GET /api/v0.1/hansard/entries/491307/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 491307,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/491307/?format=api",
"text_counter": 180,
"type": "other",
"speaker_name": "",
"speaker_title": "",
"speaker": null,
"content": "Kwa mfano, Kwale kwatoka maji yanayotoka Marere, lakini wenyeji wa Kwale hawanywi maji ya Marere. Lakini wanayaona yale maji yakipita yakienda Mombasa ili watu wa Mombasa wayanywe, kwa sababu watu wa Mombasa ni watu zaidi; wa Kwale sio watu! Hii ni hatari! Watu wa Mombasa wanywe maji na watu wa Kwale wayatizame tu kwa sababu watu wa Mombasa ni watu zaidi; wale watu wa kule Kwale sio watu! Hawa basi wanywe haya maji ndio watu wa Kwale angalau wapate chochote; lakini hakuna wanachopata! Sasa huu ni mtihani bin examination! Maji yanatoka Tiwi yakienda Mombasa, ingekuwa bora angalau kupatikane japo hata sumni – hizi sio pesa nyingi tunazosema sisi – kusudi kaunti nayo iweze kupata chochote. Lakini kaunti bado zaja hapa tukizozania katika mfuko wa Serikali kuu. Ingelikuwa rasilmali hizi zinaweza kupatikana kusudi kaunti zile ambazo rasilmali hizo ziko, wananchi wa pale wafaidike. Hayo ni mambo tuliyoyaona, Bi. Spika wa Muda. Tulikwenda Nakuru karibu na Ziwa la Nakuru. Jambo tuliloona kule ni wenyeji wakilalamika nyani walioko kule. Je, ni faida gani wenyeji wa Kaunti ya Nakuru wanapata? Hakuna! Hata hawandikwi kazi katika shirika la Kenya Wildlife Service (KWS). Je, wanaoandikwa kazi wametoka wapi? Sijui! Haya maneno sikuyasema mimi; waliosema ni wananchi tuliokwenda kuzungumza nao. Sisemi mimi haya maneno. Naibu Mwenyekiti alikuweko, Bi Mwenyekiti alikuweko na Wanakamati wenzangu pia walikuwepo. Kando ya hayo, malalamishi mengine tuliyoyasikia ni kwamba hata zile kazi ndogo ndogo pia watu wa kule hawapati. Hayo ndio maneno wananchi walikuwa wakilalamikia. Sasa, pamoja na kwamba hawa watu twawataka – wawekezaji – ambao ndio wajasiliamali, lakini kuna mambo muhimu ambayo lazima wakija huku wayafahamu. Kuna watu hohe hahe wa kule na lazima wapate kazi. Sasa wewe, kila kitu kinachozungumzwa watafuta watu walio na shahada, basi pia kufagia barabara wataka mtu aliye na shahada? Asalaalaa! Kupika chai kwataka shahada? Kuweka maji moto ndani ya kikombe kwataka shahada?"
}