GET /api/v0.1/hansard/entries/209896/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 209896,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/209896/?format=api",
    "text_counter": 119,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Wamwere",
    "speaker_title": "The Assistant Minister for Information and Communications",
    "speaker": {
        "id": 352,
        "legal_name": "Koigi Wamwere",
        "slug": "koigi-wamwere"
    },
    "content": "Bw. Naibu Spika wa Muda, hiyo ni kweli, lakini si hoja. Mashirika ya umma yalijengwa na pesa za umma na ni wazi kwamba umma ndio unapata hasara kubwa wakati mashirika yake yanauziwa watu binafsi kwa bei ya kutupa. Wakati huu, kuna haraka ya kuyauza mashirika ya umma. Hili ni jambo lisiloeleweka. Ni majuzi tu tumeona shirika la bima la Kenya Re-insurance likiuziwa watu binafsi, ijapokuwa kuna hisa chache ambazo zimekwenda kwa umma. Kitambo, tuliona Shirika la Reli likiuziwa kampuni ya kigeni. Sasa tuko katika harakati za kuuza mashirika ya simu ya Safaricom na Telkom. Bw. Naibu Spika wa Muda, kampuni kama vile Safaricom na Telkom zimekuwa zikipata faida. Imekuwa kisingizio kikubwa kwamba mashirika ya umma yanaleta hasara na kwa sababu hiyo, yanapaswa kufungwa. Lakini ikiwa kampuni ya Safaricom ndiyo inaongoza katika kupata faida, je, kuna sababu gani ya kuibinafsisha? Kuna sababu gani ya kuuza kampuni ambayo inapata faida? Kwani hasara ndio msingi wa falsafa ya kubinafsisha makampuni katika nchi hii. Bw. Naibu Spika wa Muda, lazima tutambue ya kwamba kuna ulafi na uroho wa mali katika ubinafsishaji wa mashirika. Kuna tabaka la watu ambao wanataka kuchuma chao mapema. Wanataka wanyakue mashirika haya kabla ya kuondoka mamlakani. Hii itakuwa ni hasara kubwa sana kwa watu wa nchi hii. Nchi hii haimilikiwi na watu wachache au tabaka fulani. Ni mali yetu sote. Kwa hivyo, kuchukua mashirika ambayo yalijengwa na wananchi na kuyapatia watu wachache katika jina la kukuza uchumi, ni kutofanya haki. Bw. Naibu Spika wa Muda, ukiangalia haraka hii ambayo inatufanya kubinafsisha maji na vitu vingi--- Ninaona kama hivi karibuni tutakuwa tunaambiwa pia tubinafsishe Serikali kwa sababu sekta ya binafsi ndio yenye ujuzi zaidi wa kuongoza kila kitu. Ninadhani kuna watu hapa ambao wako tayari kusema hata Serikali isimamiwe na watu binafsi kwa sababu wao ndio wenye ustadi wa kuleta faida. Isitoshe, tumesoma vitabu vya riwaya juu ya kubinafsishwa kwa hewa. Wakati tulikuwa tunakisoma kitabu cha Ngugi tulidhania kwamba huu ulikuwa ni mchezo. Inaonekana ya kwamba watawala tulionao sidhani itakuwa vigumu kwao kubinafsisha hewa. Hakuna tofauti ya kubinafsisha maji na hewa! Leo hupati maji isipokuwa machafu bila kulipa pesa. Hivi karibuni tutakuja kuambiwa kwamba ukitaka hewa safi, lazima uwe na mashine ambayo utavalia baada ya kuinunua. Mambo haya yamefanyika katika Mji wa Mexico na yanaweza kufanyika hapa. Bw. Naibu Spika wa Muda, jambo lingine ni kwamba tunaambiwa mantiki kubwa ya ubinafsishaji ni kwamba