GET /api/v0.1/hansard/entries/591269/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 591269,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/591269/?format=api",
"text_counter": 335,
"type": "other",
"speaker_name": "",
"speaker_title": "",
"speaker": null,
"content": "Jambo la kwanza, ningependa kutoa rambirambi zangu kama Mbunge wa Turkana ya Kati maana kuna wanafunzi wanaotoka katika eneo langu la Bunge na wanaosomea sehemu hiyo. Ningependa kutuma rambirambi zangu kwa familia ambazo zimepoteza watoto wao. Jambo la pili ni kwamba maisha yaliyopotea ni maisha ambayo yalikuwa na matumaini makubwa katika nchi hii. Wazazi wao na nchi pia ilikuwa imewaangalia kwa njia moja au nyingine kuleta tofauti, maendeleo au kuleta elimu yao kubadilisha maisha ya wazazi wao na kutumikia wananchi wa Kenya. Jambo la askari kutumia silaha zaidi ya wale watu ambao wanaenda kukubaliana nao limekuwa jambo ambalo tumerudia mara nyingi. Hao wanafunzi hawakuwa na silaha wala hawakutisha maisha ya askari kiwango cha kutumia risasi kuwaua. Kisheria, maisha ya askari pia inalindwa, lakini ni lazima pia askari aone adui ama mtu ambaye anakabiliana naye kama yuko na silaha ama hana ili ajue jinsi ya kukabiliana naye. Imefika wakati ambapo lazima askari wetu waende wapate mafunzo na elimu jinsi ya kutumia silaha, kwa maana mtu anapoajiriwa katika kazi ya askari wengine wanaishi miaka mingi bila kuenda kwa mafunzo au kwa elimu ya kujua kuendeleza kazi yake mbele. Imefika wakati ambapo askari akiua mtu, naye pia lazima aadhibiwe vikali ili iwe mfano kwa wengine. Kila mara askari anapoua mwanafunzi ama mtu yeyote kesi hiyo inaenda polepole mpaka “inakufa”. Hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya askari huyo. Ningependa kuona kwamba wanaohusika na vifo vya hao wanafunzi wamepatikana na mkono wa sheria ili nao wapitie uchungu ambao wazazi wa hao wanafunzi wanapitia sasa. Licha ya hayo kuna mambo ambayo pia yanachangia mambo hayo kutendeka katika vyuo vyetu. Jambo la kwanza ambalo Mhe. Millie Odhiambo amesema ni ukabila. Ukabila umezidi katika vyuo vyetu vikuu. Utakuta kwamba kuanzia juu mpaka katikati ni kabila moja. Wakati kuna jambo ambalo limetokea katika vyuo, utaona kwamba linahusu kabila majo ambalo pengine wanabishana kisiasa na lingine; utaona kabila hili likifukuzwa ndiyo chanzo cha mambo yanayotendeka katika chuo. Tuangalie mambo hayo. Ni lazima makabila yote yawakilishwe katika chuo kikuu kuonyesha sura ya Kenya kwa maana tuna makabila zaidi ya 40. Ni lazima katika vyuo vyote, kama mmoja ni wa kabila fulani, wa pili awe wa kabila lingine. Kuna siasa kutoka nje ambazo zinaingia kwenye vyuo. Sisi kama wanasiasa, tunaleta siasa za vyama na kuziinginza kwa wanafunzi. Hili ni jambo linalochangia wanafunzi kugawanyika na kuwa na ule mtindo wa kuchukiana na kuanza ukabila wakiwa bado shuleni."
}