GET /api/v0.1/hansard/entries/223461/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 223461,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/223461/?format=api",
    "text_counter": 213,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Khamisi",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 246,
        "legal_name": "Joseph Matano Khamisi",
        "slug": "joseph-khamisi"
    },
    "content": "Bw. Naibu Spika wa Muda, sababu ya kwamba taasisi hizo hazijapimwa wala kupewa stakabadhi za ardhi ni kuwa baadhi yake ziko katika ardhi za watu binafsi, ambao tunawaita \"absentee landlords\" . Baadhi yake kuna shule nyingi. Nimewahi kuleta katika Bunge hili Hoja au masuala katika kutaka kuziwezesha shule hizi au hospitali hizo kupewa stakabadhi za kumiliki ardhi. Kila mara tumepewa ahadi kutoka kwa Serikali kwamba hivyo ndivyo ingefanya. Lakini ninasikitika kwamba miaka minne tangu Serikali hii ichukue uongozi, hatujaona dalili yoyote kwamba kutatolewa stakabadhi za kuziwezesha taasisi hizo za umma kumiliki ardhi. Bw. Naibu Spika wa Muda, ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba hata vituo vya polisi katika sehemu yangu ya uwakilishi Bungeni vinakaa katika ardhi zisizokuwa zao. Hii ni kusema kwamba vituo hivyo vya polisi ni maskwota! Kwa kuwa ni maskwota, hawana title deeds za kuweza kumiliki sehemu hizo. Hivi majuzi katika stesheni ya polisi ya Mtwapa, ilibidi wananchi waliokuwa wanakaa kando ya stesheni ya polisi ile kuhamishwa kwa nguvu, kwa sababu pahali pale panawekwa bunduki na silaha za Serikali. Hivyo basi, kunahitajika kuwe na usalama wa kutosha kuwezesha kituo kile kifanye kazi kama inavyotakikana. Lakini hiyo imekuwa haiwezekani na hata ile ardhi ambayo kituo kile cha polisi kimepata haiwezi kukaliwa na inawabidi polisi wakae katika sehemu ndogo pale Mtwapa kwa sababu ardhi ambayo wangekwenda kuchukua haina stakabadhi za Serikali. Bw. Naibu Spika wa Muda, jambo hili pia linahusu kituo cha polisi cha Kijipwa katika May 2, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 1039 sehemu yangu, na hata kile kituo cha polisi cha Kilifi, ambapo ekari saba zinazosemekana ni za polisi zina maskwota na title deeds hazimo! Kwa hivyo, Hoja hii ni muhimu sana kwa sababu itaweka umiliki wa taasisi hizi mikononi mwa wananchi wenyewe, badala ya kuwa mikononi mwa watu binafsi ambao hila zao hazijulikani katika siku zinazokuja. Bw. Naibu Spika wa Muda, tuko na shule ambazo, vile vile, zina shida. Mwisho wa wiki iliyopita, nilikwenda katika shule moja inayoitwa Kararacha Primary School, na huko pia kuna shida kubwa ya wananchi kuingia katika eneo lile la shule kwa sababu hamna stakabadhi za shule ile. Kwa hivyo, naweza kusema kwa uthabiti kabisa kwamba shule nyingi, zaidi ya asili mia 80 ya shule za sehemu yangu ya Bahari hazina stakabadhi. Nina hakika kwamba tukiangalia katika hospitali, vyuo vya ufundi vijijini na haya mambo mengine ambayo yametajwa hapa, tutaona kwamba hali hiyo iko vile vile. Hii ndio sababu inanifanya niunge mkono Hoja hii; ili kwamba ikiwa watapimiwa ardhi ile, basi itawezekana kwamba sehemu zile zipewe stakabadhi zao ili ziweze kuzimiliki. Bw. Naibu Spika wa Muda, ajabu ya jambo hili ni kwamba wengi ambao wanaingia katika ardhi hizi za shule sio tu wale wanaotoka nje, lakini hata maskwota pia. Kwa sababu hakujakuwa na mipaka ya kutosha, maskwota wanaingia katika ardhi hizi na kuleta bughudha kwa wasimamizi wa shule hizi. Katika shule fulani, tumejaribu kutumia pesa za Constituencies Development Fund (CDF) kujenga ua au fence ili kuzuia watu hawa, lakini hili ni jambo la muda tu. Ukweli ni kwamba, stakabadhi hizi zinahitajika, na zinahitajika haraka sana, ili uvamizi wa ardhi kama tunavyouona katika sehemu zetu ukomeshwe mara moja! Bw. Naibu Spika wa Muda, Hoja hii inazungumzia kutolewa kwa fees ama ada zinazolipwa na shule kwa idara za Serikali. Hivi majuzi, tunaishukuru Serikali ilipokuja na ikajaribu kutoa stakabadhi hizi kwa kuondoa ile riba au interest iliyokuweko katika miaka yote hiyo. Sioni kuna shida gani au shida kubwa katika kuondoa hii pia, haswa kuhusu hizi taasisi ambazo tunazizungumzia hivi leo. Bw. Naibu Spika wa Muda, katika enzi hii ya Uhuru wa nchi hii, ni muhimu kwamba Serikali iwajibike katika kazi zake inazofanya. Mimi siamini kwamba, baada ya miaka 45 ya Uhuru, tutakuwa na Serikali ambayo haitilii maanani mali ya umma. Sielewi kwa nini inakuwa hivi, hali wakijua vizuri kwamba taasisi hizi ni za wananchi; kuna wananchi wanaokwenda katika shule na hospitali hizi, lakini inaonekana Serikali haitilii maanani uzima au umiliki wa ardhi hizi kwa sababu ambazo hazijulikani. Mimi naona kwamba wakati umefika kwamba Hoja hii ipitishwe, na ikipitishwa, tunataka iweze kutekelezwa upesi iwezekanavyo. Ikiwezekana, kabla ya uchaguzi, kwa sababu inaonekana kuwa Serikali hii inatia ndoano ya kuvuta watu kwa namna mbali mbali. Kwa hivyo, ikiwa ni kutia ndoano kwa kuvuta watu kwa jambo hili, mimi nitalikaribisha vizuri na tutaweza kuunga ndoano hiyo mkono ili kwamba mali hii iweze kuhifadhiwa kwa manufaa yetu na ya watu wanaokuja. Kwa hayo machache, Bw. Naibu Spika wa Muda, ningependa kuunga mkono."
}