GET /api/v0.1/hansard/entries/244535/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 244535,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/244535/?format=api",
    "text_counter": 106,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Capt. Nakitare",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 348,
        "legal_name": "Davis Wafula Nakitare",
        "slug": "davis-nakitare"
    },
    "content": "Asante, Bw. Naibu Spika wa Muda, kwa kunipa nafasi hii ili nami niunge mkono Hoja hii. Kulingana na vile eneo la pwani lilivyo, mkorosho ni mmea ambao hukuzwa katika eneo lipatalo kilomita 480 mraba. Eneo lote la pwani lina rutuba inayowezesha kukua vizuri kwa huu mmea. Korosho ni zao ambalo lina manufaa mengi sana. Huu ni wakati ufaao kwetu sisi kutunga sheria ya kulilinda zao hili. Kuna kanju ambazo zinapatikana kutoka kwa mkanju. Makanju ni matunda na vile vile ni dawa ya homa. Korosho na kanju hutokana na mti uitwao mkanju. Zao hili linaweza kulinganishwa na cacao ambalo ni zao linalokuzwa huku Afrika Magharibi. Wizara ya Kilimo haijawa na mwongozo mzuri juu ya zao hili la korosho. Watu wa pwani wameumizwa kiasi cha kuishi kama mayatima kwa sababu hakuna mwongozo wa kilimo unaofaa kuhusu ukuzaji wa korosho. Ukiangalia upande wa soko, kuna wale wanaovuna korosho nao huwauzia wale walio na pesa. Wao hulipeleka zao hili nje ya nchi hii ili likapate kutiwa thamani kidogo na baadaye hurudishwa humu nchini kuuzwa kwa bei ghali mno. Watalii wanapokuja hapa kwetu, wao hupendelea kula korosho namna wanavyopenda kula njugu karanga. Ikiwa tutakuwa na sheria ambayo itaweza kumlinda mkulima aliye Lunga Lunga, Vanga, Miritini, Ribe na hata Sultan Hamud, tutaweza kukuza mikorosho kwa wingi. Sehemu hizi zote zina uwezo wa kukuza mikorosho na kudumisha kile kiwanda cha korosho kilichoko wilayani Kilifi. Miti aina ya mikandaa ama mikoko hukuzwa kule pwani, lakini kwa vile hakuna sheria inayolinda ukuzaji wa hii miti, wageni ndio wanaopata faida kutokana nayo. Kwa hivyo, wakati umefika sasa wa kila idara katika Serikali kuulinda uchumi wetu kwa kuzingatia sheria zilizoko. 1816 PARLIAMENTARY DEBATES July 5, 2006 Ninaamini kwamba sheria kabambe itakayosaidia ukuzaji wa korosho itatokana na hii Hoja ambayo imeletwa na mhe. Khamisi. Ikiwa tutapitisha Mswada juu ya uzalishaji wa korosho, tutaweza vile vile kuvifaidi vyama vya ushirika. Bw. Naibu Spika wa Muda, nikiangalia maisha ya watu wa pwani, siwezi kusema kuwa ni hao watu wa kukaa chini ya mnazi kungoja nazi zianguke ndipo wapate chakula. Watu wa pwani ni watu wenye nguvu. Iwapo watapewa mwongozo, wataweza kukuza uchumi ambao unaridhisha. Kuna wakati ambapo uchumi wa pwani ulikuwa unategemea miwa. Wakati kiwanda cha sukari cha Ramisi kilipoanguka, watu wa pwani hawakuwa na uchumi tena. Watu wa pwani na wa bara walikuwa wanategemea mkonge. Ukienda Kilifi au Vanga, utamkuta Mjaluo ambaye alikwenda kukata mkonge. Amekuwa mwenyeji ambaye anaweza kuangazia mambo ya kipwani na maisha yake ni ya kipwani. Kwa hivyo, ikiwa tutakuwa na mwongozo huu, wakulima wataweza kupata nafasi ya kuwaelimisha watoto wao kwa sababu watakuwa na vyama vya ushirika. Pia, korosho italindwa na sheria, na tutaweza kuiuza katika nchi za nje ikiwa imetengenezwa badala ya kuipeleka nchi za nje kabla haijatengezwa, halafu irudishwe na tuuziwe itakapotengezwa. Tunaona vibaya kwa sababu ukipeleka maziwa kwenye kiwanda unalipwa pesa kidogo. Baadaye unauziwa maziwa hayo kwa bei ya juu kuliko ile uliyouza. Bw. Naibu Spika wa Muda, kama nilivyosema hapo awali, mti wa mkorosho una faida nyingi. Kwa hivyo, tukizingatia mambo haya na vile uchumi wetu unavyoangaziwa, inatakikana uchumi huu pia uwafaidi watu ambao hawajiwezi kwa sababu wao ndio wengi. Kuna matajiri wachache, lakini maskini ni wengi. Maskini hawa ndio hutumia jasho lao kulima, kukuza na kuuza bidhaa zao. Matajiri hununua bidhaa hizo kwa bei nafuu kabla ya kuziuza katika nchi za nje. Bw. Naibu Spika wa Muda, naliomba Bunge hili litunge sheria ambazo zinalinda masilahi ya Wakenya. Tuwahimize watu wetu wanunue bidhaa za Kenya ili tujenge Kenya kuliko kutegemea bidhaa zinazotengezewa nje ili tufurahie matunda ya nguvu na jasho letu ili watoto wetu na vizazi vijavyo wawe wakitembea nje na kusema:- \"Hizi ni bidhaa zetu za Kenya\". Ni aibu kwetu iwapo tutategemea vitu vinavyotengezewa nje ilhali sisi pia tuna uwezo wa kutengeneza vitu hivyo. Bw. Naibu Spika wa Muda, ninaiunga mkono Hoja hii na ningependa kuwaomba waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao hawajawahi kuonja korosho waende wakazionje makanju ili wapate kujua utamu wake. Ni hakika watafurahia na wataona umuhimu wa kuwa na sheria za kuulinda mkorosho. Naomba kuunga mkono."
}