HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 197229,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/197229/?format=api",
"text_counter": 25,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Mung'aro",
"speaker_title": "The Member for Malindi",
"speaker": {
"id": 76,
"legal_name": "Gideon Mung'aro Maitha",
"slug": "gideon-maitha"
},
"content": " Asante, Bw. Naibu Spika. Nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Majina yangu kamili ni Mung'aro Gideon Maitha, Mbunge wa Eneo Bunge la Malindi. Kwanza, ningetaka kuchukua nafasi hii kuwashukuru watu wa Malindi kwa kunichagua kuwa katika Bunge hili la Kumi, ambalo ni la kihistoria. Wamenipa uwezo wa kuwa mmoja wa Wabunge katika Bunge hili. Pili, ningetaka kumpongeza Dkt. Khalwale kwa sababu anaomba Bunge hili lipeleke Wabunge kule Malindi. Mji wa Malindi ulikuwa wa amani wakati wa vurugu zote zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu. Pia, nawapongeza watu wa Pwani kwa jumla kwa sababu tulipoenda huko kama Wabunge, tuliwaambia watu wa Pwani ni lazima waishi kwa amani, kwa sababu Bunge hili la Kumi lilipofunguliwa, hatukuona Wabunge wa PNU na ODM wakipigana makonde; walikuwa wakicheka na kubadilishana mawazo. Bw. Naibu Spika, nikichangia Hotuba ya Rais, kwanza kabisa ningependa kuwapongeza wote waliohusika katika kuhakikisha kwamba kuna amani na maridhiano katika nchi yetu ya Kenya. Lakini pia ningependa hasa kutilia mkazo Mswada wa Utalii ambao utaletwa katika Bunge. Mswada huu unagusia mambo mengi katika Mkoa wetu wa Pwani. Tungependa Mswada huo ukiletwa hapa Bungeni, tuulize maswali na tuufanyie marekebisho yanoyowezekana ili watu wa Mkoa wa Pwani waanze kupata manufaa ya shughuli za utalii. Miaka nenda, miaka rudi, kila kunapotajwa masuala ya utalii katika Bunge, utamsikia Waziri wa Fedha akituambia kwamba utalii umeleta mchango mkubwa katika nchi hii. Inasikitisha kwamba mpaka leo, watu wa Mkoa wa Pwani bado ni maskini na hali wao wanaleta mabilioni ya pesa katika nchi hii. Tungependa Mswada huu ukiletwa hapa Bungeni ufanyiwe marekebisho ili tupate jinsi ambavyo watu wa Mkoa wa Pwani watapata fedha katika kila kitanda kinacholaliwa na mtalii kwa siku na vile vile tuweze kupata ushuru kutoka Mbuga ya Wanyama ya Tsavo kama ambavyo watu wa Maasai Mara na Baraza la Narok linavyopata ushuru kutoka kwa watalii wanaoenda kwa Mbuga ya Wanyama pori ya Maasai Mara. Sisi tunayo Mbuga ya Wanyama ya Tsavo na sioni tofauti kati ya watu wa Maasai Mara na 234 PARLIAMENTARY DEBATES March 19, 2008 watu wa Mkoa wa Pwani. Ikiwa tunaongea kuhusu usawa katika ugawaji wa raslimali, basi ni muhimu kila sehemu iangaliwe kuambatana na mapato yake. Hatujasema eti pesa zote za utalii zibaki katika Mkoa wa Pwani, bali tunasema kwamba kuna haja ya kiasi fulani cha fedha kubaki pale katika Mkoa wa Pwani ili tuweze kuendesha shughuli hizo za utalii. Fedha hizo zitatumiwa katika kukarabati barabara na vifaa vingine ambavyo vitawavutia wageni zaidi. Bw. Naibu Spika, kuhusu suala la ardhi, natumai nitashirikiana na Wabunge wenzangu kwa sababu katika Mkoa wa Pwani, hili limekuwa suala sugu. Sababu hasa ya hili suala la ardhi kuleta taabu katika Mkoa wa Pwani ni bahari. Imekuwa desturi ya viongozi Serikalini, kila kunapoibuka suala la ardhi katika Mkoa wa Pwani, kwa sababu ya ufuo wa bahari--- Inaonekana mwenyeji katika Mkoa wa Pwani hastahili kupata shamba katika ufuo wa bahari ila anastahili tu kupata shamba kando ya bahari. Hii ndiyo imeleta tatizo la maskwota hasa kule kwetu Malindi. Kila siku utasikia - hasa katika sehemu moja iitwayo Chembe Kibabamchu na Kilifi Jimbo - Waziri anayechaguliwa mara ya kwanza huja Malindi kujaribu kutatua suala hili. Baada ya muda, utasikia wamesimamisha ugawaji ardhi katika sehemu hii. Kinachoshangaza ni kwamba kila wanaposimamisha utoaji wa stakabadhi za kumiliki ardhi katika sehemu hii, utapata watu wakitoka Nairobi wakiwa na stakabadhi tayari kuuza ardhi hizo hizo. Wao huzibadilisha kwa watu wengine huku wenyeji wakiangalia tu. Hili jambo likiendelea, hatutaweza kutatua suala la ardhi