GET /api/v0.1/hansard/entries/226167/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 226167,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/226167/?format=api",
    "text_counter": 293,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Wamwere",
    "speaker_title": "The Assistant Minister for Information and Communications",
    "speaker": {
        "id": 352,
        "legal_name": "Koigi Wamwere",
        "slug": "koigi-wamwere"
    },
    "content": " Ahsante, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipa nafasi hii ili niuchangie machache mjadala huu juu ya Ripoti ya PAC. Ninataka kuongeza sauti yangu kwa sauti za wenzangu waliosema kwamba tatizo kubwa la Kamati za Bunge, ambazo hukagua matumizi ya pesa za umma, ni kwamba, hatimaye, mapendekezo ya Ripoti za Kamati hizo hayatekelezwi. Hatimaye, inakuwa Kamati hizo zimefanya kazi ya bure, ambayo ukiitizama vizuri utaona kwamba inaweza pia kutajwa kama ufisadi. Ninasema hivyo kwa sababu sielewi ni kwa nini Bunge, ambalo linauwezo mkubwa, haliwezi kutumia uwezo huo kuhakikisha kwamba mapendekezo ya Ripoti za Kamati zake yanatekelezwa. Bw. Naibu Spika wa Muda, ukiliangazia jambo hili, utaona kwamba kuna uvivu wa makusudi. Kamati za Bunge hutayarisha mapendekezo, ambayo huletwa hapa kujadiliwa na kupitishwa, halafu tunarudi nyuma na kuacha mambo yaendelee kama yalivyokuwa mwaka baada ya mwingine. Kama huo si ufisadi, basi sijui maana ya \"ufisadi\" ni nini. Huo ni \"ufisadi\" ambao unatekelezwa na Bunge, ambalo linatakiwa liwe bingwa wa kuhakikisha kwamba katika nchi hii ufisadi umeangamizwa. Ninashindwa ni kitu gani kinacholifanya Bunge lisiwe na ari ya kuhakikisha kwamba mapendekezo ya Ripoti hizo yanatekelezwa, au hakuna ufisadi nchini. Utaona kwamba Ripoti hizo zinaongea juu ya vitendo vingi vyetu na, labda, tunaogopa kuzitekeleza tusije tukaumia sisi wenyewe. Kwa hivyo, ningetaka kuunga mkono matamshi ya mhe. Ethuro kwamba kama kwa kweli hatuna nia ya kuyatekeleza mapendekezo ya Ripoti za Kamati za Bunge, hakuna haja ya kuwa na Ripoti hizo. Ni afadhali tuwe waaminifu kwa dhamira yetu, tuseme kwamba hata sisi tunaunga mkono ufisadi nchini, potelea mbali, halafu litakalokuwa na liwe, badala ya kuongeza ufisadi juu ya ufisadi mwingine. Bw. Naibu Spika wa Muda, ukiiangalia Ripoti hii, utaona kwamba ina lugha ya kushangaza. Kinachozungumziwa ni wizi wa pesa za umma, lakini lugha iliyotumiwa katika ile Ripoti ya awali ya mkaguzi wa pesa za umma, pamoja na lugha iliyotumiwa katika Ripoti hii, ni ya kuficha wizi. Tunaubatiza wizi kwa maneno mengine ambayo yanaufanya uonekane kana kwamba umestaarabika, au kana kwamba si kitu hatari ambacho kinaweza kumwuudhi mtu; kwa hivyo, tunauacha wizi ubaki hivyo. Tulipokuwa katika Kamati ya ugaguzi wengine wetu tuliulizana: \"Kwa nini tuendelee kutumia lugha ya kunyerereza au kudanganya?\" Kama tunapigana na ufisadi, kwa nini neno \"ufisadi\" halimo katika Ripoti hizo? Hakuna pahali utaona neno \"ufisadi\" aidha katika Ripoti hii au ile ya mkaguzi wa fedha za umma. Mfanyikazi wa Serikali, ambaye alifanya wizi wa moja kwa moja anasemekana kwamba \"alijikopesha\" pesa za Serikali. Kusema kwamba \"alijikopesha\" pesa za umma ni kusema nini? Mtu anachukua pesa za Serikali na kuzifanyia shughuli zake za kibinafsi halafu Ripoti inaongea juu ya mtu \"aliyejikopesha\" pesa za umma. Bw. Naibu Spika wa Muda, mtu mwingine aliye nje ya Serikali akifanya hivyo, atakamatwa mara moja, kushtakiwa na kufungwa. Ni kana kwamba wizi Serikalini umehalalishwa kupitia lugha ambayo lengo lake ni kuficha uhalifu. Ningetaka kupendekeza kwamba kama Kamati zitakazofuata zitataka