GET /api/v0.1/hansard/entries/487825/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 487825,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/487825/?format=api",
"text_counter": 595,
"type": "speech",
"speaker_name": "Hon. Chea",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 1694,
"legal_name": "Mwinga Gunga Chea",
"slug": "mwinga-gunga-chea"
},
"content": "Bi. Naibu Spika wa Muda, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia suala la vitambulisho. Kwanza kabisa, ningependa kuchukua fursa hii kusema kwamba ninaunga mkono suala hili. Pili, ningependa kupeana shukrani kwa mhe. Diriye Mohamed, ambaye ameileta Hoja hii Bungeni. Ukweli ni kwamba suala la vitambulisho ni muhimu. Kama Hoja inavyosema, usipokuwa na kitambulisho, kuna mambo mengi ambayo huwezi kuyafanya. Kwa hivyo, kuna haja ya Serikali kuhakikisha kwamba vitambulisho vimewafikia watu wote kote nchini. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba wasajili wamepelekwa katika sehemu ambako usajili unafaa kufanyika. Kuna baadhi ya maeneo humu nchini ambako mpaka sasa hakuna wasajili. Ni muhimu wasajili wapelekwe huko mara moja ili waweze kuzingatia suala hili na Wakenya wapate vitambulisho. Tunapopeleka wasajili katika sehemu hizo, ni lazima pia tukumbuke kwamba sehemu nyingi humu nchini hazina magari. Mara nyingi tunaona watu wanafuatilia vitambulisho kutoka makao makuu ya wilaya. Kwa hivyo, Serikali inapaswa kujizatiti vilivyo na kuhakisha kwamba imepeana magari na mafuta ya kutosha ili kuwawezesha wasajili kusafiri hadi kwenye kata ndogo ndipo wananchi waweze kupata vitambulisho. Bi. Naibu Spika wa Muda, tukiendelea kuzungumzia suala la vitambulisho, ni lazima tukumbuke kwamba kuna kamati ambazo huteuliwa kuchuja na kuona iwapo watu fulani wanastahili kupewa vitambulisho. Ni maoni yangu kwamba kamati hizo zinafaa kukaguliwa kwa kina. Inafaa wanakamati wenyewe wawe wamechujwa kuhakikisha kwamba wanaweza kuchuja wenzao kwa uadilifu. Katika sehemu ninayowakilisha Bungeni ya Kaloleni kuna wananchi wanaoishi sehemu kama vile Mariakani, ambao mara kwa mara hubaguliwa vitambulisho vinapotolewa. Sababu za wao kubaguliwa si za msingi. Hili ni jambo ambalo hata sisi, tukiwa viongozi, tunashindwa kulielewa. Ni muhimu tukubali kwamba wale wanaofanya kazi ya kuwakagua na kuwachuja wengine pia ni binadamu. Kwa hivyo, wanakuwa na vikao na wasajili, na wana mahitaji kama binadamu wengine. Kuna umuhimu wa kuzingatia maslahi ya watu hao, ndipo wanapokuwa na vikao pia waweze kupata kiinua mgongo. Kitambulisho ni stakabadhi muhimu sana. Tunazungumzia ugatuzi, na sielewi ni kwa nini bado Wakenya waendelee kusafiri mwendo mrefu kufuatilia vitambulisho vyao. Inafaa Serikali iweke mikakati ya kuhakikisha kwamba watu wanafuatwa kusajiliwa mashinani ili kila mtu aweze kupata kitambulisho chake katika shule ya msingi ama katika zahanati. Tukifanya hivyo, tutarahisisha maisha ya Wakenya. Wananchi pia watakuwa wanaona faida ya ugatuzi. Kwa hayo machache, ninaiunga mkono Hoja hii."
}