katika Mkoa wa Pwani. Kwa hivyo, upo umuhimu kwamba watu wakae pamoja. Kila mtu anaruhusiwa kuwa na ardhi katika nchi ya Kenya. Mswada wetu wa maridhiano unatuhimiza sisi Wakenya kuishi pamoja kama Wakenya. Lakini hatutaweza kuishi pamoja ikiwa utakuja kuishi nami kama jirani na wakati ninakukaribisha wewe unapata kibali cha kumiliki ardhi ilhali mimi mwenyeji nabakia skwota. Kwa hivyo, suala hili ni lazima liangaliwe kwa undani sana. Bw. Naibu Spika, Bandari ya Kilindini huiletea nchi yetu ya Kenya mapato makubwa sana. Bidhaa zote kutoka nje zinazoenda nchi jirani hupitia Kilindini. Kwa miaka mingi sana, watu wa Pwani hata kama si Pwani kwa jumla lakini Baraza la Jiji la Mombasa, wameuliza wapate angaa dola moja kwa kila tani ya mizigo inayoingia Kilindini. Hili suala ni lazima liangaliwe. Hakuna haki ikiwa mtu ataleta mizigo kutoka kokote katika nchi ya Kenya, kisha alipe ushuru ama cess kwa baraza lake la manispaa lakini akifika Mombasa, mizigo hiyo itapitia mabaraza ya Voi na Mariakani mpaka ifike Kilindini, ilhali hakuna faida kwa mkaazi wa pwani. Sharti kuwe na faida kwa wakaazi wa Mkoa wa Pwani. Kwa hivyo, kuna haja ya kuona kwamba kiasi fulani cha pesa ama ile dola moja ambayo inatozwa katika Bandari ya Mombasa iweze kupatikana ili iweze kusaidia Mkoa wa Pwani. Natumai wenzangu ambao mara hii tumechaguliwa kuja Bungeni kutoka Mkoa wa Pwani, tumekubaliana kwa kauli moja kwamba ajenda yetu kubwa ambayo tutatekeleza kama watu wa Mkoa wa Pwani, na kama Wakenya, ni kuhakikisha kwamba watu wetu hawatabaki maskini ilhali utajiri umejaa katika mkoa huo. Bw. Naibu Spika, suala la uchaguzi wa moja kwa moja wa mameya katika mabaraza ni muhimu sana. Naongea hivyo kwa sababu nimekuwa Meya wa Malindi kwa muda wa miaka mitano. Vile vile nilikuwa Naibu Mwenyekiti wa mabaraza yote nchini. Nilihusika sana katika kuibua Mswada wa kuwachagua mameya moja kwa moja. Kile tunachoomba ni kwamba Mswada huu ukiletewa Bungeni, basi isiwe tu unahusu wananchi kuwachagua mameya moja kwa moja, lakini pia upendekeze kwamba makatibu wa mabaraza waweze kuajiriwa moja kwa moja kutoka kwa mabaraza ili ufisadi unaoendelezwa na makatibu, hasa baada ya mabaraza kuvunjwa, uondolewe. Utashangaa kutambua yaliyofanyika tangu mabaraza yavunjwe kuanzia Oktoba mpaka kura zilipopigwa. Sheria za baraza zinasema kwamba hakuna pendekezo ama kitu kitakachopitishwa kama hakuna baraza. Utashangaa kwamba maendeleo mengi hufanywa na makatibu wa mabaraza mbio mbio wakati ambapo mabaraza hayo yamevunjwa, kwa sababu March 19, 2008 PARLIAMENTARY DEBATES 235 wakati huo kuna nafasi ya kufuja mali, pesa na kutwaa mashamba ya mabaraza. Kwa hivyo, ni muhimu kwamba Mswada huu ukija, mameya walioko waweze kukaa ofisini hadi meya mwingine achaguliwe ili aweze kuchukua ofisi na ajue anachukua nini. Mhe. Sambili aliongea kuhusu uhamiaji kutoka mashambani hadi mijini ambako kumeibuka mitaa ya mabanda kama vile Kibera na mengineyo. Kuna umuhimu kwetu sisi Wabunge, kama tunahitaji kupunguza uhamiaji kutoka mashambani hadi mijini, kuleta maendeleo vijijini ili tupunguze uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini. Mara nyingi sababu kuu ya watu kuhamia mijini ni kwamba wao wanajua watapata taa ya stima na barabara nzuri huko mijini. Tukiendeleza vijiji vyetu, tutapunguza uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini. Bw. Naibu Spika, mwisho, ningependa kusema kwamba sisi watu wa Mkoa wa Pwani, badala ya kutegemea tu utalii--- Ijapokuwa kumekuwa na shida Kenya nzima, watu walioathirika zaidi kiuchumi ni watu wa Mkoa wa Pwani. Kwa mfano, Malindi ilikuwa inapokea wageni 500 kwa wiki, lakini juzi tulimsikia Waziri Mkuu mtarajiwa akisema kwamba badala ya idadi hiyo ya wageni 500, tulianza kupata wageni saba kwa wiki. Kwa hivyo, tunataka Serikali itilie maanani viwanda vyetu hasa vile vya matunda kwa sababu kule Mkoa wa Pwani tuna matunda mengi yakiwemo maembe, mananasi na mengineyo. Hii itatuwezesha kupata pesa kupitia njia nyingine kando na utalii. Ninashukuru kwa nafasi hii na ningependa kuiunga mkono Hotuba ya Rais."
}