GET /api/v0.1/hansard/entries/212113/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 212113,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/212113/?format=api",
    "text_counter": 278,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Mwandawiro",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 253,
        "legal_name": "Mwandawiro JD Mghanga",
        "slug": "mwandawiro-mghanga"
    },
    "content": "Bw. Naibu Spika wa Muda, sababu ya kwanza ambayo imeelezwa na muhimu ni kuwa hukumu ya kifo ni kinyume cha Katiba ya nchi yetu. Sheria inasema kwamba Katiba ndio msingi wa sheria zote. Kwa hivyo, hatufai kuwa na sheria yoyote ambayo inaruhusu hukumu ya kifo kwa sababu inaenda kinyume cha Katiba. Pili, maisha ni haki ya msingi ya binadamu. Tukisema kwamba tunaheshimu haki za binadamu, haki ya msingi kabisa ni haki ya maisha. Kwa hivyo, hukumu ya kifo inavunja haki ya kimsingi ya binadamu na ni muhimu tuiondoe. Tatu, tunajua kwamba binadamu si wakamilifu. Nimekaa gerezani Kamiti mwaka wa 1985 na niliona watu wengi sana wakinyongwa huko Kamiti. Kuna watu niliozungumza nao na wakanieleza kwamba wanaenda kunyongwa kwa makosa ambayo hawakufanya. Walisema kuwa walikosa pesa za kulipa wakili shupavu wa kuwatetea, wakaenda kortini kujitetea na wakapatikana na makosa. Kwa hivyo, sheria hailindi haki za watu wote. Wale mahakimu na majaji ni binadamu. Kuna wakati ambapo majaji hutoa hukumu ya kifo kwa mtu ambaye hakufanya makosa kwa sababu huyo mtu ameshindwa kujitetea kikamilifu kwa sababu ya umaskini. Je tutawaruhusu watu wengine wawe na haki juu ya wenzao na mnajua binadamu si mkamilifu? Tunajua kuna mifano halisi kote duniani ambapo watu waliuawa kwa makosa ambayo hawakutenda. Wakati mwingine ushahidi unapatikana baadaye kueleza kwamba huyu mtu amehukumiwa kifo lakini kumbe ni mtu mwingine aliyefanya kosa. Mtu akishahukumiwa kifo, hata kosa likigunduliwa baadaye, maisha yake hayawezi kurudishwa tena. Inakuwa kama maji yaliomwagika na ambayo hayazoleki. Hatuwezi kuyafanya maisha ya binadamu yawe kama mchezo wa karata, ambapo makosa yanaweza kufanyika kwa sababu yakishaenda; yameenda kabisa. Kwa hivyo, kwa sababu binadamu si mkamilifu na tunajua kuwa kuna majaji ambao wanaweza kuhongwa na pesa, ama mshukiwa anaweza kutokuwa na sababu za kutosha na kushindwa kuelewa ushahidi wa uongo, majaji wanaweza wakatoa hukumu ya kifo na mtu akanyongwa. Kwa sababu hiyo, hatuwezi kuruhusu uhuru wa watu fulani kuvunja haki ya kimsingi ya binadamu kwa kutoa hukumu ya kifo. Bw. Naibu Spika wa Muda, lengo la adhabu ni nini? Falsafa ya adhabu ni nini? Katika mila za Kiafrika, falsafa ya adhabu ilikuwa ni kurekebisha. Hii hukumu ya kifo imeletwa na wazungu ambao ni maharamia, mabepari na wakoloni, ambao walikuja kugandamiza watu huku. Katika 36 PARLIAMENTARY DEBATES July 25, 2007 mila za Kiafrika, hakukuwa na kulipizana kisasi. Lengo adhabu, katika mila za Kiafrika, halikuwa kulipiza kisasi. Lengo la kimsingi la adhabu ya kifo ni kulipiza kisasi; haina kurekebisha. Binadamu waliostaarabika hawawezi kutoa adhabu kwa lengo tu la kulipiza kisasi. Kwa mfano, nchi kama za Marekani, New Zealand na Australia tunajua kwamba wale watu walioenda kule asili kutoka Ulaya walikuwa ni majambazi ambao walifukuzwa kwao Ulaya. Ndio sababu walikwenda huko Marekani, Australia na New Zealand. Kwa hivyo hatuwezi kuweka misingi ya sheria kutokana na mifano ya majambazi ambao wametoka huko Ulaya. Ndio kwa sababu wenye asili ya kijambazi wanaotawala huko Marekani bado falsafa zao ni zile zile za kusisitiza juu ya hukumu ya kifo. Ndio unaona kwamba huko kwao Ulaya wakati waliwaacha watu waliostaarabika, hukumu ya kifo haipo. Hukumu ya kifo inapatikana kwa nchi zile majambazi walihamia kutoka nchi nyingine na wakaenda kuitumia kwa nia ya kugandamiza na kuvunja watu ambao hawakuwa wanawahesabu kama binadamu. Mifano iko halisi, kwamba watu wengine wanaogopa kwamba hukumu ya kifo ikiondoka kutakuwa na uhalifu zaidi; watu watauana zaidi na ujambazi utazidi. Lakini mifano halisi imeonyesha kwamba kote duniani ambapo kumeondolewa hukumu ya kifo, hakujaongezeka ujambazi. Pia visa vya watu kuuana, kuuawa kwa ujambazi na kwa makosa havijaongezeka. Hata huko Marekani wana hukumu hii ya kifo na wanaitekeleza, lakini ujambazi unaongezeka. Kwa hivyo, hukumu ya kifo haiondoi ujambazi, inauongeza. Tunajua hapa kwetu, wakati Bw. Charles Njonjo, aliyekuwa Mkuu wa Sheria, wakati alipoleta hukumu ya kifo kwa wizi wa mabavu haikupunguza wizi wa mabavu katika nchi yetu ya Kenya. Badala yake uliongezeka, na hata iliongeza mauaji, kwa sababu mtu akienda kuiba, anaona kuwa badala ya mtu aende akatoe ushahidi dhidi yake kortini, afadhali amuue kabisa ili kukosekane mtu wa kutoa ushahidi kortini. Kwa hivyo, sababu zote, na hasa sababu ya kimsingi, ni kwamba maisha ni haki ya msingi ya binadamu, na binadamu anamakosa; si mkamilifi; hata akiwa ni hakimu, anaweza kutoa hukumu ambayo haiwezi kurudishwa nyuma. Ikitolewa ni basi, hata kama imetolewa kwa makosa. Hatutaki kuwa na hukumu ya kifo katika nchi yetu, na hasa katika nchi ambayo inaelekea kusimama imara katika ustaarabu. Tukiwa Waafrika, sisi ni watu ambao tuna misingi ya utamdaduni halisi wa kuheshimu haki za binadamu na maisha. Kwa kweli, hii hukumu ya kifo hatustahili kuwa nayo. Kwa maneno hayo machache, naunga mkono."
}