GET /api/v0.1/hansard/entries/216694/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 216694,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/216694/?format=api",
    "text_counter": 102,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Khamisi",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 246,
        "legal_name": "Joseph Matano Khamisi",
        "slug": "joseph-khamisi"
    },
    "content": "Bw. Naibu Spika wa Muda, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia kwa Hoja hii ya Bajeti ya nchi hii katika mwaka unaokuja. Ningependa kuipongeza Serikali na haswa Waziri wa Fedha kwa kutoa Bajeti ambayo, kusema kweli, imeangalia maslahi ya watu mbalimbali katika nchi hii. Hata hivyo, kuna mambo fulani ambayo ni muhimu yatajwe katika mchango huu. Kwanza, ni vigumu sana kwa Serikali kujaribu kueleza kwamba kweli umaskini umepungua kutoka asilimia 46 na hivi sasa umefikia asilimia 56.8. Na kwamba, Wakenya hivi sasa, wanaishi katika hali bora zaidi kuliko awali. Nasema hivyo kwa sababu ukizunguka katika maeneo ya mashambani, utaona umasikini duni ambao, kusema ukweli, haujaweza kukubalika. Katika sehemu yangu ya uwakilishi Bungeni ya Bahari na Wilaya nzima ya Kilifi, ni wazi kwamba umasikini bado unatandaa. Ni shida kwa Serikali kuweza kueleza na watu kuweza kukubali kwamba uchumi kweli umeimarika. Nafikiri Serikali ina wajibu wa kuwaeleza zaidi wananchi, ili wapate kuelewa ni vipi uchumi umeendelea na hali bei za vitu zimeenda juu. Bw. Naibu Spika wa Muda, ninatoka katika eneo la utalii -eneo la Pwani - ambapo asilimia 60 ya wageni wote watalii wanaoingia katika nchi hii wanapitia. Hata hivyo, wakati huu ambapo Serikali inatuambia kwamba pesa zinazotokana na utalii zimeongezeka mara tatu kutoka Kshs22 billioni mwaka wa 2003 hadi Kshs56 billioni mwaka wa 2006, hatujaona mtiririko wa pesa hizi au mapato haya katika sehemu zinazopakana na hifadhi za utalii. Kwa hivyo, ni muhimu kwamba wakati tunapowakaribisha wageni, ni lazima tuhakikishe kwamba watu wanaotoka katika sehemu ambazo wageni wale wanahudumiwa, wanafaidika kutokana na mapato yanayotokana na huduma hiyo. Inasikitisha kwamba wengi wa wageni wanaokuja wanalipa pesa zao nyingi za kigeni katika nchi zao wanakotoka ilhali hapa nchini, kazi za hoteli ni kulipa mishahara tu. Kwa hivyo, ingawa idadi ya watalii wanaokuja Kenya imeongezeka hadi millioni moja na zaidi, ni wazi kwamba pesa zinazoingia katika nchi hii hazifananishwi na idadi ya watalii wanaoingia katika nchi hii. Hii ina maana kwamba watalii wa nchi hii, au Wakenya wenyewe wanaotembelea mbuga za wanyama wa pori au Pwani, wanalipa pesa nyingi zaidi za hoteli kuliko watalii. Itawezekanaje kwa familia moja ya watu wawili na watoto wawili kulipa Kshs30,000 ili kugharamia chumba cha hoteli ya utalii hivi leo, na kulipa Kshs140 ili kuweza kunywa bia katika hoteli hiyo? Ikiwa tunaambiwa kwamba uchumi umeimarika, basi hili ni jambo ambalo linataka ufafanuzi zaidi wa Serikali. Tukiangalia hali ya barabara, tunaona kwamba hali hii haijaweza kuendelea. Barabara zetu zimeporomoka. Juzi nilitembelea sehemu ya Mt. Kenya na kuangalia barabara inayotengenezwa kutoka Nairobi hadi Nyeri ambako Rais mwenyewe anatoka. Kampuni inayotengeneza barabara hiyo ni Kirinyaga Construction Company. Masikitiko makubwa ni kwamba barabara ile iko katika hali mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa hapo mbeleni. Hii ni kwa sababu utengenezaji na ukarabati wa barabara ile ni duni mno. Naomba Serikali itilie mkazo uchunguzi wa barabara, hasa