GET /api/v0.1/hansard/entries/238985/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 238985,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/238985/?format=api",
    "text_counter": 145,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Khamisi",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 246,
        "legal_name": "Joseph Matano Khamisi",
        "slug": "joseph-khamisi"
    },
    "content": "Bw. Naibu Spika, asante kwa kunipa fursa hii ili nichangie Hoja ya bajeti ya Wizara ya Afya. Kwanza, ningependa kumpongeza Waziri na maofisa wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Wamejitolea kuhakikisha ya kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya katika sehemu mbalimbali nchini. Bw. Naibu Spika, naunga wenzangu mkono kulalamika juu ya kiasi cha pesa ambacho kimetengewa Wizara hii. Katika hekima ya Serikali, ingekuwa bora kama Wizara hii ingetengewa kiwango sawa cha pesa na Wizara ya Elimu. Hii ni kwa sababu maradhi na ujinga ndiyo matatizo mawili makubwa yanayokabili nchi hii. Hii ndio njia ya pekee ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za karibu zaidi na ambazo zinaweza kutimiza matakwa ya akina mama wajawazito na watoto katika sehemu za mashambani. Bw. Naibu Spika, ningependa kulalamika kwamba nyingi za hospitali zetu, hasa hospitali ya Wilaya ya Kilifi, zina ukosefu mkubwa wa vifaa katika maabara, magari ya kuwabebea wagonjwa kwa jina maarufu ambulansi, na vyumba vya kuwahifadhia maiti. Ningependa kuona hospitali hizi zikiwa na vifaa vya kutosha ili zitoe huduma bora za afya kwa watu wetu. Ningependa kuiomba Serikali hii iwaajiri wauguzi wengi ili huduma hii muhimu iwafikie wananchi wote hapa nchini. Waziri alisema hapa kuwa miaka miwili iliyopita wamejaribu kuongeza idadi ya wauguzi katika hospitali zetu. Hata hivyo, tatizo hilo bado linakabili hospitali zetu. Pia alituhakikishia hapa kwamba watawaajiri wauguzi zaidi ya 1,000. Hili ni jambo nzuri. Lakini watu wa Wilaya ya Kilifi hawajawaona hao wauguzi. Ningependa kuihimiza Serikali itilie mkazo jambo hili la kuwaajiri waguuzi na kuwapeleka katika hospitali ya Wilaya ya Kilifi. Bw. Naibu Spika, ningependa Serikali itilie mkazo swala la zahanati na vifaa vingi vya afya ambavyo kwa wakati huu havitoi huduma yoyote kwa sababu ya ukosefu wa wafanyakazi. Kwa mfano, katika Eneo Bunge la Bahari, kuna zahanati ambayo ilijengwa na wadhamini wa Uingereza. Inajulikana kama zahanati ya Msumarini. Zahanati hii ilimalizika mwanzo wa mwaka huu. Lakini kulingana na mipango ya wafadhili hao, walitaka kuipanua zahanati hii. Lakini kwa kuwa zahanati hii haijapewa kibali na Wizara ya Afya, hata baada ya sisi kupeleka maombi mengi, imewabidi wafadhili hao wakwame katika mipango yao. Hawawezi kutoa pesa zaidi za kupanua zahanati hii kwa sababu haijasajiliwa na Serikali. Mr. Naibu Spika, ningemwomba Waziri ahakikishe ya kwamba zahanati na vifaa vingi vya afya vitasajiliwa kwa upesi iwezekanavyo ili viweze kutoa huduma zinazotakikana na wananchi. Bw. Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kutilia maanani vita dhidi ya ugonjwa wa malaria. Ugonjwa huu ni tatizo kubwa katika Wilaya ya Kilifi. Ni masikitiko makubwa ya kwamba watu fulani katika eneo langu walirejeshea Serikali neti za mbu zaidi ya 3,000 kwa sababu ya hisia za kitamaduni. Walikuwa wanasema kwamba wakilala ndani ya neti hizo, walikuwa wanaona mazingaombwe yakiwajia usiku na kuwatisha."
}