GET /api/v0.1/hansard/entries/71123/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept

{
    "id": 71123,
    "url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/71123/?format=api",
    "text_counter": 333,
    "type": "other",
    "speaker_name": "",
    "speaker_title": "",
    "speaker": null,
    "content": "Sisi tunaelewa kwamba kama kuna Mpokot anamwibia Mturkana, basi anamwibia ndugu yake. Mbali na kwamba wameibia ndugu zake, vita vikitokea wanauana. Kwa hivyo, wanasema kwamba wameua Wapokot, Wamaasai, Wakamba na Wakikuyu na hawakuua mtu. Ni dhahiri kuhakikisha kwamba tunarudi katika sehemu zetu na kuanza na naibu wa chifu, chifu na Mkuu wa Wilaya ili wafanye mikutano na kuwaambia watu kwamba tunawaongoza ili wasifikirie kwenda kuiba kwa sababu hii ni hatia. Bi. Naibu Spika wa Muda, kuna watu wanaona kwamba watu wao wanaiba na hawatambui kwa sababu ya kura. Mara nyingi anataka kumkinga huyo mtu ili ampigie kura. Kesho yake yeye ndiye atakuwa mtu wa kwanza kufika katika ofisi ya Serikali kusema kwamba kuna wizi. Tena, Serikali inapochukua hatua, wanasema kwamba wale wezi wako na silaha kali, na wanaponyang’anywa hizo silaha, watu hao wanawaita vijana wetu wa polisi “hawa maaskari”. Hao askari ni watoto wetu na walinda usalama. Hawa ni watu ambao wanatumia amri ili kuhakikisha sheria inafuatwa. Baada ya hayo yote kufanywa, tunakuja hapa bungeni na kusema mambo matamu ya kupendeza kwa kusema kwamba ukoo wangu unalinda wanyama. Tulikuwa tunaambiwa kwamba ukiwekea Maasai shilingi milioni moja upande mmoja na upande mwingine uweke ng’ombe kumi na umuulize achague moja, atachagua ng’ombe kumi na wala sio hizo pesa. Wakati huo, milioni moja ilikuwa kama bilioni moja. Lakini tumetoka wakati huo. Kila mwananchi nchini amepata elimu na wale ambao hawajapata tuko hapa na tutawapelekea ujuzi na mambo yanayoeleweka na kuwaambia kwamba mlango wa kwenda mbele ni huu. Ndugu zangu na dada zangu, tuwache mambo ya kutaniana. Tuwache kuona kwamba Serikali itakuja kulinda boma lako na wala si yule mwingine. Amani na usalama huanza na sisi wananchi kabla Serikali ije kuangalia wale waliovunja sheria. Lakini sisi kama viongozi jukumu letu ni nini? Ni kusifia, kukinga, kulinda, kuzuia madhara yasionekane na tuache kasheshe. Ni lazima tulenge mambo sasa na kwa kidhahiri. Sasa ninaamini kwamba ni sisi viongozi tutaweza kusimama kwenye umati na kuwaambia watu kwamba kuiba mali ya mtu, kutusi mtu au kuvunja sheria ni vibaya. Shida ambayo tuko nayo katika nchi hii ni kuvunja sheria bila heshima. Tunavunja sheria kama tunavyovunja bakuli la uji. Hatuna heshima kwa sheria. Ni lazima tuiheshimu sheria ndiposa wenzetu waweze kutufuata. Tukifanya hivyo, tutasimamisha wizi wa ng’ombe, mbuzi na hata wizi wa benki. Wengine wanaambiwa kwamba kuiba benki ndiyo njia ya mwanamme kutajirika na huku ameiba na kuumiza watu. Inafaa sisi Wabunge tuchunge sana kwa sababu sisi ndio tunatumiwa vibaya kwa sababu mtu atakuja kwako na kukuambia kwamba mtoto amekamatwa bure bila kuiba na kwamba alikutana na polisi akienda nyumbani na akachukuliwa. Wengine wanasema kwamba ng’ombe walichanganyika na wengine na wakachukuliwa. Kwa nini hawakuchukuliwa upande wa kaskazini mwa Kenya, bali walichukuliwa upande wa kuzini. Hii ni kwa sababu pale kulikuwa na mwizi aliyetekeleza hayo. Kwa nini huyo alikamatwa usiku na mwingine hakukamatwa akiwa katika nyumba yake? Hii ni kwa sababu yule aliyekutana na polisi usiku alikuwa ni mwizi. Lakini sisi ndio watu wa kwanza kukataa sheria na kuwaita vijana wa idara ya polisi majina. Wakati wa kuajiri, sisi ndio watu wa kwanza kusema kwamba niandikie mtoto katika idara ya polisi au jeshi. Lakini akiingia huyo, tunamwita “huyu askari”. Lazima tuwe na tabia na lugha nzuri na tuchunge midomo yetu na sheria. Kwa hayo machache, ninaomba kuunga mkono ripoti hii."
}