GET /api/v0.1/hansard/entries/255677/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 255677,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/255677/?format=api",
    "text_counter": 342,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Mr. Wario",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 252,
        "legal_name": "Ali Wario",
        "slug": "ali-wario"
    },
    "content": "Ahsante, Bw. Naibu Spika. Ninachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuweka hai na kutujalia fursa ya kujadiliana juu ya Hotuba ya Rais, ambayo ninaamini inakejeli na kuchezea shere werevu wa Wakenya. Bw. Naibu Spika, nimesema mara nyingi kwamba mtu hupewa cheo na Mwenyezi Mungu na kunyang'anywa cheo hicho na Mwenyezi Mungu. Watu wengi husahau kwamba cheo ni amana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wao hutumia vyeo vyao kuwadhulumu wanyonge. Ninasema hivyo kwa sababu ya ule uvamizi uliotekelezwa na maofisa wa usalama katika maeneo ya makazi ya Kipkurere katika Wilaya ya Uasin Gishu. Katika kisa hicho, maofisa wa usalama waliovalia sare zao rasmi, na kujihami kwa bunduki, walionekana katika televisheni wakiteketeza nyumba walimokuwa wakiishi wanawake na watoto. Maofisa hao waliharibu mali na mimea ya vyakula ya maskini. Sina budi kumuomba Mwenyezi Mungu awachukulie hatua wale wanaowadhulumu wanyonge. Bw. Naibu Spika, sina unyonge wa kuficha ukweli. Ninasema kwamba Serikali hii imefanya kazi na pia kuharibu mambo mengi katika muda ambao imekuwa mamlakani. Ninataka kuzungumza kama mtu mzima. Sitaki kuichambua Hotuba ya Rais. Pengine nikiichambua, mambo kadhaa yataharibika. Lakini, nitasema kwamba mambo kadhaa yalifanywa na mambo kadhaa yameharibika. Katika Hotuba yake, Rais amegusia juu ya Bunge kukosa kutekeleza wajibu wake. Alisema kwamba kati ya Miswada 25 iliyoletwa Bungeni katika Kipindi kilichopita, Miswada saba peke yake ilipitishwa na kuwa sheria. Ninamlaumu Rais kwa hali hiyo. Katika Kipindi hicho, tulipitisha Miswada kadhaa lakini Rais alikataa kuweka sahihi ili iwe sheria na badala yake kuirudisha Bungeni kwa sababu moja au nyingine. Wanaofaa kulaumiwa zaidi ni baadhi ya Mawaziri wake, ambao hawajui kushirikiana na Wabunge wenzao. Wengi wao hawatutambui kama wawakilishi wa watu katika Bunge hili. Wanaona kuwa sisi tunafaa kudhalilishwa tu. Kwa sababu ya huo mvutano, Bunge halikuweza kupitisha Miswada mingi katika Kipindi kilichopita. Kwa hivyo, ni lazima Wabunge washirikiane ili tuweze kutekeleza wajibu wetu. Hivi juzi wakati wa kuunda Kamati ya shughuli za Bunge, upande wa Serikali ulikwamilia nafasi mbili ambazo zilistahili kuchukuliwa na Upinzani. Serikali ingekubali kuupatia Upinzani March 28, 2006 PARLIAMENTARY DEBATES 133 nafasi hizo mbili na shughuli za Kamati hiyo ziendelee kama kawaida. Sasa tunasubiri kuona mambo yatakavyokuwa. Hakuna hata Mswada mmoja utakaopitishwa na Bunge hili katika Kipindi hiki. Upande wa Serikali una tabia ya kuonyesha uwezo ulionao katika Bunge hili. Nguvu hazipitishi sheria! Bw. Naibu Spika, katika Hotuba yake, Rais alisema kwamba uchumi wa nchi hii umekua kwa asilimia tano katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Kwani, wale wanaotunga sera za nchi hii hawaendi madukani kununua unga, sukari au chumvi? Bei za bidhaa hizi hupanda siku baada ya nyingine. Hali halisi ya kiuchumi nchini na utafiti wa Serikali haviambatani. Wale wanaotuambia kwamba uchumi wa Kenya umekua yafaa watuambie hali ya bei za unga, sukari na chumvi hapa nchini. Kadhalika, katika Hotuba yake, Rais alisema kwamba anajivunia uongozi bora, na haswa uongozi katika sekta ya fedha, ambao alisema umeboresha uchumi wa nchi hii. Sina shaka juu ya swala hilo. Lakini, Gavana wa Benki Kuu ya Kenya, Bw. Mullei, amekosea nini? Mbona kuna mzozo juu ya uongozi wa Benki Kuu ya Kenya? Ukimfungulia mashtaka Gavana wa Benki kuu, inamaanisha kwamba uongozi katika benki