu haelewi lugha yake, na anataka kujilazimisha kwa lugha nyingine huku akijiona msomi. Kiingereza si elimu tosha. Mtu asiye na elimu ya lugha yake amepotoka. Hata katika mahamaka zetu, asilimia kubwa ya wanaofungwa na kuwekwa katika magereza ni watu ambao hawajui kujitetea. Hii ni kwa sababu, wanapopelekwa kizimbani, wanasomewa mashataka kwa lugha ya Kiingereza. Mara nyingi hawaelewi kinachosemwa, na wanakubali tu. Wanasikiza mawakili wao bila kujua cha kusema. Asilimia kubwa katika jela hizi zetu wamefungwa kwa lugha ya mkoloni. Wao huitikia tu pasi na kujua. Lakini, hukumu ikitolewa na majaji ambao wanaelewa lugha ya Kiswahili, itakuwa ni rahisi kwa hustler pale kizimbani kujitetea na kueleza mambo yalivyokuwa. Bi. Spika wa Muda, sitaki kunena sana, lakini ninataka kumpongeza Mhe. Yusuf kwa kuleta swala hili la Kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya. Kongole sana. Natumahi Bunge hili litapitisha na kuhakikisha kuwa nchi inaunganishwa na lugha teule ya Kiswahili. Ahsante sana, Mhe. Spika wa Muda. Naunga mkono Hoja hii."
}