HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 220989,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/220989/?format=api",
"text_counter": 245,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Mwandawiro",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 253,
"legal_name": "Mwandawiro JD Mghanga",
"slug": "mwandawiro-mghanga"
},
"content": "Asante sana, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipatia hii fursa nami nichangie kidogo kuhusu Mswada huu wa Taasisi za wafanyakazi. Kutoka mwanzo, nataka kusema ingawa Wizara ya Leba imechelewa sana katika kuleta Miswada hii Bungeni, ni heri kuchelewa kuliko kutofika. Kwa hivyo, tunasema, haidhuru Waziri, tunakushukuru! Bora tu huu Mswada wa Taasisi ya Wafanyakazi ni kukumbuka kwamba sheria zote za leba ambazo tunazifanya hapa, si sheria ambazo zitawaokoa wafanyakazi. Tusiwadanganye wafanyakazi wa Kenya kwamba hizi sheria tunazowatengenezea ndizo sheria zitawakomboa. Hizi sheria ni za kutengeneza uwanja wa harakati za kitabaka za wafanyakazi, ili kuwe na fursa nzuri ya wafanyakazi kupambana kujiokoa. Kwa hivyo, tukiwa na sheria bora na nzuri zaidi za kuleta huo uwanja, na kuufanya uwe wazi - tuna wahusika wawili; mwajiri na mwajiriwa. Hao ndio wahusika wawili. Na hata tukiangalia hizi taasisi ambazo zimezungumziwa na huu Mswada, tukumbuke kwamba taasisi hizi ambazo tunazungumzia, kwa jumla, ni taasisi ambazo zinasaidia waajiri hapa kuwanyanyasa wafanyakazi. Ndio maana nataka kusisitiza kwamba taasisi ya muhimu zaidi ambayo ndio ngao ya wafanyakazi ni chama cha wafanyakazi. Chama cha wafanyakazi ndio taasisi ambayo ni muhimu zaidi na itakayowaongoza wafanyakazi waingie katika hizi harakati za kupambana kuhakikisha sheria hata zikiwa bora zaidi, kwamba zinatekelezwa kwa manufaa yao. Hii ni kwa sababu tunajua kila wakati mwajiri atakuwa anatafsiri sheria ili kulinda maslahi yake. Wafanyakazi nao watakuwa wanapambana kutafsiri sheria ili kulinda maslahi yao. kwa hivyo mawazo yote ambayo yako hapo ambayo yanalenga kujaribu kutoa picha kwamba tunaweza kutengeza sheria ile ambayo inamfanya mwajiri awe na huruma kwa wafanyakazi au tuseme Waziri wa Leba awahurumie wafanyakazi--- Historia ya nchi hii imeonyesha kwamba Wizara ya Leba, Waziri wa Leba na mwajiri ni kitu kimoja katika kulinda maslahi ya mwajiri dhidi ya wafanyakazi. Mpaka sasa nataka kuona tukiwa na waziri - naomba kwa hii miezi michache ambayo imebaki, Waziri huyu ambaye ametuletea hizi sheria nzuri sana Bungeni, aonyeshe mfano kwamba kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, kumekuwa na Waziri ambaye amesimama upande wa wafanyakazi. Ni rahisi sana kujaribu kufanya hivyo. Bw. Naibu Spika wa Muda, Waziri anaweza kurudi huko Taita Sisal Estate, Mwatate ama Salt Lick Lodge ambayo nilimuuliza Swali hapa akaenda, aende aone kwamba wale watu tangu aende, hawajatekeleza chochote na awaamuru watekeleze amri ambazo alitoa, kulingana hata na sheria za leba ambazo ziko sasa. Ndio kwa maana tukiangalia historia halisi ya nchi yetu, maanake sheria hazitoki hewani, lazima tukumbuke