GET /api/v0.1/hansard/entries/532159/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 532159,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/532159/?format=api",
    "text_counter": 215,
    "type": "speech",
    "speaker_name": "Hon. Gichigi",
    "speaker_title": "",
    "speaker": {
        "id": 1909,
        "legal_name": "Samuel Kamunye Gichigi",
        "slug": "samuel-kamunye-gichigi"
    },
    "content": "Nakushukuru, mhe. Spika kwa kunipatina nafasi hii. Namshukuru Rais kwa Hotuba aliyotoa hapa Alhamisi, wiki jana. Kwanza, nina furaha kusema kwamba nimekuwa mashinani leo. Wananchi wamefurahi kwa sababu ya stima iliyowafikia wakati huu ambapo Serikali inalenga shule za msingi. Tunatarajia kwamba, kama vile Rais alivyoahidi, zile shule ambazo hazijafikiwa zitafikiwa kufikia mwisho wa mwaka huu wa kifedha; yaani mwezi wa sita. Mhe. Spika, pia tunaishukuru Serikali kwa kuanza kugharamia malipo ya mitihani katika shule zetu za umma. Kwa niaba ya wananchi, na haswa wakazi wa Kipipiri, tunashukuru kwa hilo. Pia, watu ambao wamefurushwa kutoka sehemu zao na sasa wanaishi na wananchi wengine wanashukuru kwa zile Kshs10 bilioni ambazo zimetengwa kuwasimamia ili waweze kupata mahali pengine pa kuishi. Maisha yao, ambayo yamekuwa ya huzuni kubwa, yatabadilika. Nikija katika Ripoti ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuna msemo wa kisheria ambao unasema, “mshukiwa hana hatia mpaka ithibitishwe kortini kuwa ana hatia”. Kwa hivyo hatupaswi kusema kwamba wale watu ambao wametajwa katika Ripoti hii ya EACC wana makosa. Nadhani Rais aliwaagiza mawaziri wake na wafanyakazi wengine wa Serikali wang’atuke afisini mwao ili uchunguzi ukamilike, na wasipopatikana na makosa watarudi kazini. Nafikiria hivyo ndivyo alivyomaanisha. Baadhi ya marafiki zetu waandishi wa habari wameripoti kana kwamba watu ambao wametajwa hapa tayari imethibitishwa kwamba ni wafisadi na wameshafanyiwa kesi, wamehukumiwa na kupatikana na makosa. Ni muhimu hilo liwekwe wazi. Kuna uwezekano kwamba baadhi ya watu ambao wametoka katika afisi zao watarudi kazini wakipatikana hawana makosa. Ni muhimu sana wananchi wa Kenya wajue kwamba sio kwa sababu eti Serikali haijafanya uchunguzi wake bali ni kwa sababu hawajapatikana na makosa. Pia ningetaka EACC ianze kufanya kazi yake vile inavyofaa. Ni vibaya sana kuanza kutajataja majina ya watu. Ukiangalia katika Ripoti hii ambayo tumepatiwa, unakuta mtu anaambiwa, “wewe waziri, uliunga mkono jambo fulani”. Hakuna ushahidi au maelezo yoyote yalitoletwa yanayothibitisha kwamba katika kuunga mkono jambo hilo ulihusika katika ufisadi wowote. Unaambiwa tu kwamba una makosa kwa kuwa uliunga mkono mradi fulani au ulipitia mahali fulani. Ni muhimu sana EACC imshauri Rais katika ombi lake la kupewa Ripoti kuwa kuna watu wamepatikana na makosa na wengine wanaelekea kushtakiwa. Wale ambao wametajwa tu katika malalamiko ya hapa na pale hawafai kuorodheshwa hapa kama watu ambao wanastahili kukaa kando. Sheria inajulikana; ni lazima wapewe nafasi yao ya kujitetea. Nikimalizia, kuna ombi ambalo limeletwa hapa Bungeni la kuwataka maafisa wa tume ya kukabiliana na ufisadi, ambayo imewafanya mawaziri na maafisa wengine wang’atuke afisini mwao, kwenda nyumbani. Kama kuna watu ambao wanastahili kuondoka afisini mwao kabla ya wengine ni makamishna wa EACC. Wanafaa kung’atuka, wafanyiwe uchunguzi na Bunge na wakipatikana hawana makosa warudi. Haifai waendelee kufanya kazi katika tume hiyo."
}