GET /api/v0.1/hansard/entries/226792/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 226792,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/226792/?format=api",
    "text_counter": 146,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Kingi",
    "speaker_title": "The Assistant Minister, Office of the President",
    "speaker": {
        "id": 248,
        "legal_name": "Joseph Kahindi Kingi",
        "slug": "joseph-kingi"
    },
    "content": " Asante sana, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuzungumzia kuhusu mjadala ambao uko mbele yetu. Ninaanza kwa kumpongeza mhe. Khamisi, ambaye ameleta Hoja hii. Ninaiunga mkono kwa sababu ni Hoja ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo, hasa ya watu wa Kilifi. Ninayo imani kwamba Kamati hii ambayo tumeitaja hapa, itakapokubalika, itafanya kazi nzuri ambayo itakua na nia ya kufufua kiwanda hicho cha korosho kilichoko Kilifi. Historia ya kiwanda hiki cha korosho ilianza kitambo. Kiwanda cha mwanzo kabisa kilianza Kibarani. Na ni kiwanda ambacho kilijengwa 1923. Hii inamaanisha kwamba uchumi wa korosho na umuhimu wake ulitambulika mapema sana katika historia ya Mkoa wa Pwani na katika historia ya Kilifi. Baadaye, hiki kiwanda kilihamishwa na kikapelekwa mahali ambapo kiliko sasa na kikapanuliwa. Wakati kiwanda hiki kilikuwa kinafanya kazi, kilisaidia wakulima wengi na wananchi wengi wa Kilifi kwa kuinua hali yao ya uchumi. Katika miaka ya mbeleni, Wilaya ya Kilifi na pia wilaya ambazo zinazunguka Kilifi, hazikuwa katika kidimbwi cha umaskini ambapo kiko hivi leo. Leo hii, tunazungumzia habari ya umaskini Kilifi, katika Wilaya yetu mpya ya Kaloleni na hata Kwale, kwa sababu mazao ya muhimu katika eneo hili ni korosho na bixa. Mara tu kiwanda hiki kilipoanguka, wakulima walikosa mahali pa kuuza bidhaa zao. Jambo hili limesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi katika wilaya hii. Imani yetu ni kwamba kiwanda hiki cha Kilifi kitakapofufuliwa, wakulima watapata mahali pa kuuza mazao yao na matatizo yale ya uchumi ambayo yanaonekana katika sehemu hizo, bila shaka, yatapungua. Bw. Naibu Spika wa Muda, ningetaka kuongeza kwamba Kamati hii haihitaji kufanya kazi kwa muda mrefu, kwa sababu, walioleta matatizo haya wanajulikana tayari. Majina yao yako katika ripoti nyingi za PAC, PIC na katika habari nyingi ambazo zimeandikwa. Hata wengine wetu ambao ni wakulima wa korosho na tulikuwa wanachama wa District Co-operative Union ya Kilifi, pia tunazo habari nyingi kuhusu ni akina nani walioleta matatizo haya. Hata mimi, nitakuwa mtu wa kwanza kupeana taarifa vile ninavyojua kuhusiana na yaliyoendelea katika sehemu hiyo. Mbali na kuunda Kamati hii ili iweze kuchunguza ni akina nani waliolete matatizo hayo, ziko njia nyingine za haraka ambazo zinaweza kutumiwa na Serikali ili kufufua kiwanda hiki. Kama tulivyoambiwa, kiwanda hiki kiliuzwa na Benki ya Barclays kwa sababu wakurugenzi ambao walikuwepo wakati huo, walikuwa wamechukua mkopo wa Kshs40 milioni, ambao walishindwa kulipa ndipo Benki ya Barclays ikauza kiwanda hicho. Lakini ukichunguza, utapata kwamba hata wale wakurugenzi ambao walikuweko wakati ule, hawakuwa wamekubalika na wakulima. Pia, njia ambazo zilitumiwa kuhamisha hisa za wakulima hazikukubaliwa. Wakulima walikuwa na hisa za kiwango cha asilimia thelathini na tano. Bw. Naibu Spika wa Muda, hisa hizo zilihamishwa na kumilikiwa na Wahindi wengine ambao waliingia katika kiwanda hicho kinyume cha sheria. Kwa hivyo, kuna uwezekano wa kutumia njia iliyopendekezwa na Bw. Wetangula: Kwamba, tunaweza kushtaki na kuchukua njia fupi zaidi kuliko njia hii iliyopendekezwa. Hata hivyo, tunakubaliana nayo ili ukweli uweze kujulikana. Tumezungumza na Waziri anayehusika na maswala ya vyama vya ushirika. Tumemwambia Waziri kwamba tumeshazungumza na wasimamizi walioko sasa katika kiwanda hicho, na kwamba wameonyesha kwamba wako tayari kufanya mazungumzo na wakulima pamoja na Serikali ili hisa za wakulima zilizokuwa zimepotea ziweze kununuliwa na Serikali, halafu April 11, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 521 baadaye Serikali iziuze kwa wananchi ili wananchi waweze kujisikia kwamba kiwanda hicho ni chao, na waweze kukipatia shikamizi. Kwa hivyo, kuna njia nyingi ambazo zinaweza kutumiwa kuhakikisha kwamba kiwanda hicho kinafufuliwa ili wananchi wapate mahali pa kuuza mazao yao. Bali na kiwanda hicho cha korosho, kuna viwanda vingi ambavyo vimeanguka huko Pwani. Ningependa kuitumia fursa hii kumwomba Waziri anayehusika kuhakikisha kwamba kiwanda cha Mariakani Milk Scheme kimefufuliwe haraka ili wananchi wapate mahali pa kuuza bidhaa yao ya maziwa. Pia tungependa kiwanda cha sukari kule Ramisi kifufuliwe ili kilimo cha miwa kiweze kuwasaidia wananchi katika sehemu hiyo. Ninaipongeza Serikali kwa kukifungua kiwanda cha Kenya Meat Commission (KMC) cha Kibarani, Mombasa, ambacho kilikuwa kimeanguka. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba viwanda hivyo vyote vimefufuliwa ili malengo yaliyokuwepo wakati vilipoundwa yaweze kutimizwa. Moja ya malengo hayo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba umaskini umeondolewa miongoni mwa wakazi wa sehemu hizo ili waweze kujimudu maishani. Kwa hivyo, ninaiunga mkono Hoja hii, nikiamini kwamba Wabunge wenzangu pia wataiunga na pia pamoja na Kamati iliyopendekezwa, ili iweze kufanya kazi yake kwa haraka zaidi. Ahsante, Bw. Naibu Spika wa Muda."
}