GET /api/v0.1/hansard/entries/1194794/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 1194794,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1194794/?format=api",
"text_counter": 109,
"type": "speech",
"speaker_name": "Likoni, ODM",
"speaker_title": "Mhe. Mishi Mboko",
"speaker": null,
"content": " Asante sana, Mhe. Spika wa Muda. Leo ni siku ya furaha na bashasha. Nampa kongole Mbunge wa Kamukunji kwa kuleta Hoja hii inayopendekeza kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili. Kwa hakika, pendekezo hili lingekuja kitambo sana. Lakini Waswahili wanasema kawia ufike. Hayawi hayawi, huwa. Leo tunaona kuwa mwanzo wa ngoma ni lele mama, na lele mama la kuweka Baraza Kuu la Kiswahili katika Taifa la Kenya limeanza. Tunajua pia ngoma itafika wakati mwafaka. Kwanza, tunatambua kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa. Vile vile, ni lugha rasmi ya kitaifa sawia na lugha ya Kiingereza. Ajabu ni kuwa tumeendeleza ukiritimba wa lugha ya Kiingereza ilhali lugha ni mbili – Kiingereza na Kiswahili. Kwa hivyo, jamani wakati umefika, na ni sasa. Kama si sasa, ni sasa hivi. Tuitukuze lugha yetu kwa sababu Kifungu cha 137 katika ule mkataba ama mapatano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, kimezungumzia kuwa ni lazima tuitukuze na kuiboresha lugha ya Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha ambayo inaweza kutupatia mawasiliano bora katika jumuiya yetu ya Afrika Mashariki. Tunajua kwamba katika jumuiya yetu ya Afrika Mashariki tuna mapatano mengi sana, ikiwemo mambo ya kilimo, ajira, biashara, mazingira na mambo mengi zaidi ambayo yanatuunganisha sisi kama mataifa katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Inafaa tutafautishe baina ya mtu ambaye ameelimika na mtu ambaye anajua lugha, tusiwe tunafikiria kwamba iwapo unajua Kiingereza basi wewe umeeelimika ama wewe una elimu ya juu. Unaweza kujua Kiingereza lakini ukawa huna elimu. Kuna yule anajua Kiswahili na akawa na elimu ya juu sana. Kiingereza ni lugha tu, si elimu. Tukiangalia Tanzania, kuna watu ambao wamebobea sana katika nyanja tofauti, lakini hawajui Kiiingereza, wanaongea lugha ya Kiswahili. Kwa hivyo, jambo hilo ni lazima kutofautisha. Jambo la pili ni kwamba lugha ya Kiswahili ndio lugha pekee ambayo inaweza kuondoa ukabila katika taifa letu la Kenya. Leo hii katika taifa letu la Kenya tuna lugha za kikabila zaidi ya 45 na hivyo basi zinazidi kututia katika mambo ya kikabila, iwapo hatutachagua lugha moja ambayo itatuunganisha. Tukiweza kutukuza lugha hii ya Kiswahili, mambo ya kikabila na tofauti zetu za kikabila zitapungua."
}