kufanikiwa zaidi ya Kamati zilizopita, ni lazima ziamue kutumia lugha ya wazi, na isiyo ya kuficha. Tunataka lugha ya kuita kijiko, kijiko, kuliita jembe, jembe, kuuita wizi, wizi na kuuita ufisadi, ufisadi. Lugha nyingine ni lugha za waongo, na lengo lake ni kuhakikisha kwamba wizi unaofanyika Serikalini hauadhibiwi moja kwa moja, na kwamba wizi huo unaendelea kuwepo. Ufisadi, hata tukiufanyia utafiti gani, tusipouadhibu tunapoteza wakati wetu. Kusema kweli, ufisadi katika nchi hii haukosi kuadhibiwa kwa sababu hakuna ushahidi. Ushahidi upo chungu nzima. Ukiziangalia Ripoti hizi tunazozungumza juu yake utaona kwamba ni Ripoti za April 17, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 673 ushahidi wa ufisadi, ushahidi ambao hautumiwi kuchukua hatua. Sasa ninashindwa kufahamu hili, kama ushahidi huu wote kuhusu ufisadi uliofanyika hautumiwi kuchukua hatua, na tunajigamba kwamba tumo vitani dhidi ya ufasidi, ni vita gani? Ni vita gani hivyo tunavyopigana dhidi ya ufisadi tunapokataa kuwaadhibu wafisadi waliodhihirika, ambao wametajwa katika Ripoti za Kamati za Bunge na Ripoti nyingine za Serikali? Bw. Naibu Spika wa Muda, afisi za Serikali zilizo na mamlaka ya kuwashtaki wafisadi, zinangojea nini? Kwa nini hazichukui hatua mara moja, kuwashtaki watu hao na kuwafunga? Ninadhani ufisadi utakua nasi mpaka Yesu arudi. Yesu akirudi, atatukuta tukiwa bado tu wafisadi kwa, sababu tumeogopa na kuamua kwamba hatutaki kupambana na ufisadi. Tumeamua juu ya jambo hilo. Tusidanganyane eti uchunguzi juu ya visa vya ufisadi unaendelea, ama kunafanyika jambo moja au lingine. Ushahidi ulioko ni mwingi mno. Ni uamuzi tumefanya kisiri. Tumeamua kwamba hatupigani na ufisadi katika nchi hii. Kama nilivyosema, ufisadi katika nchi hii utaendelea mpaka Yesu arudi. Kama Wakenya watakuwa na dhambi kubwa zaidi itakayowafanya wachomwe, itakuwa dhambi ya ufisadi, kwa sababu Wakenya ni wafisadi miongoni mwao kutoka walio katika ngazi za juu mpaka walio katika ngazi za chini. Tumeukumbatia ufisadi kwa mikono yetu yote. Huo ndio msingi wa utajiri wetu, lakini hatutaki kusema hivyo. Tukiongea juu ya ufisadi, unaweza kujiuliza: Hatima ya kashfa ya Goldenberg ni nini? Kulikuwa na tume ya kuchunguza kashfa ya Goldenberg ambayo ilitoa repoti yake, lakini hatujui hiyo ripoti ilipendekeza nini. Sijui kama ilipendekeza kuwa Goldenberg ilikuwepo ama haikuwepo. Hivi sasa, wale watu ambao walitajwa katika kashfa hiyo wamegeuka kuwa watakatifu. Hakuna mtu yeyote ambaye anawaita wafisadi tena. Hatuongei juu kashfa ya Goldenberg tena. Tumefika wapi, Bw. Naibu Spika wa Muda? Tumeambiwa hiyo kashfa ya Goldenberg imeisha. Huo ndiyo mwisho wake? Watu wamesafishwa na damu ya nani? Itakuwa damu ya NARC(K), damu ya Yesu au damu ya nani? Magazeti yanaongea juu ya watu hao kama viongozi wa kesho. Eti wengine watakuwa Rais wa nchi yetu mwaka wa 2012. Ni wale wale! Wengine wao wanatafuta urais. Jameni, mwizi anatafuta urais! Sasa, itakuwa ni nchi ya aina gani? Nakubaliana na wale ambao wanasema hii nchi ni ya ajabu. Katika nchi zingine zote, hakuna mtu mwenye kesi ya ufisadi kortini anaweza kuthubutu kusema anataka kuwania kiti cha urais. Hii ndiyo nchi ya pekee ambayo watu wafisadi na ambao wamehusishwa na kashfa kubwa kama ya Goldenberg wanathubutu kusimama na kutuambia ya kwamba miaka kadha ijayo, wanataka kuwania urais wa nchi yetu. Watatupeleka wapi? Mtu kama huyo atatupeleka jahanam! Mtu kama huyo akishika hatamu ya nchi hii, itakwisha! Lakini bado wanaendelea kusema wanataka kuwania kiti cha urais! Bw. Naibu Spika wa Muda, methali moja ya Kiswahili inasema: \"Johari za mtu ni mbili - akili na haya\" Kwa