barabara ya Mombasa kwenda Malindi. Kampuni mbili zimepewa kandarasi ya kukarabati barabara hii. Kampuni ya Danjel itakarabati barabara hiyo kutoka Mombasa hadi Kilifi na ile ya Haye Construction itakarabati barabara ya Kilifi hadi Malindi. Masikitiko ni kwamba barabara hiyo, mbali na kwamba zabuni ilitolewa zaidi ya miezi sita iliyopita, haijaweza kukarabatiwa. Usafiri kutoka Kilifi hadi Mombasa sasa unachukua zaidi ya masaa mawili, kwa sababu magari hayawezi tena kupitia katika barabara hiyo. Ikiwa hawa wanakandarasi hawawezi kufanya kazi vizuri, kwa nini Serikali haiwezi kutafuta wanakandarasi wengine wanaoweza kutengeneza barabara zetu vizuri? Kuna uvumi kwamba barabara muhimu ya kuunganisha upande wa Kilifi na Mariakani 2062 PARLIAMENTARY DEBATES June 27, 2007 huenda ikatengenezwa. Naomba kwamba barabara hii iharakishwe ili kuwawezesha wasafiri wanaotoka Nairobi kupata njia ya kupitia Mariakani hadi Kilifi bila kuingia Jiji la Mombasa. Hatua hii itaendeleza hali ya uchumi katika Wilaya nzima ya Kilifi. Bw. Naibu Spika wa Muda, tumeambiwa na Waziri wa Fedha ya kwamba deni la Kshs66.4 bilioni wanaodaiwa wakulima wa pareto limefutiliwa mbali. Vile vile, deni la Kshs641 millioni wanaodaiwa wakulima wa kahawa limefutiliwa mbali. Hatupingi jambo hilo, lakini, je, wale wakulima wengine wanafaidika namna gani kutokana na hali hii? Katika sehemu ya Pwani, korosho ni zao la muhimu sana. Hata hivyo, zao hilo limesahauliwa na Serikali. Serikali inaonekana haina tena hamu ya kufungua kiwanda cha korosho na kuendeleza ukulima wa zao hilo katika sehemu ile. Hii ina maana kwamba uchumi wetu umeporomoka kutokana na uhafifu wa Serikali katika kuendeleza kilimo. Bw. Naibu Spika wa Muda, mnazi ni mti wenye mazao zaidi ya 40 yanayoweza kuleta hali bora ya uchumi. Hivi sasa, Serikali imeshindwa kukamilisha kazi ya kuendeleza zao la mnazi, ili kuhakikisha kwamba yale mazao 40 ambayo yako, kuanzia mbao, fito, makuti, madafu na kadhalika, yanawasaidia wananchi wa sehemu zile ambako zao hilo linakuzwa. Bw. Naibu Spika wa Muda, tumeambiwa kwamba Kshs1.3 bilioni zimetolewa na Serikali ili kuwezesha kupewa makao watu ambao walinyang'anywa makao yao. Tunataka ufafanuzi wa Serikali kama pesa hizi pia zitatumiwa kuwasaidi maskwota katika sehemu ya Pwani, ambao hivi sasa wanataabika. Kwa muda wa miaka minne, Serikali imekuwa inatuhadaa, kwamba hali ya uskwota itamalizika. Hadi leo, zaidi ya asilimia 80 ya wakaazi wa Pwani, wanaishi kama maskwota. Baada ya miaka 40, hatuwezi kukubali hali hii iendelee. Tunataka Waziri atufafanulie ikiwa hizi Kshs1.3 bilioni zitakwenda pia kwa maskwota wa Pwani, au tu kwa wale ambao wameondolewa katika makaazi yao katika sehemu ya Mt. Elgon. Bw. Naibu Spika wa Muda, hivi sasa, kuna mambo yanayozungumzwa kuhusu kuchelewesha uchaguzi hadi mwaka ujao. Mimi napendelea mabadiliko ya Katiba, lakini tusahau mafikira ya kuchelewesha uchaguzi hadi mwaka ujao. Wananchi wa Kenya wanataka uchaguzi ufanywe mwaka huu. Kama kuna ujanja wowote ili kuchelewesha uchaguzi huo hadi mwaka ujao, sisi tunapinga jambo hilo. Bw. Naibu Spika wa Muda, vile vile, ningependa Serikali iwe wazi kuhusu maeneo ya uwakilishi Bungeni. Inafaa kutueleza upesi ni maeneo mangapi na ya wapi ambayo yataweza kukatwa, kubadilishwa na kuongezwa. Kwa kuwa nchi hii hivi sasa ina shida ya pesa, sidhani kama tuna uwezo wa kuweza kuhudumia tena maeneo ya uwakilishi Bungeni 70 zaidi katika nchi hii. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa hayo machache, naunga mkono Hoja hii."
}