kwamba hii sheria ambayo inaletwa na huu Mswada inampa Waziri wa Leba nguvu nyingi kupita kiasi. Tukiitegemea, ni kama inajaribu kusema kwamba eti Waziri wa Leba atakuwa mzuri ambaye atatengeza sheria ambazo zitasaidia kila mtu; mfanyikazi na mwajiri. Nataka kusema kwamba Waziri wa Leba, tukimpatia hizi nguvu ambazo ako nazo katika hii sheria, tutakuwa tumekosea wafanyakazi na wataendelea na hiyo taabu milele. Ningetaka kuona kwamba Waziri wa Leba kama anateuwa taasisi yoyote nyingine katika sheria hii, ateue lakini iidhinishwe na taasisi zingine, hasa Bunge. Tukisema kwamba tumpe, kama tukiangalia, tunataka kusema kuwa Waziri wa Leba ndiye ana mamlaka kabisa hata ya kutengeneza halmashauri ya kitaifa ya nguvu kazi ambayo ni muhimu sana; ambayo ina uwezo wa kutengeza taasisi zingine za wafanyakazi. Mimi ningetaka kupendekeza kwamba hata kama anateuwa, ateue lakini kuwe na taasisi ya kuidhinisha kwa Bunge ili wawe watu ambao kwa kweli watakuja kusimama katika halmashauri, wale ni watu ambao wanaonekana wamepanda kwa kiwango cha May 17, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 1465 juu. Hasa, wawe ni watu ambao ni wasomi. Mimi ningependa kama wangekuwa ni wasomi wa mrengo wa kushoto. Lakini, haidhuru, wawe ni wasomi ambao wanaweza kutegemewa kwamba watatengeneza sheria ambazo zitasaidia kila mfanyikazi. Mfanyikazi ni mtu amenyanyaswa katika hii nchi mbele na nyuma kwa kila hali, tangu ukoloni mpaka sasa. Bw. Naibu Spika wa Muda, ukiangalia Mswada huu vizuri, katika kifungu 43(1), utaona kwamba ni Waziri wa Leba na Ustawi wa Wafanyakazi ambaye ana uwezo wa kumteua Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi. Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi ni mtu muhimu sana hasa tukitilia maanani hoja kwamba taasisi ya vyama vya wafanyakazi ndiyo taasisi pekee yake ambayo, katika mswada huu, inamtetea mfanyakazi halisi. Hizi taasisi nyingine tunaziunda tu tukidhani kuwa zitawasaidia wafanyakazi. Lakini kwa kweli, katika mfumo wa kibepari kama huu wetu, linalofanyika ni mabepari kuwasaidia waajiriwa tu. Ile taasisi ambayo inaweza kumkomboa mfanyakazi na kupigania kwa ukweli haki za wafanyakazi ni taasisi ya chama cha wafanyakazi. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa hivyo, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi sharti awe ni mtu ambaye ana heshima na taadhima ya hali ya juu. Aidha, sharti awe mtu ambaye hawezi kutumiwa na waajiri mabepari. Hafai kuwa mtu ambaye atakataa kuandikisha vyama vya wafanyakazi ambavyo vinaonekana kuwa vikali katika kutetea maslahi ya wafanyakazi. Bw. Naibu Spika wa Muda, hali halisi ilivyo sasa, wafanyakazi wengi wa Kenya - mimi nimeshirikiana sana na wafanyakazi wengi wa Kenya - wanalia kwamba kile Chama Kikuu cha Wafanyakazi nchini (COTU) kinawanyanyasa na kuwagandamiza wafanyakazi mbele na nyuma. Aidha, vyama vingine vya wafanyakazi haviwapatii haki wafanyakazi ambao ni wanachama wavyo. Kwa hivyo, kumekuwa na mwamuko na lazima tuende na nyakati. Wakati tunapozungumzia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, vile