GET /api/v0.1/hansard/entries/530892/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 530892,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/530892/?format=api",
    "text_counter": 179,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Hon. Kangara",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 12543,
        "legal_name": "Benson Mutura Kangara",
        "slug": "benson-mutura-kangara"
    },
    "content": "Vile vile, nitawaomba kwa heshima na unyenyekevu wakipata nafasi, wanifunze Kiswahili pia nami niweze kukifahamu kama wanavyokifahamu. Lakini ninawatolea tahadhari, wasinifunze kupitia kwa mtandao au kwa kutumia arafa fupi maanake mimi sijaimarika kidijitali. Kiswahili kimetiliwa mkazo sana na ni lazima tukitilie mkazo jinsi Katiba ilivyokitilia mkazo kuliko lugha nyingine zozote. Ukitazama vyuo vikuu vya Amerika, Mexico na Japan na hata nchi zinginezo duniani, wameanza kufunza Kiswahili katika vyuo vyao. Kwa hivyo, ni vyema pia sisi hapa nyumbani tukichukue Kiswahili kuwa lugha muhimu. Mara nyingi Kiswahili kimechukuliwa kama lugha ya watu hohehahe, maskini na wa chini kabisa. Sasa ni lazima tuipatie umuhimu maana ni lugha kama zile nyingine. Lazima tujivunie kama Wakenya. Hii ni lugha yetu. Kama watu wa Afrika mashariki nasi pia lazima tujivunie kwamba ni lugha yetu vile vile. Ningeomba pia katika Bunge ni lazima tuweke mfano mzuri, tupitishe kuwa tunapopiga chapa hizi Hoja na nakala zingine ziwe zinachapishwa kwa lugha ya Kiswahili. Hatuwezi kuziambia idara zingine umuhimu wa Kiswahili ilhali sisi wenyewe hapa Bungeni hatuyafuati hayo maadili. Ninajua mawakili wengi sana wakiwa pale kortini huwa wamebobea katika lugha za kikoloni lakini inapofika wakati wa kuzitafsiri kwa lugha ya Kiswahili huwa wanapata shida. Hapa namuona Mheshimiwa Gladys ambaye pia ni wakili lakini ninajua akiambiwa atafsiri kwa lugha ya Kiswahili atakuwa na changamoto. Kwa hivyo, katika mambo ya sheria ni vigumu zaidi. Ukiangalia mambo ya kesi inavyoripotiwa ama kuchukuliwa pale tunasema statement, mara nyingi inakuwa katika lugha ya Kiingereza. Hapo ndipo pana shida maanake mshatikwa mara nyingi anasomewa na kuambiwa, “hii ndio taarifa uliyosema.” Kwa vile hana ule uelewaji wa lugha inakuwa ni tatizo kwake na hata akienda kortini anakumbwa na changamoto. Hii lugha yetu ni lazima tuijivunie na tuonyeshe umuhimu wake. Mambo ya kubuni sheria na kuziandika ina shida. Katiba inatuambia Kiswahili ni muhimu. Mambo mengi katika majarida yaliyoko yameandikwa kwa Kiingereza na wakati mwingine watu hawawezi kuelewa. Naiunga mkono Hoja hii. Asante."
}