HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 242902,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/242902/?format=api",
"text_counter": 290,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Wario",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 252,
"legal_name": "Ali Wario",
"slug": "ali-wario"
},
"content": "Asante, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipa fursa hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia fursa hii ili nichangie sera hii iliyo mbele yetu. Nampongeza Waziri ambaye aliamua kuleta mwanga katika mashirika yasio ya Serikali. Bw. Naibu Spika wa Muda, baada ya kumshukuru Waziri, ningependa kusema kuwa nilikuwa katika sekta hii kwa muda mrefu, na ni muhimu kutambua mchango wao katika jamii. Kama alivyozungumza msemaji mmoja aliyezungumza kabla yangu, maudhui au matilaba ya kuwa na mashirika yasio ya Serikali ni kuhakikisha kuwa utandawazi na haki imefanywa katika jamii nyingi za nchi hii. Katika kuunga mkono mashirika yasio ya Serikali, ningependa kusema kuwa mashirika haya yamefika sehemu nyingi ambazo Serikali haijaweza kufika hadi leo. Nikisema 2116 PARLIAMENTARY DEBATES July 13, 2006 hivyo, sio fursa kwa mashirika haya kuuza Kenya kwa nchi za nje. Ikiwa Kenya ni nzuri au mbaya, bado ni nchi yetu. Watu wengi wanaoendesha shughuli za mashirika hayo ni Wakenya na ni muhimu wawe na uzalendo. Lazima wafahamu kuwa hii ni nchi yetu na wale wanaowahudumia ni watu wetu. Kwa hivyo, ni vizuri waendeshe mashirika hayo kwa kiwango fulani. Nikisema hivyo, simaanishi wasifanye kazi yao kwa uhuru. Kila mwaka kuna mzozo baina ya Transparency International na Serikali kwa sababu mienendo yao haifurahishi watu wengi katika Serikali. Kwa hivyo, ni vizuri Serikali iwape fursa watekeleze wajibu wao. Bw. Naibu Spika wa Muda, watu wengi walio katika Serikali leo wamesaidiwa na mashirika yasio ya Serikali ili kufika mahali walipo sasa. Kama sio mashirika yasio ya Serikali, sehemu kame za Kenya leo zingetaka kujitenga kutoka kwa Serikali hii. Kwa hivyo, ni muhimu Serikali itambue kuwa mashirika hayo, yana majukumu muhimu yanayotekeleza katika jamii. Swali la utandawazi linahusisha Serikali na umma. Ikiwa mashirika yasio ya Serikali yatasimama kuiambia Serikali iwe na utandawazi, basi ni muhimu wao pia wafanye utandawazi ndipo tuweze kutekeleza wajibu wetu sote tukiwa katika Serikali au umma. Uwezo wa baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali ni mdogo. Ninahimiza sera mpya itakayoletwa na Waziri iangazie jambo hilo. Ingefaa kuweko kwa ofisi ya baraza hilo katika kila wilaya au mkoa ili iweze kuangalia jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yanavyotekeleza shughuli zao. Kama walivyosema Wabunge wenzangu, shughuli zinazotekelezwa na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali zinafaa kuchunguzwa. Bw. Naibu Spika wa Muda, katika nchi hii, ni rahisi kusajili chama cha kisiasa kuliko kusajili shirika lisilokuwa la kiserikali. Kwa nini ni vigumu sana kusajili shirika lisilokuwa la kiserikali? Kwa nini tusiwawezeshe Wakenya wanaotaka kusajili mashirika hayo kufanya hivyo kwa urahisi? Ukitaka kusajili shirika kama hilo, unatakiwa kupitia huduma ya jinai nchini, miongoni mwa ofisi zingine. Kwa hivyo, ni bora Sera mpya tunayoitarajia iguzie swala la usajili wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ili watu waweze kusajili mashirika kama hayo kwa urahisi. Kuna mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yanaitwa \"makeshift NGO\" kwa lugha ya kimombo. Hayo ni mashirika ambayo husajiliwa na watu fulani na kuyatumia kuwawezesha kupata pesa kutoka kwa hazina maalum. Wakishapata pesa kutoka kwa hazina kama hiyo, watu hao hutorokea nje kwenda kufanya shughuli zao. Kwa hivyo, tunataka sera mpya tunayoitarajia iongeze uwezo kwa ofisi husika ili iweze kuwachunguza watu kama hao. Bw. Naibu Spika wa Muda, usimamizi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali humu nchini imekuwa fursa ya kuidhulumu jamii ya Kiislamu. Mengi ya mashirika yaliyokuwa yakizihudumia jamii za Kiislamu humu nchini yamefungwa. Yale mashirika ambayo hayajafungwa, yanatishwa. Wakurugenzi wa mashirika hayo wamefukuzwa kutoka humu nchini. Kwa mfano, hivi majuzi, wakurugenzi wa shirika la Africa Muslims Agency (AMA), ambalo linahudumu katika zaidi ya nchi 57 duniani, walifukuzwa kutoka humu nchini. Pia, wakurugenzi wa mashirika ya Al-haramein na Almuntada-al-Islami walifukuzwa kutoka humu nchini. Licha ya kwamba mashirika haya yana majina ya Kiarabu, mengi yao yanawahudumia watoto wa nchi hii. Kwa mfano, shirika la AMA lilikuwa likisimamia zaidi ya shule 20 humu nchini. Nyingi ya shule hizo zilikuwa zikiwahudumia watoto mayatima. Wakurugenzi wa shirika hilo walipofurushwa kutoka humu nchini, watoto hao wakawa machokora. Kwa hivyo, inafaa dhuluma dhidi ya jamii ya Kiislamu ikomeshwe. Serikali hii inaendesha sera hiyo zaidi. Bw. Naibu Spika wa Muda, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanastahili kuwa na mbinu za kuwawezesha wananchi wasimamie shughuli zao. Inafaa mashirika hayo yatekeleze wajibu wao halafu yawawezeshe wananchi kuchukua nafasi yao. Haifai mashirika hayo kuendesha shughuli zao kwa njia ambayo itawafanya wananchi kuwa waombaji milele. Ninachozungumzia hapa kinajulikana, kwa lugha ya kimombo, kama \"exit strategy\". July 13, 2006 PARLIAMENTARY DEBATES 2117 Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanastahili kutekeleza miradi ambayo itaachiwa wananchi kujisimamia pindi mashirika hayo yatakapoondoka kutoka sehemu hizo. Kwa mfano, hatutaki shirika la DFID liende kuhudumu katika sehemu ya uwakilishi Bungeni Bura, milele. Tunataka shirika hilo liende huko likatusaidie kwa muda, halafu liondoke liwaachie watoto wetu jukumu la kusimamia miradi ambayo litakuwa limeanzisha. Bw. Naibu Spika wa Muda, baadhi ya Wabunge wenzangu wamezungumzia juu ya pesa nyingi zinazotumiwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Pesa za mashirika hayo hupatikana kwa njia ya kipekee. Kwa hivyo, inafaa mashirika hayo yapewe nafasi ya kutekeleza wajibu wao. Ikibidi, mashirika hayo yachunguzwe, kwa njia ya haki, lakini yasinyanyaswe na kudhulumiwa Kwa hayo machache, ninaiunga mkono Hoja hii."
}