GET /api/v0.1/hansard/entries/1194787/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 1194787,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1194787/?format=api",
"text_counter": 102,
"type": "speech",
"speaker_name": "Sigor, UDA",
"speaker_title": "Mhe. Peter Lochakapong",
"speaker": null,
"content": " Asante sana, Mhe.Spika wa Muda kwa nafasi hii. Naunga mkono Hoja hii ambayo imeletwa na mwenzetu Mhe. Yusuf Hassan, Mbunge wa Kamukunji, ya kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili la Kenya. Mhe. Spika wa Muda, kabla niendelee na Hoja hii, kwa sababu nimepata fursa ya kuongea mara ya kwanza katika Bunge hii ya kumi na tatu, niruhusu niwashukuru watu wa eneo Bunge la Sigor kwa kunichagua mara ya pili mfululizo. Wamenipatia nafasi ya kuwahudumia kwa mara ya pili katika Bunge hili la kitaifa. Kwa hivyo, ninawashukuru wote ambao waliniunga mkono na kunipigia kura, haswa watu wazuri wa eneo Bunge la Sigor kwa kuweka historia na kunichagua kwa mara ya pili, jambo ambalo halijawahi kufanyika katika miaka 35 iliyopita. Kwa hivyo, ninaahidi kwamba katika muhula huu ama kipindi hiki cha miaka mitano ambacho niko katika Bunge hili kuwawakilisha watu wangu wa Eneo Bunge la Sigor, nitaendeleza ile kazi nzuri ambayo tulikuwa tumeanza. Nawashukuru sana kwa nafasi hii. Nikirudi kwa Hoja iliyoko mbele yetu, ningependa kusema kwamba Kiswahili kinatambuliwa na Katiba ya Kenya kama mojawapo ya lugha za taifa. Kwa hivyo, tumechelewa kubuni Baraza hili ambalo litashughulikia mikakati, kubuni sera na kuweka utaratibu wa kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa ajili ya watu wetu. Lugha ni muhimu katika jamii. Lugha inapokuzwa inasaidia sana kuunganisha jamii na kuendeleza biashara. Jambo la muhimu ni kwamba Baraza hili litakapoweka mikakati ya kuendeleza lugha ya Kiswahili katika Jamhuri ya Kenya, watu wengi wataelewana. Hii ni kwa sababu lengo kubwa la lugha yoyote ni kuwawezesha wanaotumia lugha hiyo kuwasiliana na kuelewana. Kubuniwa kwa Baraza hili, ambalo kazi yake itakuwa ni kuhakikisha kwamba Wakenya wanaelewa, wanaongea na wanawasiliana kwa lugha ya Kiswahili, ni jambo muhimu litakalonufaisha Wakenya wote."
}