GET /api/v0.1/hansard/entries/90920/?format=api
HTTP 200 OK
Allow: GET, PUT, PATCH, DELETE, HEAD, OPTIONS
Content-Type: application/json
Vary: Accept
{
"id": 90920,
"url": "https://info.mzalendo.com/api/v0.1/hansard/entries/90920/?format=api",
"text_counter": 213,
"type": "speech",
"speaker_name": "Mr. Muthama",
"speaker_title": "",
"speaker": {
"id": 96,
"legal_name": "Johnson Nduya Muthama",
"slug": "johnson-muthama"
},
"content": "Ahsante sana Bw. Naibu Spika wa Muda. Ninasimama kuchangia Hoja hii ya maana sana ambayo inahusu mifugo ambayo ni nguzo ya uwezo wa mwananchi wa kawaida. Ni dhahiri kwamba lazima Waziri achukue jukumu la kuhakikisha kwamba masilahi, mahitaji, na raslimali za wananchi zimelindwa kupitia Wizara hii. Jambo lililofanya mambo ya mifugo kuwa hatari ni wizi. Hii Wizara inaweza kushirikiana na Wizara inayohusika na mambo ya ulinzi wa ndani kuona kwamba wananchi na mali yao wanalindwa. Haifai, katika nchi huru kama Kenya ambayo ina watu walioelimika, kuona mtu akienda kuchukua mali ya mwenzake na kuyaweka kwake. Ninazungumzia hasa kuhusu mifugo. Tumefikia kiwango cha kuzungumza na wezi wa mifugo. Ni lazima Waziri ahimize na asisitize kwamba hii Wizara ni ya Serikali na inayo wafanyakazi wanaolipwa na Serikali. Hii Wizara vile vile inalinda mali ya wananchi na kwa hivyo wezi wa mifugo lazima wapewe adhabu kubwa. Mambo ya mifugo haihusu wafugaji peke yao. Ukitembea kote nchini, utagundua kwamba katika asili ya Mwafrika ng’ombe, mbuzi na wengineo ni raslimali kubwa na inatiliwa maanani sana. Hawa mifugo ni mali na haki yao. Kamwe hakuna mtu anayeweza kuishi bila ng’ombe. Mimi sina shamba la kufuga mifugo lakini siwezi kukosa ng’ombe mmoja kuashiria kwamba mimi ni Mwafrika. Kwa hivyo, tunataka maslahi haya yaangaliwe kwa kindani na si kwa wafugaji tu bali kwa Wakenya wote. Ninaomba Wizara hii ihakikishe kwamba wananchi wa kawaida wanapata dawa za kutibu mifugo wao. Imekuwa vigumu kwa mtu kupata matibabu ya mifugo hasa katika mtindo wa zero grazing. Katika huu mtindo wa ufugaji wa zero grazing ndipo unaona kiini na uwezo wa Mwafrika. Ng’ombe huyo wa kukamuliwa maziwa hutoa mapato kwa familia kubwa na jamii nzima. Mfugaji yule hawezi kutoka pale kijijini kuja mjini kutafuta kazi. Yeye atajimudu na mapato anayopata kutokana na maziwa ya ng’ombe. Vile vile ufugaji huu unatusaidia na nyama. Utakuta kwamba watu katika eneo hilo hawaendi mbali kutafuta nyama. Ni jukumu la Waziri kuangalia hali ya mifugo kama vile mbuzi, kondoo nakadhalika. Ngamia amekuwa mnyama wa maana sana. Nyama ya ngamia ina bei ghali. Nyama hiyo inategemewa na inahitajika sana. Ni sisi tu tunaona kwamba kula nyama ya ngamia ni dhambi. Huyu ni mnyama ambaye hustahimili ukame na hali yoyote ile. Kwa hivyo, hatusemi kwamba ni Mkoa wa Kaskazini Mashariki pekee unaoweza kumudu ufugaji wa ngamia. Tungempenda Waziri awahimize wananchi wafuge ngamia ili waweze kujimudu. Ngamia anaweza kukaa miezi miwili bila kuhitaji maji huku akisaidia jamii nzima. Sisi tunamshukuru Rais kwa kuiunda na kuisaidia Wizara ya Mifugo ili iweze kujisimamia vilivyo. Kwa hayo machache ningependa kuunga mkono."
}