HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 238512,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/238512/?format=api",
"text_counter": 193,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Wamwere",
"speaker_title": "The Assistant Minister for Information and Communications",
"speaker": {
"id": 352,
"legal_name": "Koigi Wamwere",
"slug": "koigi-wamwere"
},
"content": " Bw. Naibu Spika wa Muda, kwanza, ningetaka kumpongeza Prof. Anyang'-Nyong'o kwa kuleta Hoja hii ambayo tunaomba kuunga mkono. Tunatoka katika enzi ya giza; kule ambako mambo mengi sana yalifichwa. Tunaelekea kule ambako tunaamini kutakuwa na mwangaza. Kwa sababu hiyo, itakuwa vigumu sana Mbunge yeyote kupinga Hoja ya aina hii. Kusema kweli, Wizara imetayarisha Mswada kuhusu uhuru wa habari. Mswada huu utakuwa tayari hivi karibuni. Mara tu utakapokuwa tayari, tutauwasilisha hapa Bungeni ili Wabunge waweze kuujadili na, ninatumai, kuupitisha. Hata hivyo, Bw. Naibu Spika wa Muda, nimezungumza na Prof. Anyang'-Nyong'o humu ndani kwa muda wa dakika chache na tumekubaliana ya kwamba lengo lake na lengo la Serikali au Wizara, kusema kweli, ni sawa. Hamna ugomvi na tunatafuta kitu kimoja. Kwa sababu hiyo, baada ya kupitisha Hoja hii, kwa sababu naamini ya kwamba Bunge litaipitisha, tutatafuta wakati na kuketi na Prof. Anyang'-Nyong'o, pamoja na wadau wengine ili, tusome kwa pamoja Miswada yote; ule wa kwake na ule wa Wizara, ili tuafikiane juu ya Mswada ambao hatimaye tutaleta hapa Bungeni. Kwa hivyo, nadhani, tuko pamoja kabisa; hamna tofauti. Huu ndio ushirikiano, nadhani ambao utasaidia nchi yetu kupiga hatua badala ya kuja hapa kulumbana na kupigana bure tu. Wakati mwingine malengo hata ya Upinzani na Serikali yanakuwa ni sawa, lakini tunapokuja hapa ni kama tunakuja na imani ya kwamba ni malumbano tu ambayo yanaweza kuendeleza malengo yetu ya kisiasa. Nadhani kuna zaidi ya malengo ya kisiasa. Lazima wakati mwingine tulenge kuendeleza nchi kuliko kujiendeleza. Bw. Naibu Spika wa Muda, Hoja hii kama nilivyosema ni ngumu kupinga. Hata katika nchi zingine, sheria kama hizi zimepitishwa. Waingereza wanayo, ijapokuwa hawana sifa ya kutoa habari ambazo ni kinyume na masilahi yao kwa uhuru kama ule ambao wangetaka tuamini wanatoa nao. Nchi ya Australia ina sheria kama hii. Nchi za India, Afrika Kusini na Mexico pia zina sheria kama hii. Kwa hivyo, kupitisha Hoja hii, kusema kweli, ni kwenda na wakati. Haipingiki! Ninaamini ya kwamba Hoja hii itatilia nguvu mambo yanayohusu maisha yetu ya sasa na pia itasaidia kutuondolea matatizo mengine ya kihistoria. Wakati huu kuna mjadala ambao unaendelea katika vyombo vya habari kuhusu kesi ambayo imewasilishwa katika mahakama ya Uingereza. Mashujaa wa vita vya Mau Mau wameishtaki Serikali ya Uingereza juu ya mateso waliyoyapata wakati wa harakati za kupigania Uhuru wetu. Ninamini ya kwamba wakati tulipopata Uhuru, tungefunuliwa siri zote kuhusu utawala wa ukoloni hapa nchini. Tungetaka kujua, kwa mfano, kwa nini Waingereza wakaja hapa? Walichuma nini walipokuwa hapa? Waliendeleza vita vyao dhidi ya watu wetu kwa namna gani? Walitumia mbinu gani? Waliwaua watu wangapi? Waliwatesa watu wetu kwa namna gani? Ni aibu kubwa kwamba habari kuhusu vita vya Mau Mau bado ni ndoto kwetu. Ni mapenzi yangu kwamba hatutapitisha tu Hoja hii, lakini tutaitumia kuwafunulia watu wetu siri kuhusu vita dhidi ya Mau Mau na unyama wa utawala wa ukoloni. Hatimaye, tutatumia Uhuru huu kudai fidia October 18, 2006 PARLIAMENTARY DEBATES 3003 dhidi ya hasara tuliyopata kutoka kwa Waingereza. Isiwe ni mashujaa wa vita vya Mau Mau ambao wanadai fidia pekee, bali iwe ni nchi yote kwa jumla. Hii ni kwa sababu ni nchi yote iliyoteswa na kuathiriwa na ukoloni. Tunataka haki hii itekelezwe wakati huu. Kwa hivyo, Hoja hii itasaidia sisi kama taifa la Kenya. Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa bahati mbaya, Bw. Raila ameondoka hapa Bungeni. Ningependa awe hapa ndio ajue hakuna wakati mimi nimesimama pahali pengine, isipokuwa pale palipo na haki. Wengine wetu, kama alivyosema Bw. Raila, tuliteswa sana tukipigania uhuru wa pili. Tungetaka kujua waliotutesa kwa sababu walipokuwa wanatutesa, walikuwa wanatumia majina ya bandia. Kama mtu alijulikana kama Bw. Kamau, alikuwa akijiita Bw. Omondi. Tungetaka kujua kama kweli ni Bw. Omondi aliyetutesa au ni Bw. Kamau. Tulipata mateso mengi katika Jumba la Nyayo. Taarifa kuhusu mateso hayo imehifadhiwa katika kumbukumbu za Serikali. Huu ndio wakati wa kutueleza ukweli wa mambo. Tusipotoa ukweli huu, wengi wa wale waliokuwa \"mashetani\" enzi hizo, watajigeuza kuwa malaika. Hii si haki. Ukweli ndio utakaotuokoa. Hatuwezi kuupata ukweli ikiwa hatutatumia nguvu za sheria ya uhuru wa habari. Bw. Naibu Spika wa Muda, hatutaki watawala wa mabavu wavalie makoti ya kidemokrasia na hata kutaka kushauri viongozi wa vyama juu ya namna wanavyofikiria nchi hii inaweza kutawaliwa bora zaidi. Ikiwa tungekuwa na sheria hii, ingetusaidia kufunua unyama wa watu hawa. Majuzi, tulimuona Prof. Anyang'-Nyong'o akienda kupata ushauri kutoka kwa mmoja wa wale unaoweza kuwaita mafundi wakuu wa utawala wa mabavu. Mtu yeyote hawezi kwenda kwa Bw. Njonjo kuomba ushauri wowote kuhusu utawala wa kidemokrasia. Alitutesa sana na wewe unajua hivyo. Alisimamia mfumo wa kidikteta katika nchi. Hawezi kuwa na mema ya kutushauri, lakini sasa, kwa vile hatuna sheria hii, hawa watu, bado wanaonekana wasafi. Wengine wetu tutakwenda kwa Njonjo. Wengine watakwenda kwa Moi. Wengine watakwenda kwa yule mwingine, na haya mabadiliko yote ambayo tumekuwa tunatafuta yatakuwa yamekuwa kitu bure."
}