GET /api/v0.1/hansard/entries/232076/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 232076,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/232076/?format=api",
    "text_counter": 148,
    "type": "other",
    "speaker_name": "",
    "speaker_title": "",
    "speaker": null,
    "content": "Bw. Naibu Spika wa Muda, asante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuichangia Hoja hii ambayo madhumuni yake ni kuanzisha bandari huru ya Mombasa. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwanza, ningependa kumpongeza mhe. Balala kwa kuileta Hoja hii mbele ya Bunge hili. Nafanya hivyo kwa sababu miaka kadha wa kadha iliyopita wakati wa Serikali ya Moi, kulikuwa na kamati iliyoundwa ili kuangalia jambo hili na nakumbuka vizuri kwamba mhe. Nicholas Biwott alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ile ili kwamba aangalie mikakati na utaratibu unaotakikana kuanzisha bandari huru ya Mombasa. Kwa bahati mbaya, hatujasikia lolote kuhusu kamati ile. Kwa hivyo, nampongeza Mbunge wa Mvita kwa kuleta Hoja hii mbele ya Bunge hili. Bw. Naibu Spika wa Muda, hili si wazo jipya ulimwenguni. Ni wazo ambalo tayari linatekelezwa katika mataifa mengine. Tunapata mfano wa Singapore, Dubai pamoja na Hong Kong na nchi nyingine kadha wa kadha ambazo zimeona umuhimu wa kuanzisha bandari huru ili kuwawezesha kuinua uchumi wa nchi zao na pia kubuni nafasi za kutosha za kuleta biashara katika nchi zao na kutoa makazi kwa wananchi wao. Kwa hivyo, kitu ambacho tunataka kufuata ni kuangalia mikakati ambayo tayari imeshafanywa na nchi zile ambazo zimeanzisha bandari huru ili kwamba tupate kuepukana na makosa ambayo pengine huenda wakawa wameyafanya; ili kwamba wakati tunapoanzisha bandari yetu huru, itaweza kutekeleza shughuli na madhumuni tunayotaka yatekelezwe. Bw. Naibu Spika wa Muda, Bandari ya Mombasa ndio utajiri mkubwa zaidi wa Pwani na nchi hii katika upande wa uzalishaji wa fedha na pia usaidizi wa ustawishaji wa biashara katika nchi ambazo hazina fuo za bahari. Bandari ya Mombasa hivi sasa inatekeleza na kusaidia uchumi wa nchi kadha wa kadha. Hivi sasa, bidhaa zinapitia bandari ile na kuna matatizo mengi kama vile msongamano wa bidhaa, kucheleweshwa kutolewa kwa bidhaa kutoka bandarini, ufisadi na ajira. Ninafikiri kwamba, badala ya baraza tulilonalo hivi sasa, ambalo, kusema kweli, halitekelezi shughuli zote zinazopaswa kutekelezwa katika bandari, itakuwa jambo la busara kuanzisha bandari huru na baraza litakaloisimamia, ili maswala tunayozungumzia hapa yaweze kupewa kipao mbele. Bw. Naibu Spika wa Muda, bidhaa nyingi huingia nchini kila siku, kupitia Bandari ya Mombasa. Bidhaa hizo hutozwa ushuru mkubwa mno. Ushuru huo mkubwa unawafukuza baadhi ya wafanyibiashara wanaoleta bidhaa na baadhi ya watu ambao wangependa kufanya biashara katika bandari hiyo. Kuanzishwa kwa bandari huru kunaweza kusaidia kuleta biashara zaidi pamoja na kuleta watalii zaidi. Itakuwa bandari ambapo wafanyibiashara watanunua bidhaa kwa bei inayofaa na kuwawezesha kuziuza bidhaa hizo na kupata faida kubwa. Kadhalika, italeta hali ambayo itawezesha bidhaa nyingi kutiririka katika nchi hii, kama hali ilivyo