HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 229112,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/229112/?format=api",
"text_counter": 172,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Mwandawiro",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 253,
"legal_name": "Mwandawiro JD Mghanga",
"slug": "mwandawiro-mghanga"
},
"content": "Iwapo tutazingatia maswala ya kiuchumi na maswala mengi mengineyo, basi tungeweza kufanya vizuri zaidi kama tungepanga mipango yetu kwa fikra zetu wenyewe kama Wakenya na kama Wafrika, tukiangalia hali halisi ya nchi yetu. Tukitazama duniani, nchi ambazo zimeweza kujikwamua kiuchumi na kwenda mbele ni nchi zilizokataa kufanya sera na mikakati yao kwa kuongozwa na watu kutoka nje. Kadiri ambapo Wakenya tutaendelea kuongozwa na kuyumbishwa haswa na mabeberu kutoka nje tukifanya sera zetu, hapo tutakuwa tumepotea zaidi. Wale ambao wanafikiri kuwa mabeberu watatuokoa ni watu waliopotoka. Ikiwa Serikali iliyoko ndio yenye jukumu la kuulinda uhuru wa kitaifa, nasikitika kwamba Serikali hii ndiyo inapeana Mkenya kwa Wamerekani na kuwaruhusu wamhoji ndani ya nchi hii, halafu kumpeleka Guantanamo Bay, sehemu ambayo mabeberu Wamarekani wameinyang'anya Cuba na kuivamia hiyo nchi. Sisi tunashinikizwa na Wamarekani, sijui kwa sababu ya misaada au marupurupu gani, kuruhusu vyombo vya usalama vya Marekani kuingia ndani ya mipaka ya nchi yetu na kuwakamata watu wetu, haswa wa kutoka Pwani. Wanajaribu kutubagua, hasa kidini. Wanasema kuwa Waislamu ndio wanaoungana na magaidi, hivyo basi wanawakamata watu waliozaliwa hapa kutoka nyumbani mwao na kuwapeana kwa Wamarekani. Nafikiri kuwa huo ni ukoloni mamboleo na ni usaliti mkubwa sana kwa nchi yetu. Kusema ukweli, ni aibu kusikia kwamba vijana wamekamatwa na wanapelekwa katika hali ambayo wanaweza kuteswa, maanake pale Guantanamo Bay ni pahali ambapo Wamarekani wanawatesa watu duniani, na sisi tumepeana watu wetu wapelekwe huko. Huo ni usaliti mkubwa kwa nchi yetu, na Serikali ni lazima iwajibike kwa jambo hilo. Bw. Naibu Spika wa Muda, kuhusu suala la marekebisho ya Katiba, tunafurahi kwamba Serikali sasa imekubali shindikizo za wananchi za kufanywa marekebisho kiasi ya Katiba. Serikali imekubali kufanya mazungumzo na Upinzani kuhusu marekebisho muhimu ya Katiba, ambayo yatatekelezwa kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Si lazima wakati wote Serikali ingojee mpaka isukumwe kwa maandamano ama maneno ndipo ifanye jambo fulani. Inatakikana Serikali iwe kwenye msitari wa mbele wakati wote katika kutoa hoja kama hiyo. Hata hivyo, tunaipongeza Serikali kwa kukubali kufanya mazungumzo na Upinzani juu ya suala hili. Hivyo ni kukubali kwamba demokrasia ipo katika nchi yetu. Kwa hivyo, tunasema kwamba ni pongezi kubwa kwa 232 PARLIAENTARY DEBATES March 28, 2007 Serikali yetu. Kuhusu suala la elimu, ninaipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango wa elimu ya bure katika shule za msingi. Ingawaje mpango huo umekumbwa na matatizo chungu nzima, hiyo ni hatua muhimu sana ambayo Serikali imechukua. Tunachopendekeza ni kwamba, kwa sababu hali ni ngumu zaidi katika shule za upili, tunaiomba Serikali ifanye juhudi za kuanzisha mpango wa elimu ya bure katika shule hizi kufikia mwaka ujao. Ninaamini kwamba Serikali inaweza kutoa elimu ya sekondari bila malipo. