GET /api/v0.1/hansard/entries/194304/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 194304,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/194304/?format=api",
    "text_counter": 243,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Gumo",
    "speaker_title": "The Minister for Regional Development Authorities",
    "speaker": {
        "id": 160,
        "legal_name": "Fredrick fidelis Omulo Gumo",
        "slug": "fred-gumo"
    },
    "content": " Asante sana, Bw. Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ili nizunngumze juu ya Hoja hii ya likizo. Ninaunga mkono Hoja hii kwa sababu kuna mambo mengi ambayo tunahitaji kuyafanya kule mashinani. Siasa si hapa Bungeni tu, bali tunahitajika kushughulikia mambo mengine kule mashinani au nyumbani. Bw. Naibu Spika, kuna watu wengi waliotimuliwa kutoka makao yao baada ya uchaguzi mkuu. Watu hawa sasa wanataka kurudi mashambani mwao ili waendelee na shughuli za kilimo. Watu hawa ni lazima wasaidiwe sana na waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine wa kisiasa. Tusipofanya hivyo, chuki itaendelea kuwepo baina yao. Ikiwa sisi waheshimiwa Wabunge hatuwezi kwenda kuongea na kushauriana na hawa watu wetu ili wakubali wale wengine warudi mashambani mwao, basi tutakuwa na shida sana hapa nchini. Ni wakati wa likizo kama hii ambapo tunaweza kufanya hivyo. Bw. Naibu Spika, baada ya uchaguzi mkuu tulishuhudia vita na vurumai za kila aina katika nchi hii. Kuna baadhi ya vijana na watu fulani waliotiwa mbaroni kwa madai ya kuhusika katika vurumai hizo. Hata hivyo, hakuna watu walioshuhudia vijana hawa wakiwapiga watu au kuhusika katika vurumai hizo. Wengi wao waliwekwa ndani na polisi kwa madai ya kushukiwa kuhusika katika matendo hayo. Sote tunajua ya kwamba wakati mwingi askari wanapofanya kazi, wanaweza kuwashika watu bila kuzingatia haki. Kwa hivyo, tunataka kumaliza hayo mambo, na huku tukizingatia tumo katika Serikali ya Mseto. Ninamuomba Rais awasamehe vijana hao wote na awakubalie kujiunga tena na jamii zao. Bw. Naibu Spika, ikiwa tutaendelea kuwazuilia vijana hao korokoroni na tunataka wahasiriwa wa vita vya baada ya uchaguzi warudi mashambani mwao, basi hili jambo halitawezekana kwa vile wazazi wa vijana hawa wana chuki ndani yao. Hatuwezi kuwa na msamaha wa kudumu. Kwa hivyo, tunaposema tumo katika Serikali ya Mseto, basi yafaa tushirikiane hata kule mashinani. Wale waliowekwa ndani yafaa waachiliwe bila masharti yoyote na tuwaonye dhidi ya kupigana tena na waishi kama ndugu kwa amani. Hiyo ndio njia mwafaka ya kumaliza chuki baina ya watu wetu. Ikiwa tunataka kuongea na Mungiki, na hata Wabunge wengine hapa wameunga mkono jambo hilo, kwa nini hatuwezi kuwaachilia huru hawa vijana? Ikiwa kuna shida au taabu katika maisha, ni lazima tuzungumze na adui wetu. Huwa tunawasamehe watu kwa sababu katika maisha, watu hufanya makosa hapa na pale. Vijana hawa walifanya makosa na ni jukumu letu kumuomba Rais awasamehe. Yafaa tuwe na mwanzo mpya na tuendelee mbele na tusahau yaliyopita. Maziwa yakimwagika hayazoleki!"
}