Dubai. Hivi sasa, 4010 PARLIAMENTARY DEBATES November 29, 2006 Wakenya husafiri hadi Dubai, hununua bidhaa na kuzileta humu nchini. Kwa nini? Kwa sababu ya bei nafuu zinazotozwa katika nchi hiyo, kupitia utaratibu wa bandari huru. Vile vile, utoaji wa ajira ni muhimu. Hivi sasa, kuna ubanifu wa utoaji wa ajira katika Bandari ya Mombasa. Kama alivyosema Bw. Balala, wafanyikazi wengi wa pwani, na hata wa bara, wameajiriwa katika hali ya kibarua miaka nenda, miaka rudi. Hii ni kwa sababu ya kutokuweko kwa utaratibu na mwelekeo kabambe. Hali hiyo inawaogopesha wasimamizi wa makampuni katika bandari hiyo kutoa kazi za kudumu kwa wananchi wa sehemu hiyo. Wanabahatisha kwa kutoa kazi za vibarua, kwa sababu hawajui iwapo biashara yao itaendelea vyema kesho au itaendelea vyema kesho kutwa. Tukiwa na bandari huru, kutakuwa na upanuzi wa biashara, ambao utawezesha kuweko kwa kazi za kudumu na ambazo zitaweza kuwasitiri wananchi katika sehemu hiyo. Vile vile, uchumi utakua. Kumetajwa hapa kwamba bandari hiyo itabidi ipanuliwe katika eneo lake. Bw. Balala amesema kwamba kuna hektea 4,000 za ardhi ambazo zinaweza kutumiwa kwa shughuli hii. Iwapo jambo hili litafanyika, uchumi wa sehemu hiyo utanawiri na wananchi watapata faida kutokana na mpango wa bandari hiyo. Vile vile, biashara ndogo ndogo zitanawiri. Kadiri watu watakavyozidi kumiminika katika sehemu hiyo, ndivyo kadiri biashara ndogo ndogo zitakavyonufaika. Barabara, pamoja na viunda msingi vingine, zitapanuka na kunufaika. Kwa hivyo, ninauunga mkono Mswada huu, ambao ni muhimu sana kwa Pwani na kwa eneo hili la Kenya. Kuundwa kwa baraza lililopendekezwa katika Mswada huu ndiyo njia ya pekee inayoweza kutusaidia kupambana na matatizo mengi tuliyo nayo; ambayo, hivi sasa, yanatukumba kwa sababu hatuna uwezo wa kupanua shughuli za biashara katika bandari hiyo. Itakuwa muhimu kwa Wabunge, kupitia Kamati maalum husika, kuzitembelea nchi ambazo, tayari, zina bandari huru, ili waweze kujifunza njia za kisasa za kuendesha biashara hiyo. Tunaposema hivyo, hatusemi kwamba sisi, watu wa Pwani, hatutaki kujumuishwa katika mambo hayo. Tunakata kuhusika kikamilifu katika upanuzi na uendeshaji wa bandari hiyo. Kwa hivyo, tunapozungumzia suala la kuanzishwa kwa bandari huru, tusiseme kwamba tunawafungulia njia watu kutoka nje kuja kuchukua nafasi za watu wa Pwani katika shughuli hii. Ni masikitiko makubwa kwamba licha ya kuweko kwa Bandari ya Mombasa katika sehemu ya Pwani, wananchi wa sehemu hiyo hawafaidiki kutokana na Bandari hiyo. Wanafaidika tu kwa kazi za kibarua. Watu wanaandikwa mwezi wa kwanza halafu mwezi wa pili hufutwa. Wanaandikwa tena mwezi wa tatu halafu mwezi wa nne wanafutwa. Ningependa kumwambia Bw. Balala kwamba baada ya kupitishwa kwa Hoja hii, katika shughuli ya kuutayarisha Mswada tunaoutarajia, atilie maanani sana faida itakayopatikana kwa wazalendo wa Pwani, na siyo kwa watu fulani tu. Kwa hivyo, ningependa kuliomba Bunge liipitishe Hoja hii upesi iwezekenavyo ili Mswada tunaoutarajia uandikwe na kuletwa hapa tuupitishe na, inshallah, Mungu akitusaidia, tuweze kuanzisha bandari huru katika Mkoa wa Pwani. Kwa hayo machache, ninaunga mkono."
}