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumepiga hatua kubwa zaidi, pamoja na kuwaajiri kazi walimu wengi zaidi. Bw. Naibu Spika wa Muda, tusikubali shindikizo za shirika la IMF ama Benki ya Dunia, eti tusiwaajiri watu wetu kufundisha shuleni ama kufanya kazi katika hospitali. Wanaoajiriwa kazi ni Wakenya. Pesa zinazotumiwa kuwalipa mishahara hazipotei, bali zinatumika humu nchini. Kwa hivyo, tutekeleze sera zetu kulingana na mahitaji yetu. Ninafurahi kwamba wakati huu takribani asilimia 97 ya Bajeti yetu inakidhiwa na fedha zetu sisi wenyewe. Kwa hivyo, sasa tunaweza, kwa ujasiri, kutekeleza sera zetu sisi wenyewe. Kama mkazi wa Wilaya ya Taita-Taveta, ninatarajia kwamba kabla ya Bunge hili kuvunjwa kwa sababu ya uchaguzi mkuu ujao, Serikali itakuwa imeleta Mswada wa kurekebisha sheria kuhusu wanyama pori, ambayo itasema kwamba takribani asilimia 25 ya mapato yanayotokana na mbuga za wanyama pori yabaki kufanya maendeleo katika wilaya husika. Kwa sababu Wilaya ya Taita-Taveta inapakana na mbuga za wanyama pori za Tsavo Mashariki na Tsavo Magharibi, tunataka tupewe asilimia 25 ya mapato yanayotokana na mbuga hizo ili tufanye maendeleo katika wilaya hiyo. Bw. Naibu Spika wa Muda, haiwezekani kwamba zaidi ya asilimia 60 ya ardhi katika wilaya hiyo ni mbuga za wanyama pori halafu tusipate cho chote kutokana na mbuga hizo. Wakenya kwengineko wana kahawa, chai na samaki. Sisi, wakazi wa Taita-Taveta, tuna wanyama pori. Kwa hivyo, tunataka maendeleo yetu yatokane na mbuga za wanyama pori. Tunajua kwamba pesa nyingi zinazotumika katika Bajeti ya nchi hii zinatokana na utalii, na shughuli nyingi za kitalii zinafanyika katika Mkoa wa Pwani. Kwa hivyo, tunataraji kwamba jambo hilo litafanyika mara moja. Vile vile, tunasema kwamba ni lazima Serikali itembelee mikoa na kutayarisha sera zake pamoja na wananchi. Tatizo kubwa miongoni mwa Mawiziri na viongozi wengine Serikalini ni kuketi maofisini huku Nairobi na kutengeneza sera zinazowahusu wananchi mikoani. Katika Wilaya ya Taita-Taveta, kwa mfano, kuna wenyeji kutoka Wundanyi na sehemu za Taveta, ambao baadhi yao ni wafanyikazi wa umma, na haswa walimu, ambao wanapata marupurupu kwa kuhudumu katika sehemu zenye shida kama vile Voi na Mwatate. Lakini, walimu wanaohudumu katika sehemu za Wundanyi na Taveta, ambazo zina mazingira magumu kama yale ya Voi na Mwatate, hawalipwi marupurupu hayo. Kwa hivyo, tunawataka wanaohusika na swala hilo Serikalini waende wakaangalie hali halisi katika sehemu hizo na wairekebishe hali hiyo ili iambatane na ukweli. Si vyema kwao kuketi tu hapa Nairobi na kufanya mapendeleo kwa sababu, labda, watu fulani waliwatembelea katika afisi zao. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa ufupi, ninafurahia kwamba Serikali inayamulika maswala yanayowahusu vijana na wanawake. Lakini ningependa kusema kwamba hizo ni sera rahisi. Tusigawanye nchi katika viwango kulingana na umaskini miongoni mwa wanawake, vijana na wazee. Tuuangalie umaskini kwa jumla. Hiyo ni sera ndogo tu inayotokana na fikira duni zinazoletwa na wageni, na ambazo zinatupotosha. Tuuangalie umaskini kama tatizo linaloikumba kila sekta ya nchi hii halafu tujaribu kupigana nao kwa ujumla. Tusijaribu kulitatua tatizo hilo kupitia sera rahisi ya kuwatengea kiasi fulani cha fedha wanawake, vijana, walemavu na wazee, March 28, 2007 PARLIAMENTARY DEBATES 233 tukidhani kwamba tutafaulu. Kwa hayo machache, ninaomba kuiunga mkono Hoja hii."
}