GET /api/v0.1/hansard/entries/228719/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 228719,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/228719/?format=api",
    "text_counter": 189,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Kingi",
    "speaker_title": "The Assistant Minister, Office of the President",
    "speaker": {
        "id": 248,
        "legal_name": "Joseph Kahindi Kingi",
        "slug": "joseph-kingi"
    },
    "content": " Ahsante sana, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa March 29, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 279 ufunguzi wa kikao hiki cha Bunge. Nakubaliana na wenzangu walionitangulia kwamba Hotuba ya Rais ilikuwa nzuri. Ilikuwa na mawaidha mazuri. Ilionyesha mafanikio ya Serikali yetu kutoka mwaka wa 2003 hadi sasa. Sisi kama Wabunge waliochaguliwa na wananchi na kupewa jina la kuheshimika tunalo jukumu kubwa sana la kutunza heshima hiyo kwa vitendo na mazungumzo yetu. Hii ni kwa sababu wananchi wale ambao tunawaakilisha, mara nyingi watafuatilia maneno yale tunayowaambia. Kwa hivyo, tukitaka kuwapotosha, mara nyingi inakuwa rahisi sana kuwapotosha wananchi. Tukitaka kuwaambia ukweli, pia tuwaambia ukweli. Kusimama mbele ya Bunge na kusema kuwa Serikali haijafanya lolote, si jambo la kweli kwa sababu Serikali imefanya mengi ambayo yanaonekana kila mahali katika Jamhuri yetu ya Kenya. Kwanza, uchumi wa taifa hili ambao ulikuwa umezorota sana unaendelea kuimarika. Kwa sababu unaimarika, wananchi popote walipo, wanaona faida za uchumi huu ambao umeimarika. Wenzangu wamesema, na mimi narudia, kwamba mfumo wa elimu ya msingi bila malipo ni dalili moja. Kuimarishwa kwa huduma za afya ni dalili nyingine ambayo tunaiona. Tukienda kwa sekta ya barabara, utapata kwamba kuna kazi nyingi za barabara ambazo zinafanywa kila mahali katika Jamuhuri yetu ya Kenya. Kuna fedha ambazo zimetengwa ili kusaidia maendeleo ya sehemu za uwakilishi Bungeni. Kuna pesa ambazo zimetengwa za kusaidia vijana na miradi yao ya biashara. Viwanda vingi ambavyo vilikuwa \"vimekufa\" sasa vinafufuliwa. Juzi tu tulikuwa huko Mombasa na tukashuhudia kufufuliwa kwa kiwanda cha Kenya Meat Commission (KMC) ambacho kwa zaidi ya miaka 25 kilikuwa hakifanyi kazi. Kwa hivyo, Bw. Naibu Spika wa Muda, tunaweza tukasema mengi yale ambayo yanaendelea na mambo ambayo yanaonekana kila mahali. Kwa hivyo, nafikiri ni jukumu letu kumpongeza Rais ambaye, tangu achukue hatamu ya uongozi, akishirikiana na wafanyakazi wengine pamoja na sisi, tumeweza kutoa taifa hili mahali ambapo palikuwa hapana matumaini, mpaka tukalifikisha mahali ambapo sasa pana matumaini. Tunachohitaji ni kufahamu ya kwamba Roma haukujengwa kwa siku moja na kwamba kujenga taifa si kitu ambacho kinaweza kufanyika kwa siku moja. Kwa hivyo, sisi kama Wajumbe, tunalo jukumu la kueleza Serikali mahali pale ambapo tunaona panahitaji kufanywa kazi zaidi; mahali pale ambapo tunaona panahitaji kuangaziwa zaidi, ili Serikali ikishirikiana na sisi, tuweze kuonyesha au kufanya kazi pamoja. Sehemu moja ambayo mpaka sasa bado inawakera wananchi wengi ni huduma ya afya. Sisi Wabunge mara nyingi tunapata wananchi wale ambao tunawaakilisha wakija nyumbani na ofisini mwetu wakiwa wana matatizo ya afya zao. Wengine wao hutaka kwenda hospitali ili waweze kupasuliwa ndio afya yao iwe nzuri. Mara nyingine, kuna gharama ambazo wananchi hawa maskini hawawezi kuzimudu. Upasuaji ni ghali! Mara nyingine, unaweza kugharimu hata kiasi cha Kshs20,000, Kshs30,000 na kwingine hata Kshs100,000. Sasa ikiwa tutawaachia gharama hii, wananchi maskini ambao hata pesa za chakula hawawezi kupata, basi sisi kama Serikali hata tukisema kwamba