hiyo, na katika taasisi zote za Serikali zinazoshughulikia maswala ya kifedha, hauko sawa. Mbona kuna shaka namna hii? Bw. Naibu Spika, Wakenya milioni saba wanalala hoi. Hawana mwelekeo. Wengi wamekufa. Serikali ni nyepesi ya kukana vifo vya watu. Watu wamekufa kwa njaa na kiu. Katika Hotuba yake, Rais alisema kwamba Serikali yake imepeleka malori 20 peke yake kusaidia katika ugawaji wa maji ya kunywa katika sehemu zilizoathiriwa na ukame. Hali ilivyo katika sehemu hizo inahitaji juhudi zaidi kutoka kwa Serikali. Wilaya nyingi katika sehemu kame zimeathirika. Malori yote ya wanajeshi wa Kenya yana kazi gani? Serikali inatangaza janga la kitaifa la ukame na inatuma malori 20 ya maji. Tunaelekea wapi? Ni wilaya ngapi ambazo zimeathiriwa na matatizo ya ukame? Ukipeleka malori 20 ya maji, tutafanyaje kule Bura na hatuna maji? Bw. Naibu Spika, sisi tunakata sera na sheria. Mara nyingi tunazungumza juu ya maswala ya kijinsia ama \"affirmative action\", lakini kwa maswala ya ukame hakuna maswali ya dharura. Mbona pesa maalum zisitengwe? Miezi mitano iliyopita, Rais alitangaza janga la ukame na baada ya miezi mitano inayokuja, atatangaza janga lingine. Kwa nini tusiwe na sera ya ukame? Tunajua ni wilaya ngapi ambazo zimeathiriwa na ukame na ni sehemu ngapi ambapo tuna tisho la kukabiliwa na ukosefu wa chakula. Kwa nini tusiwe na sera maalum? Kwa nini Serikali inatangaza janga kila siku? Hiyo ni kazi ya wazima moto na kazi yao kamwe, haijengi nchi. Ninafurahi kwa sababu Rais, katika Hotuba yake, alisema kuwa anatambua kwamba asilimia 72 ya Wakenya ni vijana. Hata hivyo, amechelewa! Angejua jambo hili mapema ili alete sera na sheria ambazo zingeboresha hali ya vijana wetu. Sisi leo tunafahamu kuwa hii ni kampeni. Mwaka wa 2007 uko karibu sana. Rais amekumbuka kuwa asilimia 72 ya Wakenya ni vijana kisha akakumbuka kuwa hawana kazi. Ni vizuri amekumbuka lakini huu ni wakati mbaya kwa sababu vijana wanajua anawachezea shere. Bw. Naibu Spika wa Muda, ninatumaini sote tunakubaliana kuwa Katiba ni kitu muhimu. Fisi akiwa na njaa huita wenzake ili wawinde pamoja na akishinda, yeye hupigana na wenzake ili asiwagawie kipande cha nyama walewaliowinda pamoja. Wenzetu hawasomi! Nimetoa mfano wa fisi na sikuita mtu ye yote fisi. Juzi, kulikuwa na maswala ya Katiba na tukakaa hapa mpaka saa sita usiku ili tushirikiane. Kilio chetu kilianguka kwa masikio ya watu ambao hawasikii. Kwa sababu wako na idadi kubwa ya Wabunge katika Bunge hili, kamwe hawatambui watu. Basi, tukaenda kwa mahakama ya wananchi na wananchi wakahukumu. Leo, badala ya kuleta washikadau wote ili tuulizane ni wapi tumekosea na ni wapi tutakosoa, tumeambiwa kuwa Serikali imetengeneza Kamati ya watu mashuhuri ili kushughulikia maswala ya Katiba. Mtu mashuhuri zaidi ni Mkenya na yuko kule nje ambako anatungojea. Hii Kamati ya watu mashuhuri inangojewa na watu mashuhuri kule vijijini. 134 PARLIAMENTARY DEBATES March 28, 2006 Bw. Naibu Spika, nikimalizia, Rais amesahau maswala ya ufugaji. Mpaka tutakapoboresha biashara ya mifugo katika nchi hii, maswala ya ukame hayatashughulikiwa. Rais amekumbuka na amegusia sekta zote na vile zinavyofanya kazi, lakini kwa bahati mbaya, amesahau ufugaji. Miaka michache iliyopita, maswala ya sehemu kame na ufugaji yaliwekwa mbele. Baada ya miaka mitatu, hakuna kitu ambacho kimefanywa kuhusu ufugaji na Rais, katika Hotuba yake na mpango wa Serikali; amesahau ufugaji. Ningetaka kumwambia asisahau ufugaji kwa sababu unachangia asilimia 10 ya Gross Domestic Product ya nchi hii. Mwenzangu amesema kuwa Serikali inajali maslahi ya akina mama kwa sababu kuna wawili katika Baraza la Mawaziri. Ningetaka kumwambia kuwa ni sikitiko kubwa kusikia haya kutoka kwake. Yeye ni mwanamke na angekuwa wa kwanza kutetea haki za wanawake. Wanawake wawili hawatoshi! Wanawake wanafaa kuongezwa katika Baraza la Mawaziri. Kwa hayo machache, ninashukuru."
}