GET /api/v0.1/hansard/entries/1194848/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 1194848,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1194848/?format=api",
"text_counter": 163,
"type": "speech",
"speaker_name": "Igembe Kusini, UDA",
"speaker_title": "Mhe. John Paul Mwirigi",
"speaker": null,
"content": " Asante sana, Mhe. Spika wa Muda kwa kunipa nafasi kuchangia Hoja hii. Kabla ya kutoa maoni yangu, nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa Igembe Kusini kwa kunipa nafasi ya pili ya kuwawakilisha. Wengi walidhani kuwa sisi vijana hatuna ubunifu wa kufanya kazi na kuwasaidia wananchi. Wengi walidhani kwamba nitakuwa kiongozi wa muhula mmoja tu na baada ya hapo nitasahaulika. Nawashukuru sana wananchi wa Igembe Kusini kwa kunipa nafasi ya pili ili niweze kuwahudumia. Kama nilivyowaambia, nitawahudumia kwa uaminifu na kutenda kazi zaidi ya vile nilivyofanya katika muhula wa kwanza. Kwa hivyo, nawashukuru sana na naomba Mungu aweze kutupa nguvu kwa miaka hii mitano ili niweze kuwahudumia vyema. Mhe. Spika wa Muda, nampa kongole Mhe. Yusuf kwa kuleta Hoja hii Bungeni. Unafahamu vyema kuwa lugha ya Kiswahili imedhalilishwa sana katika taifa hili ilhali tunajua kuwa ni lugha ya kitaifa na pia imekubalika katika Katiba yetu kutumika kama lugha rasmi. Kwa hivyo, kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili katika taifa hili kutachangia pakubwa kuhakikisha kwamba lugha hii imeweza kupata nafasi yake katika taifa hili. Huwa tunasema kila wakati kuwa taifa letu limejengeka katika Kiswahili lakini wakati ambapo tunaenda katika mikutano mikuu, tunaendelea kutumia lugha ya wakoloni bila sisi wenyewe kujielewa kwamba tuko na lugha na utamaduni ambao tunafaa kuhifadhi. Baraza la Kiswahili likibuniwa, litasaidia taifa letu kushiriakiana kwa pamoja na pia kuleta umoja. Wakenya wakizungumza lugha moja na kutupilia mbali lugha za makabila yao, hii lugha itakuwa ni ya kuleta umoja. Wakenya wote tutakuwa kabila moja kwa maana wataunganishwa na hii lugha, itatusaidia pakubwa na itainua na kuimarisha utaifa wetu. Naibu Spika wa Muda, ninampongeza Mhe. Yusuf kwa kuleta hii Hoja Bungeni. Ninaiomba Wizara husika kuangazia na kutilia mkazo suala la kubuniwa kwa baraza lililopendekezwa punde tu Bunge litakapopitisha Hoja hii. Tutakapoipitisha hii Hoja, Serikali iichukulie kwa uzito ili iweze kuwasaidia wananchi. Vilevile, ningeomba sana Wakenya, na haswa taasisi za elimu, watumie lugha ya Kiswahili ili waimarishe utamaduni wetu na pia wanafunzi waweze kuelewa nchi hii imetoka wapi na inaelekea wapi. Wanafunzi wanafaa kuelewa kuwa hii si nchi ya ukabila kwa maana watakuwa wameunganishwa na lugha ya Kiswahili. Kubuniwa kwa Baraza la Kiswahili ni jambo ambalo limechelewa sana na huu ni wakati mwafaka wa kulitekeleza jambo hili. Baadhi ya Wabunge wenzangu wamesema kuwa tulipokuwa tukiomba kura, tulitumia lugha ya Kiswahili. Tuliwasiliana na wananchi moja kwa moja na walituelewa. Sio vyema basi kila wakati kutumia lugha ya mkoloni, ambayo mwananchi haelewi. Kuna pendekezo kwamba lugha rasmi ya Kiingereza iwe inatumika kutoka Jumatatu mpaka Ijumaa. Ni vyema kuhimiza matumizi ya Kiswahili. Vilevile, Baraza la Kiswahili litakapobuniwa litasaidia mpaka vyombo vya habari. Lugha zinazozungumzwa kwenye vyombo vya habari sio sanifu. Baadhi ya wazungumzaji wanaharibu lugha. Baraza lililopendekezwa litasaidia kuwalazimisha wahusika kwenye vyombo hivyo kusanifisha lugha ya Kiswahili. Baadhi ya Wabunge wamegusia suala la vijana wanavyotumia lugha ya Sheng. Hili baraza litakapobuniwa, tutaweka kanuni mwafaka ili kutoa mwelekeo kuhusu matumizi ya Kiswahili. Hii lugha itajengeka vyema katika taifa hili na itasaidia kukua kwa hili taifa. Kwa hayo mengi, ninaunga mkono."
}