GET /api/v0.1/hansard/entries/1326417/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 1326417,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1326417/?format=api",
    "text_counter": 163,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Sen. Faki",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 13211,
        "legal_name": "Mohamed Faki Mwinyihaji",
        "slug": "mohamed-faki-mwinyihaji-2"
    },
    "content": "Asante Bw. Naibu Spika, kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia Ripoti ya Kamati ya uchunguzi wa Shakahola. Naipongeza Kamati hii ambayo iliongozwa na Seneta wa Gatuzi la Tana River, Sen. Mungatana. Nikiwa mmoja wa wanakamati, tulihudumu katika Kamati hiyo kwa hali iliyokuwa ngumu kidogo. Hii ni kwa sababu, baadhi ya mambo tuliyoyapata yalihitaji uchunguzi wa kina. Lakini, tulizuiliwa kimfuko kufanya uchunguzi na kuwaona na kuwahoji baadhi ya mashahidi. Kazi ya Kamati ilikuwa ngumu kidogo, lakini tulijitahidi tukaja na Ripoti ambayo ni muhimu sana kwa nchi yetu. Bw. Naibu Spika, swala hili la mkurupuko wa mashirika ya kidini ni jambo ambalo halijaangaliwa katika nchi yetu, mpaka alipokuja Pastor Mackenzi na kanisa lake ndio watu wakaona kwamba kuna hatari na baadhi ya watu walikuwa washapoteza maisha yao. Kwa hivyo, kulikuwa na haja ya serikali kuingilia maswala ya mkurupuko wa dini tofauti tofauti. Imekuwa rahisi kwa mtu yeyote akitaka kufungua kanisa ama shirika lolote la dini. Akishika Bibilia, asimame Jeevanjee ama Mama Ngina Mombasa na ahubiri, baada ya wiki moja au mbili, kanisa limesimama. Ipo haja ya kuwa na kanuni za kuweza kusimamia mashirika ya kidini. Hii ni kwa sababu hata sisi katika Bunge, kuna mambo ambayo tunaweza kufanya na kuna yale ambayo hatuwezi kufanya. Kwa hivyo, haiwezekani kwamba mashirika ya kidini yana jificha chini ya uhuru wa kuabudu na kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili na dini zao na kanuni za nchi yetu ya Kenya. Mauaji ya Shakahola hayakuanza na Pastor Mackenzie. Kwa muda mrefu, kwa vile Shakahola inapakana na Mbuga ya Wanyama ya Tsavo, ilikuwa mahali ambapo watuhumiwa wa mauaji ya kiholela ya polisi walikuwa wakitupwa pale. Hili ni swala ambalo hata polisi wenyewe walikuwa wanajua kwa sababu wakati uchungunzi ulipoanza, wale ambao walitupwa mwanzo, polisi walijaribu kuwapuuza kwa sababu walijua ni jambo la kawaida. Tungependa uchunguzi zaidi ufanywe kuhusiana na wale ambao walipotezwa, hususan katika sehemu za Pwani. Hii ni kwa sababu, wengi ambao walipotea, simu zao zilikuwa zinapotea maeneno ya Malindi karibu na msitu wa Shakahola."
}