GET /api/v0.1/hansard/entries/365177/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 365177,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/365177/?format=api",
"text_counter": 157,
"type": "other",
"speaker_name": "",
"speaker_title": "",
"speaker": null,
"content": "Pia, tumekuwa na sera ya kitaifa kuhusu vijana ama ukipenda kwa kimombo “the National Youth Policy”. Lakini hii sera, ambayo pia mimi nilikuwa mmoja wa waliohusika kuitengeneza, hatujaona ikitekelezwa na Serikali. Kwa hivyo, baraza hili lina jukumu la kueneza na kutangaza yale mapendekezo, maafikio ama ile ndoto ambayo iko katika hii sera ili tuweze kuinua kiwango cha uchumi na uwakilishaji wa vijana katika mambo ya kitaifa. Kwa hivyo, ni jambo muhimu sana kuhakikisha kwamba hili barasa limetengewa hela ndio liweze kufanya kazi yake. Baraza la Vijana la Kitaifa pia limepatiwa jukumu la kutafuta rasilimali na fedha ili kuipatia nguvu miradi ya vijana. Hii ni kusema kwamba hili baraza linaweza kufadhili mikakati ama miradi ya vijana hata katika maeneo Bunge ambapo Wabunge wetu wanatoka. Kwa hivyo, ni jambo la muhimu tuwe na baraza hili ili liweze kuangalia ni njia zipi tutatumia kuhakikisha kwamba miradi ya vijana haibaki nyuma ili tuweze kuondoa umaskini kati ya vijana na kufatufa ajira. Vijana wetu wana taranta na wanaweza kusoma. Wanafaa kupatiwa nafasi ya kuonyesha ni nini ambacho wanaweza kufanya ili kuchangia kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Hili baraza pia limepatiwa nafasi ya kupigia upato sheria zile ambazo zitakuwa zikizungumzia maswala ya vijana. Wengi wetu tumepigiwa simu na vijana wetu wakituuliza, kwa mfano, ni vipengele vipi vinavyomfanya kijana akose ajira kwa sababu hana uzoevu wa kufanya ile kazi. Hiki ni kikwazo kikubwa kwa vijana wengi ambao wanatafuta kazi ilhali ukiangalia kazi nyingi hakuna mtu yuko na ule uzoefu isipokuwa apatiwe nafasi ili apate ule uzoevu. Kwa hivyo, hili baraza linahitaji kuwepo na nafasi ya kutazama ni vipi, kwa mfano, vijana watapata nafasi kupitia sheria ambazo sisi kama Wabunge na Bunge zijazo tutapitisha. Hili Baraza la Vijana la Kitaifa pia limepatiwa nguvu za kutafuta nafasi ya vijana kupata rasilimali ili waweze kupata huduma za kijamii. Ukiangalia huduma za kijamii na ufukara utapata kuwa vijana ndio maskini zaidi kwa sababu hawajapata riziki yao ya kila siku. Asilimia sabini ya vijana katika nchi hii hawana ajira yoyote. Huduma za kijamii hata mikopo inahitaji uwe na mali ama una pesa kidogo za kulipia zile ada ambazo zinatozwa. Kwa hivyo, ni lazima hili Baraza liwepo ili liweze kuwa na mikakati ya kuhakikisha kwamba vijana hawatupiliwi mbali wakijaribu kujisatiti kuchangia katika mambo ya kitaifa. Jambo lingine ambalo ni la muhimu mno ni kuwa tumetoka tu katika uchaguzi ambapo kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa kikabila. Kumekuwa na tetezi kwamba vijana ndio wametumiwa kufanya ghasia na kuweka bughudha katika nchi. Lakini sheria hii inatoa uwezo kwa hili baraza kuhakikisha kwamba vijana wamehusishwa kuleta utengamano na umoja na hata kuhakikisha kwamba wanashiriki katika huduma za jamii au community development . Hii sheria inanuia kuhakikisha kwamba zile nguvu za vijana sizitumiwe vibaya. Ukiangalia pale chini, inasema kwamba hili baraza litoe mikakati ama muongozo wa kuhakikisha kwamba vijana hawatumiwi na watu ambao wanajitakia mambo yao. Utakuta kwamba wale ambao wananawiri katika biashara, kwa mfano, za mihadarati, wanatumia hawa vijana kujitajirisha. Kwa hivyo, hili baraza lina umuhimu na wakati wake umefika. Huu ndio wakati mwafaka wa kuhakikisha kwamba hili baraza limepatiwa zile fedha linalohitaji. Ukiangalia, tumekuwa tukitengeza sheria ambazo zinatengeza mabaraza tofauti tofauti itakuwaje hili baraza ndilo litakuwa tofauti?"
}