GET /api/v0.1/hansard/entries/1194851/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 1194851,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1194851/?format=api",
    "text_counter": 166,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Gilgil, UDA",
    "speaker_title": "Mhe. Martha Wangari",
    "speaker": null,
    "content": " Asante Mheshimiwa Spika wa Muda. Ninaunga mkono Hoja hii. Ninampa kongole Mhe. Yusuf Hassan wa Kamukunji kwa kuileta Hoja hii Bungeni. Nafikiri leo ni mara ya kwanza sisi wenyewe kuendeleza mazungumzo na mjadala karibu kikao kizima cha asubuhi tukitumia lugha hii ambayo tunaienzi. Sisi sote tumeweza kusoma mambo mengi. Tumeona kwamba baadhi yetu tumeshindwa kutumia dakika kumi tulizotengewa kuchangia Hoja hii. Hakuna hata mmoja wetu aliyewashiwa taa nyekundu wakati anapozungumza, kuashiria kumalizika kwa muda wake. Hii ni kwa sababu hatuna uzoefu wa kutumia hii lugha. Tunafaa kuwa kwenye mstari wa mbele kuendeleza na kuonyesha vile lugha ya Kiswahili inafaa kutumika. Mambo na historia ya Kiswahili yanajulikana tangu zamani. Lugha hii imetumika haswa kwenye taifa la Tanzania. Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliweza kutumia Kiswahili sana Tanzania ilipokuwa ikipigania uhuru kupitia chama cha TANU. Hatimaye, UNESCO ilitenga tarehe 7 Julai kila mwaka kuwa siku ya ya kusherehekea Kiswahili duniani. Idadi ya watu wanaotumia Kiswahili ulimwenguni ni zaidi ya milioni mia mbili. Uzuri ni kwamba hili jambo limeweza kuchukuliwa kuwa la maana sana na UNESCO, ambayo imeidhinisha Kiswahili kitumike kama lugha ya kiasili na utangamano duniani. Hapa Kenya, tumeweza kuwa na utangamano wa jamii tofauti. Tumewahimiza watu kutoka jamii tofauti hata waweze kuoana na tumepoteza lugha zetu za kiasili. Lugha ambayo imebaki ni Kiswahili – ambayo inatuunganisha sisi sote. Baadhi ya Wabunge wenzangu waliotangulia kuchangia Hoja hii, wamesema kwamba wakati tulipokuwa tunapiga siasa muda usiokuwa mrefu, hatukuwa tunatumia sana lugha ya Kizungu. Tulitumia Kiswahili. Wakati unahudhuria mchanganyiko wa jamii nyingi unafaa kutumia lugha ya kiasili. Kwa mfano, ukihudhuria mkutano wa Wakikuyu, unafaa uongee Kikuyu. Unapohudhuria mkutano wa Wajaluo, unaongea Dholuo ama Kijaluo. Lakini unapokwenda kwenye mkutano unaohudhuriwa na mchanganyiko wa jamii tofauti, kama vile Wakisii, Wajaluo na Wakalenjin, itabidi utumie Kiswahili ndiyo muweze kuongeleshana na kusikilizana. Hapa Bungeni, tumeonyesha kuwa hii lugha inawezakutumika. Pia, tumeitumia lugha katika Kanuni za Kudumu za Bunge ama National Assembly Standing Orders . Nchini Tanzania, majina ya taasisi za umma na wizara za serikali yamenukuliwa kwa Kiswahili kwenya majengo ya serikali. Utaona jina la maabara ya sayansi limechapishwa kwa Kiswahili kwanza na kuwekwa kwa Kiingereza kwenye mabano. Hapa kwetu, hatuweki jina la taasisi ama wizara kwa Kiswahili hata kwenye mabano. Tunachapisha tu kwa Kizungu bila Kiswahili. Tunafaa kuwa kwenye mstari wa mbele kuonyesha kuwa inawezekana kutumia Kiswahili kama lugha rasmi. Tunafaa kuhakikisha kuwa Kiswahili kinatumika katika jamii. Tunapaswa tuwafunze watoto wetu pia. Haswa, sisi ambao ni wazazi wa watoto wachanga wanaopitia mfumo wa elimu wa CBC, ni jukumu letu kwenda shuleni kuona kwamba watoto wanafunzwa lugha ya Kiswahili. Tukishazaa watoto, kabla wafikishe umri wa kisheria wa kuenda shuleni, inafaa wawe wanapata mafunzo ya Kiswahili. Tunafaa kutumia Kiswahili katika jamii zetu kwa sababu lugha usiokuwa na uzoefu wa kuizungumza itapotea kwa sababu haitumiki. Kwa hivyo, ni jukumu letu kama wazazi kuhakikisha kwamba tunaitumia vizuri na tunawafunza watoto wetu ndio wakienda shuleni waweze kuendeleza mazungumzo na lugha zingine. Uzuri wa watoto ni wanaweza kujifunza lugha haraka. Hata ukizaa mtoto Uchina na umlete Kenya leo, atafunzwa Kiswahili na atashika kutoka mwanzo wake. Kwa hivyo, ni jukumu letu tuanze pale mwanzo. Tuko na wakati mzuri sasa kwa maana tuko na Baraza jipya la Mawaziri."
}