bahati mbaya, viongozi wetu wanakosa zote mbili. Wanakosa akili na, wakati huo huo, wanakosa haya. Hiyo ni kwa sababu, mtu mfisadi akisema anataka kuongoza nchi, basi nchi hiyo imo taabani kabisa. Kule kukosa somi ni kubaya kuliko kosa alilolifanya. Mtu kama huyo akishika hatamu za uongozi, tutaona cha mtema kuni, kama siyo kile kilichomfanya punda akose pempe. Ukweli wa mambo ni kwamba tuko taabani. Nilimsikia Bw. J. Nyagah akisema ya kuwamba mikataba iliyowekwa ya kulipa pesa wakati ujao ni lazima iheshimiwe. Mimi nikiulizwa ningesema: Mikataba iliyowekwa na Anglo Leasing haiwezi kuheshimiwa kwa sababu ilikuwa ya kimagendo. Sasa, usipomlipa mwizi, atakupeleka wapi! Unaweza kweli kuheshimu mkataba kati yako na shetani? Unaweza kuheshimu mkataba kati yako na mtu ambaye anakufanyia hila - mwizi? Katika nchi jirani ya Tanzania, hivi tunavyoongea, tangu wapate Rais wao mpya - mhe. Kikwete - wamekuwa wakitazama upya mikataba iliyowekwa hapo awali. Katika nchi nyingine kule Marekani Kusini, kuna Marais ambao wamechaguliwa na wameanza kuangalia mikataba kama ya Anglo Leasing iliyowekwa na Serikali 674 PARLIAMENTARY DEBATES April 17, 2007 zilizotangulia. Wengine wamesema mikataba hiyo haiheshimiki na wakaibadilisha. Waliziambia kampuni husika: \"Mfanye kazi na mikataba hii kama tilivyoibadilisha au mrudi mlikotoka!\" Walitii amri hiyo kwa sababu waliona hakuna mchezo. Sasa hivi, tunasema tunalazimika kisheria kulipa bilioni zilizoko katika mikataba hiyo ya uongo. Tukilipa bilioni hizo, nchi hii itafilisika! Tutakuwa tumehalalisha ufisadi. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa hivyo, kwa kweli ikiwa tuna nia ya kupigana na ufisadi, na isiwe sababu ya kuruhusu ufisadi huo wa Anglo Leasing uendelee, ni afadhali hata tupelekane katika mahakama ya dunia na hao wezi. Lakini tusithubutu kulipa pesa hizo. Itakuwa ni makosa! Hata wanasheria waseme nini! Kwanza, wanasheria hawana haja ya kutuambia kitu. Ufisadi huu wote umefanyika kwa mapendekezo yao. Ni huyu huyu Mkuu wa Sheria ambaye tumemuuliza mara nyingi ajiuzulu kwa hasara ambayo ameiletea nchi hii, lakini hasikii. Yeye ndiye alipendekeza na akasema kisheria: \"Hili linatosha na linafaa!\" Kama kuna watu ambao hawafai kusikilizwa katika nchi hii, ni wanasheria! Wapotelee mbali na utaalamu wao! Ni utaalamu wa wizi. Ukipata ufisadi-- Mpaka sasa, tunaimbiwa ya kwamba system hii imekuwa ni system ya majambazi. Mawakili ni majambazi. Mawaziri ni majambazi! Maaskofu ni majambazi! Kila mtu--- Hata vijana wa gheto wanasema hata wao ni majambazi! Nafikiria huo wimbo unatakiwa uwe wimbo wa Bunge hili, ndio tuelewe ya kwamba tumejenga mfumo wa kijambazi ambao umefanya kila mtu kuwa jambazi katika nchi hii. Kwa hivyo, hatuwezi kuambiwa: Kwa vile maoni ya mawakili ni hivo na hivi, ni lazima tutii mikataba ya kijinga kama hii. Hii ni mikataba ya kukatiliwa. Afadhali tupelekane na watu hao hadi mahakama ya dunia. Ikiwa tutashindwa, afadhali tushindiwe kule. Na, Bw. Naibu Spika wa Muda, tunaweza tukashindwa katika mahakama ya kibeberu na tukasema: \"Potelea mbali! Bado tunakataa kulipa! Mkitaka kuleta majeshi yenu, leteni!\" Kwani, watatufanya nini? Tunaweza kukataa kwa sababu hatuwezi kufuata mikataba ya kutumaliza. Kufanya hivyo ni kufanya makosa makubwa sana kwa vizazi vijavyo. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa hivyo, sikubaliani na Bw. J. Nyagah ya kwamba kilichopitishwa ni lazima kitekelezwe. Wakati umefika wa kusema mikataba hiyo ni mibaya. Tufanye vile majirani wetu Watanzania wanafanya. Tukatae kutekeleza mikataba ambayo ni mibaya, mibovu na ya kututia hasara. Itatufanya tusiamke miaka yote!"
}