vile ni muhimu tutilie maanani kuwepo na mfumo wa vyama vingi vya wafanyakazi kama ilivyo katika nchi nyingine duniani. Haifai wafanyakazi walazimike kuwa chini ya COTU ama chama kingine ambacho kinadai kuwatetea maslahi yao ilihali viongozi wa vyama hivyo wamenunuliwa. Tunafahamu kwamba kila wakati wafanyakazi wanalalamikia haki zao, kuna baadhi ya viongozi wanaopewa chai. Katiba za vyama vya wafanyakazi hazijulikani na wafanya kazi wenyewe. Kwa hivyo lazima tuufanye uwanja huu uwe huru. Wafanyakazi sharti wawe na haki ya kutengeneza taasisi ya vyama vya wafanyakazi ambayo inaaminika. Sharti chama chochote kile cha wafanyakazi kiweze kuaminika na wafanyakazi wakisadiki na pesa zao. Chama hicho lazima kiweze kutetea maslahi yao. Kwa hivyo, yule ambaye atakuwa anaongoza taasisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi lazima awe mtu ambaye ameidhinishwa na watu wengi, kwa mfano, Wabunge. Sharti watosheke kwamba huyo mtu ana taadhima ya kutosha na kuaminika kwamba anaweza kuandikisha vyama vya wafanya kazi kama ilivyo, kwa mfano, katika tume ya wapigaji kura. Taasisi hiyo ndiyo itakuwa inaandikisha vyama vya wafanya kazi. Tusipokuwa na watu kama hivyo nilivyosema--- Bw. Naibu Spika wa Muda, nimesema mswada huu una mambo mengi sana. Kwa mfano, unapendekeza kwamba ni Waziri ambaye atachagua kila mtu na kutengeneza kila taasisi. Hii hali itatengeneza mtu ambaye atakuwa ni imla kwa wafanyakazi. Kwa hivyo, kwa mujibu wa kujaribu kuzifanya hizi taasisi zifanye kazi kwa maslahi ya wafanya kazi, lazima tuhakikishe kwamba wakati Waziri anateua watu, kuwe na taasisi nyingine ya kuidhinisha uchaguzi wake. Isiwe tu ni jukumu la mtu mmoja, yaani Waziri kuteua watu. Tunajua kwamba kwa kawaida mtu mmoja hawezi kuaminiwa na uwezo mkubwa. Mkimpa mtu mmoja uwezo mkubwa kama huo, kuna uwezekano kwamba huyo mtu atautumia vibaya. Katika historia ya harakati za wafanyakazi humu nchini, tunajua kwamba Wizara ya Leba na Ustawi wa Wafanyakazi, Waziri Wa Leba na Ustawi wa Wafanyakazi na taasisi nyingine zote zimekuwa zikitetea tu maslahi ya waajiri. Kwa hivyo Bw. Naibu Spika wa Muda, ni muhimu tuupitishe huu mswada. Lakini tuupitishe tukihakikisha kwamba wakati utarudishwa tuukamilishe kabisa. Tuurekebishe 1466 PARLIAMENTARY DEBATES May 17, 2007 tukihakikisha kwamba taasisi ile muhimu ya wafanya kazi sharti ipatikane katika sheria zote nyingine. Katika hizo sheria tunazotengeneza tuhakikishe kwamba chama cha wafanyakazi, tunakipa uwezo mkubwa na vile vile hatutengenezi chama cha wafanyakazi ambacho kitawapa watu binafsi wanaoajiri mamlaka makubwa ama kupendwa na Serikali iliyoko. Tusiwape nafasi ya wao kulazimisha wafanyakazi wengine kuwa chini yao ili hali wanawasaliti. Hakuna kitu watakachofanya. Vile vile, kuwe na uwezekano wa wafanyakazi kuhakikisha kwamba taasisi ya wafanyakazi ni ile itakayokuwa ya mfumo wa vyama vingi ili iweze kutetea kila upande wa wafanyakazi. Bw. Naibu Spika wa Muda, mwisho, Waziri wakati wote anapoteua watu, waweze kuidhinishwa na taasisi nyingine. Kwa maneno hayo, naomba kuunga mkono mswada huu."
}