GET /api/v0.1/hansard/entries/1604320/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 1604320,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/1604320/?format=api",
    "text_counter": 275,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Sen. (Dr.) Murango",
    "speaker_title": "",
    "speaker": null,
    "content": "Katika hekima ya Sen. Omogeni ambaye in Seneta wa Nyamira, alipendekeza marekebisho ambayo yatahakikisha kwamba tunaanza mfumo mpya wa kugawa pesa bila tashwishi au kelele zozote na vile vile bila kubadilisha mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Fedha na Bajeti inayoongozwa na Sen. Ali Roba. Sababu kubwa ya kutaka marekebisho ni kuwa vigezo vilivyotumika katika ugavi wa fedha mwaka huu ungefanya kaunti ndogo ndogo zisifaidike kwa kiwango kubwa. Kama ni ukubwa, kaunti ndogo sio kubwa. Ukiangalia wingi wa watu, utapata ya kwamba hizo kaunti ndogo hazina watu wengi. Hizo kaunti ziko na uzito wa watu sehemu fulani lakini hazina watu wengi. Ukiangalia kiwango cha ufukara, utapata ya kwamba hizo kaunti, na hata Kirinyaga, haziko hapo. Baada ya kusikizana, tumejenga ukuruba na usuhuba ya kwamba wakati Bunge itakapoendelea kujadili mfumo, hakutakuwa na shida yoyote kuipitisha. Ninasema hivi lakini kuna kitu ambacho ningependa kumwambia Gavana wangu, Gavana Anne Waiguru. Saa hizi, tunapigania huu mfumo mpya ili tuweze kupeleka pesa katika gatuzi zote za Kenya na moja wapo ni ile ya Kirinyaga. Nyumba ya Seneti huwa inatumika na magavana kama tinga tinga. Kazi yetu ni kubomoa mlima. Barabara inapopatikana, sisi huwa tunawekwa juu ya lori ili tusiharibu barabara. Ukienda katika gatuzi nyingi, Seneta anapouliza jambo fulani lifafanuliwe, unapata ya kwamba anachukuliwa kama adui na gavana. Ningependa kumwambia gavana wangu ya kwamba, katika shamba la mpunga wa Mwea, barabara hazijawahi kutengenezwa kutoka wakati wa ukoloni mpaka tukapata uhuru. Saa hii, katika mfumo mpya ambao tumejadili, tukasikilizana na tukajenga usuhuba kama Bunge la Seneti ni kwamba Kirinyaga itapata zaidi ya Shilingi 300 milioni juu. Ninaomba Seneti iweze kujua ya kwamba fedha zile zinafanya kazi gani. Pesa zikiongezewa Kirinyaga, ziweze kuangalia zile barabara za shamba ya mpunga wa Mwea. Wakulima wamekuwa wakiogelea katika hizo barabara badala ya kutembelea kwa sababu kukinyesha, zinakuwa ziwa na zingine zinakaa mahandaki ambayo zinatumika na jeshi letu la Kenya. Ninamwomba Gavana ya kwamba akipata hizi pesa ambazo ni zaidi ya Shilingi 200 milioni aziweke katika mfumo na kutengeneza miundo msingi katika gatuzi ya Kirinyaga, atengeneze barabara. Mbeleni alikuwa akisema ya kwamba hana pesa. Mtu akikuambia ya kwamba ameshika chura kwa mkia na akamrusha, jua ya kwamba hiyo ni uongo. Sasa, hatakuwa na sababu ya kushika chura kwa mkia. Pesa ikimfikia, ajenge barabara na aweke dawa kwa hospitali. Mwakilishi wadi kutoka eneo la Mwea lazima ajue ya kwamba kuna mhunzi na mfyatua moto. Sisi ni wahunzi na tushawatengenezea. Hao waende wafyatue moto wakati wanatengeneza bajeti. Lazima wahakikishe ya kwamba pesa ambazo tumeng’ang’ania kama Maseneta na wakazipata zimefanya kazi vilivyo."
}