GET /api/v0.1/hansard/entries/1323778/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 1323778,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1323778/?format=api",
    "text_counter": 106,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Matuga, ANC",
    "speaker_title": "Hon. Kassim Tandaza",
    "speaker": null,
    "content": "kwamba ‘huyu ni babu’ ama ‘nyanya’ yetu na wakati wote mwendazake alikumbukwa. Hii inaleta familia pamoja wakijua kwamba walikuwa na nyanya au mzee wao mahali pale. Endapo kuna ugomvi, kigango hicho kilikuwa kinatumika kama ukumbusho. Kigango hicho kinaskia mnapoteta, na kinajua kwamba kuna haja ya kuleta uwiano katika familia. Ni muhimu hii historia iweze kuhifadhiwa na kurudishwa. Tukizungumzia utalii, ambao ndio tegemeo la maeneo ya Pwani, kuna hoteli na bahari, lakini baadhi ya watalii hutaka kuona asilia ya jamii. Basi inafaa hivi vigango virudishwe moja kwa moja viweze kudumisha utalii – siyo tu kwa watalii wa kutoka nje; ninasema kwamba hata Wakenya kutoka sehemu nyingine za nchi wangetaka kujua ni kwa nini vigango hivyo vilitumika na vina historia gani. Ningetaka kuongezea sauti Hoja hii kwa sababu wazungu walichukua raslimali zetu za kiasili na kuzipeleka kwao. Wamenufaika pakubwa kwani kama wenzangu walivyosema, kuna wageni ambao huenda tu kuona raslimali zetu za kiasili. Kwa hivyo, kwa muda wa takriban miaka 100, wameweza kupata hela nyingi kupitia vitu kama vigango na raslimali nyingine. Kwa hivyo, mbali na hii Hoja inayosema kwamba tusimamishe kusafirishwa na turejeshewa raslimali zetu za kiasili, ni bora tudai mgao wa pesa ambazo wameweza kukusanya miaka hiyo yote. Kwa sababu, kule ughaibuni, watalii hulipishwa kwa sarafu ya juu sana kuliko shilingi ya Kenya. Watatupatia asilimia ngapi ya hela walizokusanya miaka hii yote? Ni wazi kwamba walikuwa wakifanya biashara haramu kutumia vitu vyetu wakitengeneza hela na mali. Kisheria, si vizuri kuwaruhusu watu, kwa sababu walikuwa mabwenyenye na mabwana wetu wakati wa ukoloni, wanufaike na pesa ambazo wametengeneza. Kwa hivyo, si vizuri mjadala huu uishie hapa. Ninasisitiza kwamba zile pesa ambazo wameweza kukusanya kupitia raslimali hizi miaka hii yote zipigwe hesabu nasi pia tupewe mgao wetu. Swala lingine muhimu ni zile raslimali ambazo bado tuko nazo na hatuzithamini. Utakuta raslimali nyingi ziko na watu wa kawaida wasio wasomi na wasio na uwezo wala ufahamu. Kwa hivyo, wizara husika ina jukumu la kusimamia. Ikiwa ni vibali ambavyo vinahitajika vya kutambulika, kama ‘patents’, basi Serikali inaweza kuvisimamia. Hii ni kwa sababu, tuna uvumbuzi mwingi ambao mpaka sasa bado uko na wizara. Iwapo Wizara haitashuhulikia jambo hili, ni wazi kwamba baadaye uvumbuzi huo unaweza chukuliwa na watu binafsi kutoka nchi za ughaibuni kwa sababu wao wanauwezo wa kitaaluma. Baadaye tutalalamika na kuleta Hoja Bungeni tukidai turegeshewe ilhali pale mwanzo wizara husika haikuweza kutambua na kushughulikia jambo hilo. Jambo la kushangaza ni kwamba, kama alivyosema mwenzangu, tunalizungumzia jambo hili ilhali hatuna hata vazi la kitaifa. Hivi saa kuna mjadala Bungeni kuhusu vivazi la kitaifa. Nimeelezwa kwamba kila anayezungumza katika Bunge hili ni lazima awe amevaa suti, koti na tai – kama alivyotufundisha mbeberu kabla tupate uhuru. Hii inamaanisha kwamba kifikira na kiakili bado tunaenzi wale waliotutawala. Tunafikiri tukiendelea kukaa, kuvaa na kula kama wao basi tutakuwa tumestaarabika. Inafaa tujikwamue kutoka fikira kama hizo. Kama kuna vazi la kitamaduni lenye heshima, au vazi la Kiafrika, basi tulishabikie. Wenzetu ambao wanaamini kwamba ukivaa koti na tai basi wewe ndiye mustarabu, tuwambie kwamba hizo ni fikira za kikoloni, ambazo hazitatusaidia. Kulingana na wataalamu wa kisaikologia, wakati umeweza kumteka mtu na kumfanya azungumze lugha yako; afikirie, akae, ale, na alale kama wewe, umemtawala kifikira na bado ni mtumwa wako. Hili ni jambo ambalo naona hata sisi Wabunge bado tunatawaliwa kifikira. Naunga Hoja hii mkono na kama nilivyosema, ningependa ipanuliwe ili raslimali hizo zisiregeshwe tu bali fedha ambazo wamekusanya kupitia vigango vyetu na rasilimali nyingine zikaguliwe ili nasi tuweze kupewa mgao wetu. Asante sana, Mhe. Spika wa Muda. Naunga mkono."
}