HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 197899,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/197899/?format=api",
"text_counter": 134,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Mwatela",
"speaker_title": "The Member for Mwatate",
"speaker": {
"id": 103,
"legal_name": "Andrew Calist Mwatela",
"slug": "andrew-mwatela"
},
"content": " Ahsante sana, Bw. Naibu Spika wa Muda. Ningependa kuwapongeza Rais Kibaki na Waziri Mkuu mtarajiwa, mhe. Raila, kwa kuafikiana ili nchi hii iingie katika mstari wa maendeleo. Bw. Naibu Spika wa Muda, ningependa pia kuwashukuru wale waliohusika katika majadiliano ya kutafuta uelewano, wakiwemo katika upande wa Serikali, mhe. Karua, mhe. Wetangula, Prof. Ongeri na mhe. M. Kilonzo; na kwa upande wa ODM, mhe. Mudavadi, mhe. Samoei, mhe. S. Kosgey na mhe. Orengo. Ningependa kusema kwamba hali iliyotanda katika nchi hii baada ya tarehe 28 Desemba, 2007, ni hali ambayo ilitishia sana taifa hili. Bw. Naibu March 12, 2008 PARLIAMENTARY DEBATES 89 Spika wa Muda, tukiangalia historia ya nchi hii kwa makini, tutaona ya kamba kabla ya Uhuru, wananchi walijitolea mhanga kupigana na mkoloni. Sababu kubwa ya wao kuchukua silaha dhidi ya mkoloni ilikuwa ni ardhi. Ardhi yao ilikuwa imenyakuliwa na mkoloni. Ningependa ieleweke kuwa watu wengi, hasa kutoka Mkoa wa Kati, walipigania ardhi yao. Hata hivyo, baada ya Uhuru, ardhi iliendelea kubaki mikononi mwa watu wachache. Wengi wa watu waliopigania haki ya kumiliki ardhi yao walihamishwa na kupelekwa sehemu mbali mbali nchini. Kwa mfano, wengi wao walipelekwa sehemu za Molo na Eldoret. Bw. Naibu Spika wa Muda, ingekuwa bora wakati tunapozungumza juu ya mambo haya tuwatambue kwa uwazi wale watu wote waliomiliki ardhi baada ya Uhuru, na hasa katika Mkoa wa Kati. Ni heri kama ardhi hiyo ingepewa watu wengi katika Mkoa wa Kati. Bw. Naibu Spika wa Muda, ningependa kuzungumza juu ya swala la watu ambao wamepoteza makao yao na sasa hivi wanaishi katika kambi mbali mbali hapa nchini. Ni kweli kuwa kuna hazina ambayo Serikali imetenga ili kuwashughulikia watu hao. Ninakubaliana na waheshimiwa Wabunge waliosema kuwa hazina hiyo haitoshi. Ingekuwa bora zaidi kama Serikali ingewasaidia wanabiashara wote walioathirika kutokana na fujo za kisiasa ili kuzindua upya biashara zao. Hii inawezekana ikiwa usimamizi wa hazina hiyo utakuwa mikononi mwa benki zetu na ikiwa wanabiashara walioathirika watapewa mikopo ya riba ya chini ili waweze kufufua upya biashara zao. Mojawapo ya majukumu ya Bunge la Kumi ni kuhakikisha ya kwamba tutakuza watoto wetu katika maadili ya kupendana. Maadili haya ni lazima yaanze katika shule zetu. Walimu wanafaa kuwafunza watoto kuishi na wenzao bila ya kujali misingi yao ya kikabila. Bw. Naibu Spika wa Muda, wenzangu wamegusia kuhusu barabara. Katika nchi hii, barabara zetu ni mbovu mno. Kwingineko, tumeahidiwa kuwa barabara zitajengwa kwa miaka mingi na hazijajengwa. Katika sehemu yangu ya Mwatate, kuna barabara ambayo imetoka Voi kuelekea mpakani Taveta, ambayo, kama ingejengwa, ingeleta faida kubwa kwa uchumi wa nchi hii. Ningependa kueleza kuwa urefu wa barabara kutoka Bandari ya Dar-es-Salaam, Tanzania, mpaka Arusha, ni mara zaidi ya mbili urefu wa barabara kutoka Bandari ya Mombasa kufika Arusha. Vivyo hivyo, urefu wa barabara kutoka Bandari ya Tanga, Tanzania, kufika Arusha ni mkubwa kuliko urefu wa barabara kutoka Mombasa mpaka Arusha. Tukichukulia kuwa sehemu za Arusha na Kilimanjaro ndizo sehemu zenye hali kuu ya uchumi wa Tanzania na zinahitaji umuhimu wa bandari, tutaona kuwa tukiijenga barabara ya kutoka Voi hadi mpaka wa Taveta, tutapanua biashara kati ya sehemu za Arusha na Kilimanjaro na nchi yetu ya Kenya. Ningependa kuiomba Serikali iharakishe ujenzi wa barabara hiyo kwa sababu bila shaka, itaongeza uajiri kwa wingi sana. Ningependa kumalizia kwa kusema kuwa nchi hii ni tajiri sana isipokuwa utajiri mwingi uko mikononi ya wa watu wachache sana. Tena utajiri huo haukupatikana kwa haki. Mara nyingi, umepatikana kupitia ufisadi. Ninaunga mkono Hoja iliyotolewa hapo mbeleni kuwa Serikali yetu isiwe na wafisadi ndani yake. Serikali yetu inafaa kuwapatia madaraka watu ambao wanajulikana kwa kupigana na ufisadi. Hapo mbeleni, imeonekana kuwa ikiwa mfanyikazi wa Serikali anapinga ufisadi, huadhibiwa badala ya kupandishwa cheo. Ningependa kuiomba Serikali ihakikishe imewapandisha vyeo wafanyikazi ambao wanatenda uzuri kwa nchi hii ili tuweze kupigana na ufisadi. Kwa hayo machache, ninaiunga mkono Hotuba ya Mheshimiwa Rais. Pia ninaunga mkono mapendekezo yaliyoko katika Hotuba hiyo."
}