mashirika ya umma hayawezi kuepukana na ufisadi. Lakini ukweli ni kwamba hata sekta ya binafsi ina ufisadi mwingi sana. Ukilinganisha ufisadi katika sekta ya umma na sekta ya binafsi, utaona ya kwamba ufisadi ni mwingi katika sekta ya binafsi kuliko sekta ya umma. Kama ilivyosemwa, ukitazama nchi kama Scandinavia, utaona kwamba si lazima shirika la umma liwe na lilemewe na ufisadi. Unaweza ukapigana na ufisadi na kuuangamiza katika 3038 PARLIAMENTARY DEBATES August 8, 2007 mashirika ya umma. Tunaweza kufanya hivyo ikiwa hayatasimamiwa na wezi. Tutahitajika kuwafuta kazi, kuwafunga na kuhakikisha ya kwamba hakuna mtu ambaye atafaidika kwa kuliibia shirika la umma. Tukifanya hivyo, hatutakuwa na haja ya kubinafsisha mashirika haya. Yataendeshwa vizuri namna yanavyoendeshwa kule Norway - pahali ambapo niliishi kwa muda mrefu. Niliona mashirika ya umma ambayo yanaendeshwa kwa ustadi sana. Sidhani watu wa Norway wakipewa uchaguzi leo kati ya sekta ya binafsi na ya umma, watachagua sekta ya binafsi. Watachagua kuendelea na mashirika ya umma. Bw. Naibu Spika wa Muda, sababu nyingine ambayo inatolewa ni ile ya ukosefu wa nafasi za kazi. Tunahadaiwa ya kwamba mashirika ya binafsi yanatengeneza nafasi zaidi za kazi. Ukweli ni kwamba, lengo kubwa la makampuni binafsi ni kutengeneza faida, si kuongeza nafasi za kazi. Hii ni tofauti kabisa na mashirika ya umma. Ukiangalia katika dunia, zile nchi ambazo zimefaulu kufutilia mbali ukosefu wa kazi ni zile ambazo mashirika ya umma yanasimamiwa vilivyo. Kwa hivyo, kama kwa kweli lengo letu kubwa ni kuzalisha kazi na kuhakikisha tumemaliza ukosefu wa kazi, hatuna budi kuendelea kuwauzia watu binafsi mashirika ya umma. Tunachotakiwa kufanya ni kuhakikisha ya kwamba yanasimamiwa vizuri ili yaongeze nafasi za kazi. Jambo lingine ambalo ningetaka kugusia ni faida kutokana na uuzaji wa mashirika ya umma. Pesa hizi zitagharamia huduma za wananchi. Lakini shirika la umma likiwa ni mali ya mtu binafsi, basi faida yake itakuwa ni mali ya anayemiliki kampuni hiyo. Anaweza kufanya jambo lolote nayo. Anaweza kuamua kwamba atawaajiri Waamerika wampeleke mwezini na pesa hizo badala ya kusaidia kupanua uchumi. Anaweza akaamua ya kwamba atakuwa anasafiri daima dawamu. Lakini faida za mashirika ya umma, tukiwa na Serikali endelevu, inaweza kusaidia kupanua uchumi na kugharamia huduma za elimu na matibabu ya bure hapa nchini. Kama alivyosema Bw. Mwandawiro, tunaweza kuwa na elimu ya bure hapa nchini kama vile Kisiwa cha Cuba. Ni kisiwa kidogo tu, lakini kinawapa watu wake matibabu na elimu ya bure, nafasi za kazi na kumaliza uhalifu. Jambo ambalo limekifanya kufaulu ni kuwa na mfumo ambao umejengwa juu ya msingi wa mashirika ya umma. Kama hawangekuwa na mashirika ya umma, hawangekuwa na huduma walizonazo. Bw. Naibu Spika wa Muda, ningetaka kusema ya kwamba hakuna ukoloni unaopita kuuza mashirika yaliyojengwa na umma kwa wageni. Uchumi wetu ukimilikiwa na wageni hautakuwa ni wetu tena. Bw. Naibu Spika wa Muda, ninaomba kuunga mkono."
}