uchumi umeimarika na wananchi wanaona furaha, inakuwa vigumu kidogo kwa wananchi kukubaliana na sisi. Kwa hivyo, ningetaka kutoa mwito kwa Wizara ya Afya ihakikishe ya kwamba wananchi ambao wanahitaji matibabu maalum, wameweza kupatiwa matibabu hayo bila malipo, ili waweze kwenda nyumbani na kuangalia shughuli nyingine za maendeleo. Wengi wa wananchi hao hawana kazi au vibarua vingine ambavyo vinawapatia mapato. Kwa hivyo, hatuwezi kutarajia kwamba wataweza kulipa gharama zile ambazo zinahitajika. Bw. Naibu Spika wa Muda, tumezungumza habari ya kufufuliwa kwa viwanda. Wananchi wengi wa Mkoa wa Pwani bado wanangojea kuona ufufuzi wa kiwanda cha maziwa cha Mariakani. Pia, tunangojea kuona ufufuzi wa kiwanda cha sukari cha Ramisi na kiwanda cha korosho cha Kilifi. Kwa hivyo, tungetoa mwito kwa Wizara zinazohusika, ambazo nyingi zimefanya kazi nzuri kufikia sasa, kuangazia Mkoa wa Pwani ili kuhakikisha kwamba viwanda vile ambavyo havifanyi kazi au havijafanya kazi kwa muda mrefu, vinafufuliwa, ili viweze kuanza kufanya kazi. Jambo hili likifanyika, wananchi wa Pwani wataweza kuvitumia kwa uchumi wao. 280 PARLIAMENTARY DEBATES March 29, 2007 Tumezungumzia mara nyingi kuhusu mfumo wa elimu. Tumesema ya kwamba Pwani ni jimbo moja katika taifa hili ambalo linahitaji chuo kikuu. Jambo hili limezungumziwa mara nyingi katika sehemu nyingi lakini mpaka sasa, Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia bado hazijaitikia mwito wa viongozi au mwito wa wananchi wa Pwani. Chuo kikuu kinapojengwa mahali kilipo, kina faida nyingi. Hasa, kwa vijana au wale wanaotaka kufuatilia mambo yao ya elimu, huwa ni vizuri chuo hiki kikiwa karibu nao kwa sababu hupunguza gharama ya elimu yao. Kwa hivyo, ukosefu wa chuo kikuu katika Mkoa wa Pwani unafanya elimu kwa vijana wetu kuwa ghali kwa sababu ni lazima wasafiri mbali watafute mahali pa malazi ambapo pia watalipia. Hili swali tunaona ni swali ambalo linaweza kumalizwa kwa kupatiwa chuo kikuu. Kuna sehemu nyingi ambazo zinaweza kumudu kuwa na chuo kikuu. Tuna sehemu kama Kilifi Institute of Agriculture, Mombasa Polytechnic, Matuga na hata chuo kilichonuiwa kujengwa huko Taita Taveta. Kwa hivyo, Wizara ya Elimu, ile ya Sayansi na Teknolojia inastahili tu, kutafuta mahali pamoja ili nasi pia tuwe na chuo kikuu. Bw. Naibu Spika wa Muda, swala la ardhi linashughulikiwa. Hata jana tulipata ripoti ya kwamba Waziri wa Ardhi alikuwa huko Kwale ambapo alikutana na wananchi. Maswala mengi ambayo yalikuwa yanawatatiza wananchi yaliangaliwa. Jambo hili la ardhi linatakikana kutatuliwa kwa haraka zaidi. Labda, maofisa wengi yafaa waajiriwe ili tuhakikishe kwamba kazi inafanyika kwa haraka ndio wananchi waweze kutambua kuwa Wizara ya Ardhi inafanya kazi katika sehemu zote za Jamuhuri ya Kenya. Pesa za CDF ni pesa ambazo zinasaidia sehemu nyingi za Jamuhuri ya Kenya. Miradi mingi ya elimu, afya na barabara imeweza kutekelezwa kwa kutumia pesa hizi. Kwa hivyo, nawaunga mkono wenzangu ambao wametangulia kusema kuwa kuna umuhimu wa kuongeza kiwango cha pesa hizi, ili angalau kila sehemu wakilishi Bungeni kwa kila mwaka iweze kupata pesa zisizopungua Kshs100 milioni. Tukifanya hivyo, mambo mengi ambayo yanatutatiza katika sehemu zetu za uwakilishi Bungeni tutaweza kuyamudu sisi wenyewe. Bw. Naibu Spika wa Muda, ningetaka pia kutoa mwito kwa viongozi katika wilaya zile ambazo tumeunda hivi majuzi na bado wanazozana kuweza kukaa, kuzungumza na waelewane ili tuweze kuwapatia wilaya yao kama ilivyo nia ya Serikali. Kwa hayo machache, nataka kuiunga mkono Hotuba ya Rais na kusema kwamba sote yafaa tumuunge mkono na tumpatie muda zaidi, ili aweze kuendelea na kazi yake nzuri anayofanya."
}