GET /api/v0.1/hansard/entries/764989/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 764989,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/764989/?format=api",
"text_counter": 207,
"type": "speech",
"speaker_name": "Hon. King’ara",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 13468,
"legal_name": "Simon Nganga Kingara",
"slug": "simon-nganga-kingara-2"
},
"content": "Ahsante sana, Mhe. Naibu Spika wa Muda kwa jicho lako zuri lililoniona na kunipatia fursa hii. Kabla sijaongea lolote, ningekuomba unipatie fursa niweze kuomboleza na jamaa na marafiki wa Daktari Gakuru, ambaye alikuwa rafiki yangu. Hata alinialika nihudhurie sherehe za Mashujaa Day kule Nyeri. Tulikuwa na yeye kule Nyeri na tukaongea mengi kuhusu maendeleo ya Kenya yetu tunayoipenda. Jamaa wa Ruiru wote wanaomboleza na familia yake pahali popote walipo. Hilo ni pigo kubwa kwa nchi yetu ya Kenya. Kama watangulizi wangu walivyoongea, ni vizuri tuwaheshimu viongozi wetu wakati wanapopata majanga kama haya. Nikigusia mjadala wa leo, ningependa kusema kuwa ni mjadala mwafaka zaidi hasa katika eneo ninalotoka la Ruiru. Katika nchi nyingi za Afrika, kuna uhamiaji wa watu kutoka mashambani kuelekea mijini. Haraka ya kwenda mjini inakuwa ya mwendo wa kasi kuliko haraka ya kutengeneza mazingira ya wale watu wanaokuja mjini. Hii ni hasa wakati tumetengeneza barabara kuu kama hii ya Thika na barabara nyingine za kando. Watu wanatoka mijini na kuhamia karibu na barabara zile. Kama wengi walivyosema hapa, unakuta kwamba hatuwekei uzito mambo muhimu katika maisha ya binadamu kwa sababu labda hatuna mjadala kama huu wa kuweka utaratibu mwafaka wa kuleta maendeleo ya watu waliokuja pale. Mambo kama ya usalama yamekuwa yakizorota kwa sababu watu wamekuja wengi na hakuna polisi na utaratibu wa maji taka. Unaona kwamba tunapata janga la magonjwa makali kama kipindupindu na mengineyo. Tukichukua mwelekeo mpya wa kuweka utaratibu katika uhamiaji wa watu kutoka mashambani kwenda katika miji mikuu, utakuta kuwa maeneo ya mashambani yatakuwa yamehusishwa katika maendeleo kutokana na ugatuzi. Kwa nini nimesema hivyo? Mhe. Naibu Spika wa Muda, unajua tumepata ugatuzi na miji sio ile miji mikuu kiongozi wa mjadala huu ametaja, bali hata maeneo ya ndani. Vile sasa tuko na kaunti na kaunti ziko na fedha zake, utakuja kukuta kuwa hata huko kutakuja kuwa na miji mikuu. Kwa hivyo, wakati tunajadiliana na kutafuta mwelekeo wa mjadala huu, ni vizuri tukumbuke ugatuzi na kujua kuwa maeneo kama Turkana yatakuwa na miji mikuu na ni vizuri tuweke uzito katika maendeleo ya watu watakaokuwa katika miji ile. Mengi yatasemwa yatakayogusia utaratibu wa kuishi kwa watu lakini bila mikakati kuwekwa, tutakuwa tunaongea jambo moja likifuatwa na lingine na tutakuwa tunajirudia. Kuna mambo ambayo yamekuwa yakijirudia katika miji. Kuna shida ambazo zimekuwa zikijirudia. Kukinyesha, unakuta tunakimbia kujaribu kutafuta mwelekeo wa kuishi lakini tukiweka mikakati, haya yatakuwa mambo ya kupita na sisi tutaendelea mbele na tutakuwa na misimamo itakayotufanya tuonekane tumekomaa kama wanasiasa waliochaguliwa na wananchi. Majukumu yetu yatakuwa ya kufaa wakati tumepewa kazi na tuje Bungeni na kutekeleza yale yametufanya tuje hapa. Tunaweza sema haya yote, lakini tusipochukua jukumu la kuyatimiza, itakuwa ni maneno tu ya bure na mwelekeo hautapatikana. Mjadala huu uko na uzito na upatiwe kipaumbele."
}