GET /api/v0.1/hansard/entries/46588/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 46588,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/46588/?format=api",
    "text_counter": 331,
    "type": "other",
    "speaker_name": "",
    "speaker_title": "",
    "speaker": null,
    "content": "Ifahamike kuwa Hoja hii inaenda sambaba na inaunga mkono kipengee 57(d) cha Katiba. Kipengee hicho kinaeleza kinaga ubaga kwamba ni jukumu la familia na Serikali kuhakikisha kuwa inatazama na kushughulikia vilivyo maslahi ya wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60 wanaoishi kati yetu. Kwa hivyo, hata tunapojadili suala hili na kuzingatia mbinu jinsi tutashughulikia maslahi ya wazee, tujue kwamba ni suala la kikatiba na ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba haki hiyo iliyomo ndani ya Katiba inatimizwa kwa niaba ya wananchi hawa. Bw. Naibu wa Spika, ni vema na bora Bunge hili lijue kuwa kwa sababu ya janga la Ukimwi wazee wengi katika jamii yetu leo hii wamegeuka kuwa wazazi na wanashughulikia maslahi ya mayatima wengi. Kuna familia nyingi sana kote nchini ambako wazee wa umri huu ndio wanawakuza mayatima ambao ni wajukuu wao. Ikiwa Serikali itachukuwa hatua hii na kuhakikisha kwamba inaangalia maslahi ya wazee hawa, vile vile msaada huo utawafikia watoto wengi sana ambao wanashughulikiwa na wazee hawa kama wazazi. Hali ya maisha hapa nchini imedorora sana. Jinsi tunavyofahamu wiki iliyopita Bunge hili lilizungumzia suala la gharama ya maisha. Ni suala nyeti na ambalo Serikali haina budi kulishughulikia. Mzigo huu wa gharama ya maisha ni mzito zaidi kwa wananchi wenye umri huu mkubwa. Hawa ni wananchi ambao hawajawahi kupata nafasi ya kuhudumu katika nyadhifa zozote ili kuweza kupata mapato na malipo ya uzeeni. Wanapoendelea kuzeeka, ndivyo uwezo wao wa kujimudu maishani unavyoendelea kupunguka. Kwa hivyo ni muhimu Bunge hili lisisitize hatua hii. Baada ya Hoja hii kupitishwa ni muhimu Serikali ihakikishe kwamba mpango huu unatekelezwa bila kuchelewa. Ningependa kuihimiza Serikali hata tunapojadili Hoja hii kwamba hoja kama hizi zinapopitishwa ni bora Serikali ichukuwe hatua mufti kuhakikisha kwamba mipangilio kama hii inatekelezwa. Mwezi ujao, Bunge hili litajadili Bajeti ya mwaka huu yaani makadirio ya pesa ya 2011/2012. Ningependa kumhimiza Waziri wa Fedha kwamba anapokamilisha Bajeti yake, kwa sababu Hoja hii ninayo imani tutaipitisha asubuhi ya leo, aweke mpangilio huu katika Bajeti ili wananchi hawa waweze kuona matunda ya Hoja hii pindi tu Bajeti ya mwaka huu itakaposomwa na kupitishwa na Bunge hili. Bw. Naibu Spika, mwisho, naona kuwa imependekezwa hapa kuwa wazee watakaonufaika na mpango huu ni wazee ambao hawapati malipo ya uzeeni. Lakini ni bora Bunge hili pia lifahamu kuwa hata wale wanaopata malipo haya ya uzeeni, wanashida nyingi sana. Hii ni kwa sababu malipo wanayoyapata ni duni sana. Hivi karibuni nimekuwa na mazungumzo na walimu waliostaafu kabla ya 1970. Wao hupata malipo ya uzeeni takriban kati ya Kshs2,000 na Kshs3,000 kwa mwezi. Ni vigumu sana kwa mzee kama huyo ambaye anagharamia familia yake kuweza kujimudu. Kwa hivyo, ni muhimu pia Serikali ibuni mbinu maalum za kuweza kushughulikia wazee hawa hata kama wanapata marupurupu ya uzeeni. Hebu tuwafikirieni ili wafaidike kama wazee wengine. Bw. Naibu Spika, Hoja hii ni muhimu. Ninalihimiza Bunge hili kuipitisha ili Serikali yetu iweze kuitekeleza kwa haraka iwezekanavyo. Kwa hayo machache, ninaunga mkono"
}